Tuesday 12 April 2016

MKUU WA GEREZA LINDI AWEKWA KIKAANGONI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mmoja wa wafanyabiashara katika soko kuu la wilaya ya Ruangwa, wakati akikagua hali ya upatikanaji wa vyakula na bei za mazao, juzi.
SERIKALI imemtaka Mkuu wa Magereza mkoa wa Lindi, kuhakikisha hakuna mtuhumiwa wa dawa za kulevya atakayetoweka katika gereza la mkoa huo.
Imesema kuna watuhumiwa wa dawa za kulevya, ambao wanahifadhiwa katika gereza la mkoa wa Lindi, hivyo ni vyema akajiridhisha kama ulinzi na usalama wa watuhumiwa hao umeimarishwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema hayo juzi, wilayani Ruangwa, wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Lindi, iliyowasilishwa kwake na mkuu wa mkoa huo, Godfrey Zambi.
Alimtaka mkuu wa gereza hilo kuwa makini na baadhi ya zabuni wanazozitoa kutoka nje na kuhakikisha ulinzi unaimarishwa wakati wote gerezani hapo.
“Mkuu wa magereza wa mkoa atembelee gereza, ambalo wanashikiliwa watuhumiwa wa dawa za kulevya na aangalie mradi unaolenga kupeleka maji gerezani hapo kama ni kweli au njia,” alisema.
Alimtaka mkuu huyo wa magereza kujiridhisha kama ulinzi na usalama wao umeimarishwa na kuhakikisha hakuna mtuhumiwa anayetoweka.
Awali, akisoma taarifa kwa Waziri Mkuu Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zambi alisema matumizi ya dawa za kulevya, hususan kwa vijana, ni miongoni mwa changamoto zinazoukabili mkoa huo, ambapo wilaya ya Kilwa inaongoza kwa kuwa na waathirika wengi.
Zambi alisema matumizi ya dawa hizo yanasababisha kupungua kwa nguvu kazi kwani watumiaji wengi ni vijana, hivyo alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kupiga vita matumizi ya dawa hizo kwa kuwafichua wauzaji na watumiaji.

Barabara ya Ruangwa-Nachingwea
 kujengwa kwa kiwango cha lami


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali inatarajia kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Nanganga, Ruangwa hadi Nachingwea.
Amesema hatua hiyo itawezesha kutatuliwa kwa kero ya changamoto ya miundombinu ya barabara, inayowakabili wananchi wa wilaya za Ruangwa na Nachingwea kwa muda mrefu.
Majaliwa alisema barabara hiyo, ambayo kwa sasa haipo katika hali nzuri, itajengwa kwa kiwango cha lami, ambapo serikali inatarajia kuanza kuifanyia upembuzi yakinifu katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Waziri Mkuu alisema hayo juzi, kwa nyakati tofauti, alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Likunja, Nkowe na Namahema, katika mikutano ya hadhara aliyoifanya wilayani Ruangwa, akiwa kwenye ziara ya kikazi.
Alisema serikali imejipanga kuboresha miundombinu ya barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwamba, mara baada ya kumalizika kwa upembuzi yakinifu, ujenzi wa barabara hiyo utaanza, hivyo amewataka wananchi kuwa na subira.
Katika hatua nyingine, Majaliwa aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuweka kando itikadi zao za kisiasa, kwa sababu uchaguzi ulimalizika tangu Oktoba 25,mwaka jana.
“Mimi nitaendelea kuwaheshimu, kuwasikiliza na kuwahudumia. Nawaomba tushirikiane na tuweke kando masuala ya itikadi za vyama, sasa ni wakati wa kazi, hivyo ni bora tukashirikiana kufanya kazi kwa maendeleo ya Ruangwa, jambo ambalo linawezekana,” alisema.
Aliongeza: “Hata kama wewe, ambaye najua ulinichukia mimi, nimekusamehe kutoka moyoni, wewe ni wangu hata kama hukunichagua, nitakuhudumia na kukutumikia kwa sababu mimi ndiye mbunge wako, hivyo naomba tushirikiane.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Rashid Nakumbya, aliwaomba wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya wilaya yao ili hatimaye iweze kupiga hatua.

Wakurugenzi wasiotenga asilimia 10
 za vijana na wanawake kutimuliwa


SERIKALI imesema mkurugenzi yeyote wa halmashauri hapa nchini, atakayeshindwa kutenga asilimia 10, ya mapato kwa ajili ya wanawake na vijana ataondolewa.
Imesema suala la kila halmashauri kutenga asilimia 10, ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi ni la lazima na si hiari.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema hayo juzi, alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kitandi, Mtimbo, Likunja, Nkowe na Namahema, ambako alifanya mikutano ya hadhara.
“Halmashauri ambayo itashindwa kutenga asilimia 10, kwa maana asilimia tano kwa ajili ya vijana na tano kwa ajili ya kinamama, mkurugenzi wake atakuwa anatafuta safari,” alisema.
Majaliwa yupo wilayani Ruangwa mkoani Lindi kwa ajili ya ziara ya kikazi, inayolenga kukagua shughuli za maendeleo, ambapo aliwasisitiza wakurugenzi wa halmashauri nchini kutimiza wajibu wao na serikali haitamvumilia yeyote atakayeshindwa kufanya hivyo.
Awataka wananchi kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili zitakapofika sh. milioni 50, za kila kijiji, zilizoahidiwa na Rais, Dk. John Magufuli, waweze kunufaika.
Alisema fedha hizo, ambazo zitatolewa kuanzia Julai, mwaka huu, zitagawiwa katika vikundi mbalimbali vilivyosajiliwa na si kwa mtu mmoja mmoja, hivyo amewataka watendaji wa kata na vijiji kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi.

No comments:

Post a Comment