NA
SOLOMON MWANSELE, MBOZI
MGOMBEA
Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, amesema endapo atachaguliwa kwenye uchaguzi
mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, atahakikisha anajenga barabara za kiwango cha
lami, zenye urefu wa kilometa 10 katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi.
“Kwa hiyo nitapoteuliwa kuwa rais, kazi yangu ya kwanza ni kuja kutengeneza kilometa 10 za lami hapa Vwawa. Mbunge mtakayemchagua kupitia CCM atachagua ni maeneo yapi yapewe kipaumbele, ili mji huu uweze kuwa na maendeleo zaidi,” alisema Dk. Magufuli.
Aliyasema hayo jana wakati akihutubia mamia ya wakazi wa mji huo na vitongoji vyake waliojitokeza kwa wingi kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa michezo uliopo Vwawa mjini.
Dk. Magufuli alisema anafahamu baadhi ya watu watasema hizo ni ahadi tu na yeye kosa lake kubwa hapa duniani anapoahidi huwa anatekeleza na kwamba anafahamu mji huo una matatizo ya maji.
Mgombea
urais huyo wa CCM aliongeza kuwa wakazi wa mji huo wanatumia maji ya mbubujiko
na wakati wa mvua maji hayo yanakuwa machafu, anafahamu hilo na kwamba kama
ameweza kutengeneza kilometa zaidi ya 17,000 kwa nchi nzima, hawezi kushindwa
kujenga visima vya maji.
“Naomba mnipe urais ili nilisimamie eneo hili. Changamoto ni nyingi, unakuta mama ntilie anasumbuliwa, wanafanya biashara vikodi vya hovyo hovyo tu, unakuta mtu una bodaboda mara ushikwe, haya mambo madogo madogo mniachie nitayamaliza,” alisema.
Aliongeza
kuwa akichaguliwa kushika nafasi hiyo, atakuwa rais wa vyama vyote, iwe
wanachama wa CCM, TLP, CUF, CHADEMA, UDP ama wale ambao hawana chama.
Alisisitiza kuwa atakuwa rais wao kwa sababu maendeleo hayana ubaguzi.
Akizungumzia changamoto ya elimu, Dk. Magufuli alisema bahati nzuri kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM imesisitiza hilo, hivyo kuanzia mwakani mwanafunzi kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne hatalipa ada bali atasoma bure.
Alisema anayasema hayo kwa sababu anao uwezo na kwamba fedha nyingi za serikali zimekuwa zikitumiwa hovyo na wakubwa na kwamba amekaa serikalini miaka 20, hivyo anafahamu hiyo mirija.
“Serikali nitakayoiunda itakuwa serikali ya watu makini, hakuna cha mchakato, hakuna cha kuja kesho.Mawaziri wangu nitawataka wafanye kazi kwa ajili ya watu, siyo kufanya kazi kwa ajili ya wao,” alisema Dk. Magufuli na kushangiliwa.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, Tanzania inayo makabila zaidi ya 121 na dini tofauti, lakini imeendelea kukaa salama na kwa umoja. Aliwashukuru viongozi waliotangulia, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na hadi sasa Rais Jakaya Kikwete.
Dk. Magufuli
alisema viongozi hao walijenga mazingira ya Watanzania kuwa wamoja, salama na yeye
ataendeleza umoja na mshikamano wa Watanzania na kwamba hatawabagua kutokana na
maeneo wanayotoka au dini walizonazo, anataka awe rais wa watanzania wote.
Aliongeza kuwa hiyo ndio Tanzania anayotaka kuijenga, ikiwa na mabadiliko yaliyo bora na kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania wote.
No comments:
Post a Comment