Thursday, 27 August 2015

DK. MAGUFULI, SAMIA NA SAFARI YA USHINDI





Na Dk. Muhammed Seif Khatib

DK. John Pombe Magufuli rubani wa anga na Samia Suluhu Hassan rubani mwenza wa ndege ya kivita ya Chama Cha Mapinduzi ‘CCM MIG 35’ jana katika uwanja tambarare wa Jangwani wameipaisha ndege yao katika mapambano ya dhidi ya ‘choppers’ za wapinzani. 
Ili kuilinda  dola safari hii ya ushindi ya rubani Magufuli kipenzi cha Watanzania, unafata nyayo za watangulizi wake waliorusha ndege ya ushindi katika kiwanja cha Jangwani kwa vipindi vinne vilivyopita kuanzia mwaka 1995 hadi 2000 Rais Mkapa na mwaka 2005 na 2010 kwa Rais Kikwete. 
Jana Rubani Dk. John Magufuli alifanikisha kuanza safari hii ya ushindi.  Kwa kuwa wengine wanayo ‘Safari ya Matumaini’ ambayo  haina hakika, rubani Magufuli ameanza safari jana huko Jangwani.  Kwa  kuwa safari ni ya  uhakika imebatizwa na kupewa jina “SAFARI YA USHINDI”.  Zipo sababu kadhaa zitakazompa  rubani Magufuli ushindi.
Rubani atafanikisha safari yake kwa vile nafasi hii ya urubani hakupewa kwa hisani au kuinunua kwa fedha. 
Ameipata kwa sababu aliingia katika ushindani mkubwa watu arubaini walichujwa katika vikao halali vya chama chake na kubaki watano.  Yeye na wenzake walipigiwa kura na wakabaki watatu.  Mkutano Mkuu wa chama chake wenye wawakilishi kutoka nchi nzima wakawapigia kura wagombea watatu yeye hatimaye akaibuka kuwa mshindi.
Mapema katika mchakato wa kusaka wadhamini, yeye  alitafuta wadhamini kwa kufata taratibu, kanuni na maadili ya chama. Hakuwa  na wapambe,  wapiga debe au wapiga mapipa. 
Hakutumia fedha wala vitu kuhonga ili avutiye  wadhamini. Hakuwakumbatia  wafanyabiashara, mafisadi ili watumiye fedha zao.  Hakuwarubuni waandishi wa habari ili wamjenge na kumtukuza ili wamwone bora kuliko wengine. 
Hakujenga mitandao ndani ya chama au ndani ya umma ili aonekane kuwa yeye ni bora kuliko wengine wote.  Yeye alijiamini kwa usafi wake, uadilifu wake na utendaji wake uliotukuka.  Kwake kutaka urais hakujawa na “kufa na kupona”.  Ushindi wake  ndani ya chama haujawa wa ghiliba, mizengwe au ufisadi. 
Rubani Magufuli anaingia katika mbio za urais akiwa hana tone ya tuhuma za ufisadi au rushwa.
Hana fedha nje wala malimbikizo  ya mali ya kufuru katika muda wote wa uongozi wake. Hakuna  chombo chochote kilichomsema kwa tuhuma za ufisadi au rushwa.  Hakuna kiongozi yoyote, mahali popote alipofungua mdomo wake na kumtaja rubani huyu kwa  chembe ya ufisadi.  Hata katika  mijadala ya Bungeni kwa miaka yote, hakuna kiongozi wa upinzani aliyefungua kinywa chake na kumhusisha na tuhuma ya rushwa. Vimbunga na tofani za ‘Richmond’, EPA na ‘ESCROW’, rubani huyu  hayumo.
Katika  muda wake wa kampeni rubani huyo hatapata taabu ya kujisafisha katika majukwaa au viongozi wenzake kumkungia kifua kwa madhambi na uchafu uliomzunguka. Hana!

Hata wapinzani, watashindwa kumnyoshea kidole kwa chembe ya uovu.  Safari yake itafanikiwa kwa sababu chama  chake kimetekeleza kwa kiasi kikubwa ilani ya uchaguzi na yeye akiwa mfano bora wa kuigwa.  Atafanikiwa kwa sabau yeye mwenyewe amekuwa ndani ya serikali kwa miaka nenda miaka rudi. 
Anajua jinsi serikali inavyofanya kazi.  Amekuwa mwanafunzi mtiifu na mwaminifu wa marais waliomtangulia Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.  Rubani Magufuli atashinda kwa sababu chama chake pekee ndicho chenye mtandao ndani nchi nzima. 
Atashinda kwa sababu chama chake siyo chama cha msimu, kufufuka wakati wa uchaguzi na hufa uchaguzi ukiisha.  Rubani atashinda kwa sababu na chama chake kinakwenda kwa watu na kukaa nao watu na hatimaye kutanzua matatizo yao. Timu yake ya kampeni ni magwiji wenye uzoefu wa kutosha.
Rubani atashinda kwa sababu chama chake si cha kidini, kikabili au kieneo.  Vipo vyama vyenye kuhubiri Upemba, Ubariadi na Ukilimanjaro!  Wala huhitaji kujua vyama hivi? 
Watazame wawakilishi na wabunge wa vyama hivyo wanatoka wapi?  Waangaliye viongozi  wa vyama hivyo wanatoka wapi?  Rubani Magufuli atashinda, kwa sababu moyo wake na nafasi yake itakuwa imepoa bila kufikiri namna ya kulipa fedha mabilioni alizopewa na matajiri.
Hawa ni wale wanaowafadhili wagombea urais katika vyama vya siasa.  Wakiingia Ikulu lazima walipe fadhila, hisani na pesa walizopewa.
Rubani huyu atashinda kwa sabau nafasi ya kugombea urais katika chama hakuinunua wala hana masharti yoyote na wenye chama chao.
Atafanya kazi bila kuogopa kufukuzwa chama na wenye chama chao.  Hivi wagombea wengine nani mkubwa? Mgombea Urais au Viongozi wa chama chao?  Yeye Magufuli si mamluki katika Chama Cha Mapinduzi.  Yeye anatoka ndani ya chama na amepata ridhaa ya chama.
Mimi nilikuwepo alasiri jana wakati rubani Magufuli na rubani mwenza wake Samia walipovuta kasi ndani ya ndege yao ya kivita iitwayo ‘CCM MIG 35’ ilivyopaaa tayari kwa mashambulizi.

No comments:

Post a Comment