WADAU wameendelea kulaani mauaji yaliyotokea katika msikiti wa Masjid Rahman Ibanda, ulioko mkoani hapa, ambapo watu wawili walikufa baada ya kushambuliwa kwa mapanga na mtoto wa miaka 13 kujeruhiwa.
Katika salamu za pole za hivi karibuni, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza, mbali na kulaani mauaji hayo, kimeliomba jeshi la polisi liharakishe uchunguzi, kuwakamata walioua na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa upande wake kwa kushirikiana na Baraza Kuu la Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania (BARAZA KUU), wameviomba vyombo vya habari nchini kutolipa tukio hilo sura ya udini kwa kuwa ni mauaji yaliyoigusa jamii.
CCM kupitia Katibu wake mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, ilisema mauaji hayo ya kinyama hayavumiliki na kwamba, wananchi wana shauku ya kujua kiini cha tukio hilo na mengi yaliyoripotiwa hivi karibuni mkoani humo.
Mtaturu alisema hayo alipokwenda kuwapa pole wafiwa na walionusurika katika mauaji hayo ya kinyama, yaliyotokea katika Msikiti wa Rahmani, Ibanda Relini, Katani Mkolani, Kata ya Buhongwa, ambapo Mwenyekiti wa mtaa huo, Alphonce Mussa (48), aliuawa kwa kupigwa risasi.
“Waliofanya mauaji msikitini hawana Mungu wala dini za kweli, hawana ubinadamu, jambo hili lisipite hivihivi, waliohusika wachukuliwe hatua na isichukue muda mrefu, vinginevyo watu hawataenda misikitini na makanisani kwa amani,” alisema Mtaturu, wakati akimsalimia mtoto Ismail Abeid (13), aliyejeruhiwa kwa kukatwa panga.
Katibu huyo, ambaye alitembelea Msikiti wa Rahman na familia za wahanga wa tukio hilo, alisema CCM imepokea kwa masikitiko tukio hilo na kuwaomba viongozi wa dini wasuluhishe mapema migogoro inayojitokeza ili kuepusha matukio ya kinyama yanayoweza kutokea.
Alieleza kuwa kwa miezi mitatu mfululizo sasa, hali ya usalama jijini Mwanza, imekuwa mbaya, hivyo polisi wakiwapata wahalifu hao, watangazwe na matokeo ya uchunguzi yajulikane maana wananchi wana shauku ya kujua kiini, lakini pia watoe ushirikiano kwa polisi ili wauaji wakamatwe.
Mei 18, mwaka huu, saa 2:30 usiku, watu wasiuojulikana walivamia msikiti huo na kuwaua kwa kuwakata mapanga Imam Msaidizi, Feruzi Ismail (27) na waumini Mbwana Rajabu (40) na Hamis Mponda (28) na kumjeruhiwa mtoto Abeid.
Wakati machungu ya mauaji hayo yakiwa hayajasahaulika, hususan kwa wakazi wa Kata ya Mkolani, Mei 22, mwaka huu, jirani zao wa Buhongwa, walishuhudia mauaji ya mwenyekiti wa mtaa wao, Mussa, aliyeuawa saa 2 usiku, kwa kupigwa risasi kifuani, wakati akisindikiza wajumbe wa mtaa wake baada ya kikao cha ulinzi shirikishi cha mtaa huo.
Kwa upande wa BAKWATA na BARAZA KUU, waliviomba vyombo vya habari nchini kutolipa tukio la mauaji ya msikitini sura ya uislamu kwa kuwa ni tukio lililofanywa na wahalifu ambao hawajulikani dini zao.
Akisoma tamko la taasisi hizo jana, mbele ya waandishi wa habari, Dar es Salaam, Shekhe Mussa Kundecha, alisema wanaunga mkono tamko lililotolewa hivi karibuni na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber kuhusiana na mauaji hayo.
Kundecha alisema uislamu unathamini zaidi uhai wa mwanadamu kiasi cha Mwenyezi Mungu kusema 'Mwenye kumuua mwanadamu bila hatia au kufanya ufisadi katika ardhi, ni sawa na kuwaua wanadamu wote.“
No comments:
Post a Comment