Sunday 27 March 2016

JENERALI MWAMUNYANGE AMPONGEZA DK. SHEIN

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania (JWTZ), Jenerali  Davis  Mwamunyange, amemtumia salamu za pongezi Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kuchaguliwa tena kushika wadhifa huo kwa muhula wa pili.

Katika salamu hizo zilizotumwa na Jenerali Mwamunyange kwa niaba ya  maofisa, askari na watumishi wa umma, wanaofanya kazi JWTZ, alieleza kuwa ushindi wa kishindo wa Dk. Shein unadhihirisha kuwa, Wazanzibar wameridhishwa na uongozi wake.

Jenerali Mwamunyange amesema historia ya Dk. Shein ya uaminifu, maadili mema na uzalendo, aliouonyesha katika utumishi wake wa muda mrefu kwenye nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika, kabla hajawa rais, imewapa wananchi imani kubwa kuhusu uongozi wake.

Aidha, salamu hizo za pongezi zilieleza kuwa JWTZ inamuhakikishia Dk. Shein kuwa, itaendelea na utiifu, uadilifu na  uaminifu mkubwa kwake kama ilivyo desturi ya majeshi ya hapa nchini.

Salamu hizo pia zilimtakia Dk. Shein afya njema na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kumuongoza katika kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa.

Wakati huo huo, Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Zanzibar, Abood Jumbe Mwinyi, amemtumia salamu za pongezi Dk. Shein kwa ushindi wa kishindo alioupata katika marudio ya uchaguzi wa Zanzibar.

Mzee Jumbe pia ametuma salamu hizo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na mgombea wake kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.

Wakati huo huo, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), umempongeza Dk. Shein kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Zanzibar.

Katibu Mkuu wa umoja huo, Amina Makilagi, katika salamu zake, alisema wana imani kubwa na Dk. Shein na kwamba, utendaji wake, umeifanya CCM iendelee kuaminiwa na wananchi wa Zanzibar.

Alisema ni ukweli usiopingika kuwa, Dk. Shein ni kiongozi makini na ushindi alioupata umedhihirisha utendaji wake uliotukuka.

No comments:

Post a Comment