RAIS Dk. John Magufuli, amefichua mpango mchafu uliokuwa unataka kufanywa na wafanyabiashara, ambao wameingiza nchini kinyemelea vichwa 11 vya treni katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la kuboresha ufanisi na kuboresha uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam, jana, Rais Magufuli alisema anaviagiza vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi.
Alisema haiwezekani Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kupokea vichwa hivyo na kuruhusu meli iliyoleta vichwa hivyo kuondoka bila ya wasiwasi wakati mzigo wenyewe hauna muhusika.
"Siwezi kunyamazia hili na ndio maana hata kulizungumzia hamtaki. Siku vitakuja vifaru hapa. Haiwezekani vichwa vinakuja muingizaji hajulikani na anayevihitaji hayuko,"alisema.
Akilitolea ufafanuzi suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Injinia Deusdedit Kakoko, alisema Rais anayo haki ya kulizungumzia kwa 'kuwagonga' ili wajue wajibu wao.
Alisema ni kweli vichwa hivyo viliiingia nchini wiki mbili zilizopita na vililetwa na wakala wa meli ya Messina Line kutoka Afrika Kusini, kwa ajili ya Shirika la Reli Tanzania (TRL), ambalo limedai kuwa, halivitambui na halivihitaji.
"MESSINA LINE katika taarifa zao tulizozipata kwenye uchunguzi wetu wa awali, inaonyesha kuwa walipata oda ya vichwa hivyo kutoka Kampuni ya Nkomazi Trading Company, ambayo inaonekana ndio ilikuwa na biashara na TRL, japokuwa biashara yao ilikufa baadaye,"alisema.
Injinia Kakoko alisema TRL inaweza kulizungumzia suala hilo kwa vizuri zaidi, japokuwa shirika hilo nalo linasema sio vyao na hawavitaki vichwa hivyo na hawana makubaliano ya kuletwa nchini.
"Inaonekana kulikuwa na biashara baina ya TRL na Nkomazi Trading ya vichwa hivyo tangu awamu iliyopita, ambapo awamu ya kwanza ya vichwa ilikuja nchini na baadae biashara hiyo ikafa,''alisema.
Kwa mujibu wa Injinia Kakoko, vichwa hivyo ndivyo vilivyompeleka mahakamani aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Injinia Kipalo Kisamfu.
Hivyo, alisema taarifa rasmi kuhusiana na suala hilo, itatolewa baada ya kukaa pamoja na TRL kwa kuwa TPA hadi sasa hakuna kitu kilichotolewa na kampuni hiyo zaidi ya kuvipokea vichwa hivyo.
"Sisi ni taasisi ya serikali, mzigo ulipokuja katika mfumo wetu na kuonyesha ni mali ya TRL, tukaona ni lazima tuupokee, ila tulipowaeleza mna mzigo wenu huku, ndipo wakatujibu hapana na taarifa kutolewa kwa rais,''alisema.
Februari 12, 2016, viongozi wakuu wa TRL walipandishwa kizimbani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), akiwemo Injinia Kisamfu na wenzake kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Hali hiyo inatokana na TRL kuipa zabuni kampuni ya HINDUSTHAN ENGINEERING AND INDUSTRIES, ambayo haikukidhi vigezo, kuleta mabehewa ya kokoto nchini.
Fedha ambazo zimeshalipwa kwa Kampuni ya HINDUSTHAN ni Dola za Kimarekani 1,280,593.75, kati ya Dola 2,561,187.50, na serikali kuunda kamati za uchunguzi kuhusiana na suala hilo, ambapo ilibaini licha ya kupewa tenda kwa kampuni hiyo, pia mabehewa na vichwa vilivyoletwa vilikuwa 'feki'.
Awali, akizungumzia mradi wa uboreshaji wa ufanisi na kuboresha uwezo wa bandari, Rais Magufuli alisema nchi imetengeneza historia kwa kuitengeneza Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema kwa muda mrefu nchi ilikuwa na mipango ya kutengeneza bandari hiyo, ambapo zaidi ya asilimia 90, ya mizigo inayokuja nchini, inapitia kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
"Tumeweza kutimiza ndoto zetu pamoja na kuboresha miundombinu mingine ya barabara na viwanja vya ndege. Tunawashukuru wadau wetu wa maendeleo, ikiwemo Benki ya Dunia kwa msaada wa ujenzi wa gati jipya la kushushua magari,''alisema.
Rais Magufuli alisema ujenzi wa gati hiyo pamoja na maboresho ya gati namba moja hadi saba, nchi imetoa Dola za Marekani milioni 64 huku mradi mzima ukigharimu Dola milioni 421, ukiwemo mkopo wa Benki ya Dunia na wadau wengine.
Naye, Injinia Kakoko alisema mradi huo ni muhimu na utaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa na uwezo mkubwa wa kupokea shehena nyingi za mizigo pamoja na kuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi za mizigo.
"Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kuongeza ufanisi wa bandari kutoka mizigo tani milioni 14, kwa sasa hadi tani milioni 38, ifikapo mwaka 2030,''alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi ya Tanzania, Bella Berd, alisema Bandari ya Dar es Salaam, ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania na nchi jirani.
Alisema upanuzi huo utasaidia kukuza uwezo wa bandari kufanya shughuli zake na kuinua biashara pamoja na kutengeneza ajira katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema mradi wa uboreshaji lango kuu la Bandari ya Dar es Salaam, unatekelezwa kama sehemu ya mipango mikakati ya nchi na bandari.
Alisema Tanzania ina mchango wake na wadau wengine wa maendeleo, ikiwemo Benki ya Dunia na Taasisi ya Trade Mark East Afrika, ambao kwa pamoja wamekuwa na mchango mkubwa kwenye ujenzi wa gati hiyo ya kushusha magari pekee.
Hivyo, alisema serikali itaendelea kusimama mstari wa mbele katika kuhakikisha miundombinu yote inaboreshwa, ikiwemo bandari ili kurahisisha safari ya uchumi wa kati wa taifa inafanikiwa kwa ufanisi mkubwa.
No comments:
Post a Comment