Na
Masanja Mabula, Pemba
MGOMBEA wa
Urais wa Zanzibar kupitia ADC, Hamad Rashid Mohammed, amesema hata kama hatachaguliwa kuwa Rais
atahakikisha anatekeleza ahadi zake kwani zinatekelezeka na kuwatupia lawama
wanasiasa wanaodai mamlaka kamili ili watimize ahadi zao .
Amesema chama
cha ADC na viongozi wake kiko kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na
si kutaka umaarufu na kuwashauri wananchi kuacha ushabiki wa
vyama bali wabadilike na kuwachagua viongozi mwenye lengo la kuwaetea
maendeleo.
Kauli hiyo
aliitoa wakati akihutubia wananchi wa wilaya ya Micheweni, mkoa wa
Kaskazini Pemba kwenye mkutano wa kampeni akiomba ridhaa ya wananchi
wamchague ili awe Rais wa Zanzibar, uliofanyika katika viwanja vya Shehia ya
Maziwang’ombe.
Aliwataka
wananchi kuwapima uwezo wagombea kwa kuwa wako walioshindwa kuwatumikia
wananchi licha ya kwamba baadhi yao ni mawaziri ndani ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa .
“ADC hata
kama haitapata nafasi ya kuongoza dola, ni lazima itekeleze ahadi zake kwani
lengo letu ni kuwaletea wananchi maendeleo na hatusubiri kuingia
Ikulu kama ilivyo kwa CUF,” alisema.
Aidha, mgombea
huyo alisema baadhi ya wizara zinazoongozwa na mawaziri kutoka CUF
zimeanza kupoteza hadhi na kuitolea mfano Wizara ya Biashara , Viwanda na
Masoko .
Alisema wakati
Mazurui anakabidhiwa wizara hiyo, kiwanda cha Makonyo Wawi kilikuwa na
mashine nane ambazo zilikuwa zinafanya kazi lakini kwa sasa mashine nne
zimahabirika na kudhoofisha utendaji wa kazi wa kiwanda hicho .
Akizungumzia
muundo wa serikali atakayoiongoza pindi akichaguliwa, alisema itakuwa na
mawaziri wasiozidi 12 huku akisema ataheshimu katiba kwa kuunda Serikali
ya Umoja wa Kitaifa .
Pia
alisema atalazimika kurejea kwa wananchi kutaka kufanyike kura ya maoni ili
kuifanyia marejebisho Katiba hiyo na kufanya vyama vyote vyenye usajiliwa
kudumu kushiriki katika kuunda serikali .
No comments:
Post a Comment