Sunday 27 March 2016

SERIKALI YATAKA ORODHA YA WATUMISHI HEWA MACHI 30




WAKUU wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmshauri nchini, wametakiwa ifikapo Machi 30, mwaka huu, wawe wamewasilisha taarifa za watumishi hewa kwenye vituo vyao vya kazi ili zikabidhiwe kwa Rais Dk. John Magufuli.

Hatua hiyo ni mkakati wa serikali kuhakikisha watumishi hewa wanaondolewa ili kuokoa fedha zinazotumika kuwalipa mishahara.

Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Geogre Simbachawe, wakati akizungumza na gazeti hili, kuhusiana na juhudi zinazofanywa na wizara yake kumaliza uwepo wa watumishi hewa, hususan kwenye halmashauri mbalimbali nchini.

Alisema tayari ameshawaandikia barua wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri ili kuwasilisha ofisini kwake, orodha ya watumishi hewa ili ikabidhiwe kwa rais kwa hatua zaidi.

Alisema mishahara hewa ni wizi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali, ambao sio waaminifu, hivyo amewataka wakurugenzi na waweka hazina wa halmashauri zote kumaliza tatizo hilo haraka iwezekanavyo.

“Tutahakikisha  tatizo hilo tunalikomesha mara moja ili kuhakisha tunaokoa  fedha nyingi za serikali zilizokuwa zinapotea,’’  alisema.

Alisema tatizo la  watumishi hewa na mishahara haliko kwa  walimu tu, bali kwa watumishi wengi wa serikali.

Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu, Rhoda Ezekiel, ameripoti kutoka Kigoma kuwa, Mkuu wa mkoa huo, Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga, amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa, kuhakikisha wanafanya uchunguzi juu ya kiasi cha fedha kilichotumika kuwalipa mishahara watumishi hewa 169, kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari, jana, Maganga alisema ametoa agizo hilo ikiwa ni itekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kufanya uhakiki wa watumishi katika halmashauri zote nchini, ili kuwabaini watumishi hewa wanaolipwa mishahara kinyume na taratibu za utumishi.
Alisema kati ya watumisho hao 169, waliowabaini kuwa ni hewa, wapo ambao walishafukuzwa kazi, waliokwishafariki na wengine hawana sifa za kuwa watumishi wa umma.
Maganga alisema suala la kuwa na wafanyakazi hewa ni wizi, ambao hauwezi kuvumilika na pia ni wizi wa kuibia wanyonge hivyo hauwezi kuvumilika.
"Hakuna anayeweza kuvumilia wizi wa waziwazi kiasi hiki unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu, wale wote watakaobainika wajiandae kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao," alisema.
Alisema fedha walizokuwa wakilipwa watumishi hao hewa kwa ajili ya mishahara, zinatakiwa kurudi zote na pia wakurugenzi wawafute watumishi hao hewa kwenye orodha ya malipo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema katika serekali ya awamu ya tano, hakuna kufanyakazi kwa mazowea na uzembe na kwamba, kila mtumishi atumike kwa nafasi yake aliyopo.
Alizitaja halmashauri zenye watumishi hewa kuwa ni Kasulu (78), Kigoma (23), Manispaa ya Kigoma Ujiji (29), Buhigwe (11), Uvinza (19), Kibondo (5), ofisi ya mkuu wa mkoa (4).

No comments:

Post a Comment