Thursday, 4 August 2016

VYUO VITANO VYAFUTIWA USAJILI, VIBALI VYA VYUO 112 VYA UFUNDI VYAFIKIA UKOMO




BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), limesitisha mafunzo kwenye vyuo vitano na kuvifuta kwenye orodha ya usajili ya vyuo vya ufundi nchini.

Vyuo hivyo ni Zoom Polytechnic College, Tabitha College, State College of Health and Allied Sciences, Financial Training Centre na TMBI College of Business and Finance vyote vya jijini Dar es Salaam.

Kufutiwa usajili kwa vyuo hivyo kumeambatana na onyo la siku 14, kwa vyuo 41, vinavyotoa elimu ya ufundi bila kusajiliwa kwa mujibu wa sheria, kujisajili mara moja kwenye baraza hilo kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha, vibali vya usajili wa vyuo 112, vya kutoa elimu ya ufundi vimeelezwa kuwa vimefikia ukomo, hivyo vyuo husika vinapaswa kutekeleza masharti ya usajili huku vyuo 57, vimefikia ukomo wa ithibati na kutakiwa kutekeleza masharti ya ithibati.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, ofisi za makao makuu ya baraza hilo, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NACTE, Mhandisi Steven Mlote, alisema pamoja na maamuzi hayo ya baraza, pia limetoa mwezi mmoja kwa vyuo 112, kutekeleza masharti ya usajili.

Alisema vyuo 52, vinatakiwa kutekeleza masharti ya ithibati kwa mujibu wa sheria za uendeshaji vyuo vya ufundi nchini, ambapo vyuo vitakavyoshindwa kutekeleza maagizo hayo, vitafungiwa na kufutwa kwenye orodha ya vyuo vya ufundi kwa mujibu wa sheria.

"Vyuo 41 vinavyotoa elimu ya ufundi bila kusajiliwa kwa mujibu wa sheria nimevipa wiki mbili na ninavitaka vijisajili mara moja kwenye baraza kabla ya hatujavichukulia hatua kali za kisheria.

"Jumla ya vyuo 175, tutavishusha hadhi yake endapo havitatekeleza maagizo tuliyoyatoa ndani ya muda husika," alisema.

Mlote alivitaja vyuo ambavyo havijasajiliwa, lakini vinaendesha programu zisizo na kibali cha baraza (na mkoa viliko kwenye mabano) kuwa ni King Solomoni College (Arusha),  Avocet College of  Hotel Management (Arusha), Kewovac Nursing Training Centre (Dar es Salaam) na St. Family Health Training Institute cha Dar es Salaam.

Vingine ni Bethesda Montessori Teachers Training College (Arusha), Green Themi Teacher’s College & Green Themi Institute of Tourism, Mainland Institute of Professionals (Arusha), St. David College of Health (Dar es Salaam), Islamic Culture School (Dar es Salaam), Tanzania Education College (Dar es Salaam) na Macmillan Training College (Dar es Salaam).

Vingine ni Tanzania International University (TIU) cha Dar es Salaam, Dodoma College of Business Management (Dodoma), Faraja Health and Emergencies (Mbeya), St. Joseph College (Mbeya), St. Peter Health Management (Mbeya), Kapombe Nursing School (Mbeya), Uyole Health Institute (Mbeya),  Josephine Health Institute (Mbeya) na Institute of Public Administration (Chake Chake Pemba).
   
Mwenyekiti huyo alivitaja vingine kuwa ni Dar es Salaam College of Hotel and Business Studies (Unguja), Zanzibar and Chake Chake College (Zanzibar),  Zanzibar Training Institute, the Professional College of Information Technology, Languages and Business Studies (Zanzibar), Azania College of Management (Zanzibar), Time School of Journalism (Pemba) na Residence Professional College (Zanzibar).

Vyuo vingine ni Mkolani Foundation Organisation (Mwanza), Kahama College of Health Sciences (Kahama), Institute of Adult Education (Mwanza), Zoom Polytechnic (Bukoba), Johrow Star Training College (Shinyanga) na St. Thomas Training College (Shinyanga).

Dar es Salaam School of Journalism and Mass Communication DMSJ (Bukoba), Dar es Salaam School of Journalism and Mass Communication (Mwanza), Dar es Salaam School of Journalism and Mass Communication (Geita)  na Dar es Salaam School of Journalism and Mass Communication (Simiyu).

Alihitimisha kwa kuvitaja Harvest Institute of Health Sciences (Mwanza), Singin International (Bukoba), College of Business Management (Zanzibar), Tanzania Star Teachers College (Pemba), Tanzania Star Teachers College (Zanzibar) na St. Mary's International School of Business (Sumbawanga).

Baadhi ya wadau wa elimu ya ufundi wakiwemo wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya stashahada ya taaluma tofauti mkoani Dar es Salaam, baada ya kikao hicho, walisema uamuzi huo wa NACTE ni mzuri kwa lengo la kuboresha taaluma, lakini kwa upande mwingine unawaumiza wanafunzi wasio na hatia.

Walisema umakini ndani ya NACTE unatakiwa uwepo katika hatua za awali za usajili wa vyuo hivyo, ili visiruhusiwe kufanya usaili wa wanafunzi kabla ya kukamilisha matakwa ya Baraza.

No comments:

Post a Comment