Tuesday, 24 May 2016
SIMBACHAWENE KUONGOZA MAZISHI YA KABWE LEO
WAZIRI wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene, ataongoza mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, yatakayofanyika leo katika Kijiji cha Mamba, wilayani Same, Kilimanjaro.
Akiwasilisha salamu za serikali kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, Simbachawene alisema serikali imempoteza kiongozi, ambaye alikuwa bado anatagemewa katika kuendeleza gurudumu la maendeleo nchini.
Pia, aliwataka wananchi kumkumbuka kwa yale mema aliyoyafanya, hasa kuuenzi mchango wake alioufanya kwa muda mrefu akiwa mamlaka za serikali za mitaa.
"Kabwe amefanya kazi na mamlaka ya serikali ya mitaa kwa takribani miaka 37 hadi kifo kinamkuta, kwa hiyo ni jukumu letu sote kumkumbuka kwa mchango wake alioutoa kwa jamii kwa muda wote huo na kuhakikisha maendeleo yanaendelea kuwepo,’’ alisema.
Kwa upande mwingine, aliwataka wanafamilia kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu na kumuomba Mwenyezi Mungu ili awape amani, umoja na upendo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akiwasilisha salamu za mkoa, aliwataka wale waliosoma na marehemu katika fani ya sheria, kuwa waaminifu na waadilifu katika mema na aliyoyafundisha wakati akiwa hai.
"Ninawataka Watanzania kutokuwa na maneno tusiyoyajua, kwa hiyo tusimvishe mzigo marehemu kwani yuko mbele za haki, bali kila mtu ajiangalie mwenyewe jinsi anavyoenda mbele za Mungu,” alisema Makonda.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, alisema atamkumbuka marehemu Kabwe, hasa siku alipokwenda kumuona hospitali na kumtaka afanye kazi kwa bidii.
Alisema atahakikisha wosia alioachiwa na marehemu anaufanyia kazi na kuitaka familia, hasa watoto kuambatana na mama ili aweze kuishi miaka mingi.
Mwenyekiti wa Jumuia ya Serikali za Mitaa Tanzania(ALAT), Gulamhafeez Mukadam, akimzungumzia Kabwe, alisema alikuwa na moyo wa kufanya kazi kwa bidii, kusaidia, kusimamia maendeleo yote yaliyopo ndani ya ALAT.
Pia, alisema kiongozi huyo alifanya kazi ya ujumbe katika kamati hiyo kwa muda wa miaka 15, kwa hiyo aliwataka wanafamilia kuwa wavumilivu na kuahidi kuwa pamoja nao na kumkumbuka katika mema yote aliyoyafanya.
Wakati huo huo, Naibu Makamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Frorience Luoga, alisema marehemu alikuwa mtu wa mfano wa kuigwa kwani alikuwa mstari wa mbele kuhimiza wenzake kusoma kwa bidii.
Akisoma wasifu, Francis Kabwe alisema marehemu alizaliwa Julai Mosi, mwaka 1956, katika kijiji cha Mamba Mpinji, wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro na alisoma elimu ya msingi Shule ya Ivuga, elimu ya sekondari shule ya Mzumbe (Morogoro) kidato cha tano na sita shule ya Mirambo.
Pia, alisoma shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baada ya kumaliza masomo yake, alisajiliwa kama wakili wa kujitegemea.
Marehemu alifanya kazi katika wilaya ya Same kama Ofisa Utumishi, Mbeya kama Mwanasheria wa Manispaa ya Mbeya na aliwahi kufanyakazi Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya, Mkurugennzi wa Jiji la Mbeya, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na Dar es Salaam.
Marehemu ameacha mke na watoto watano .
Kabwe alifariki dunia Mei 20, mwaka huu, katika Hospitali ya Mama Ngoma, iliyoko Sinza, Dar es Salaam alipokwenda kwa ajili ya matibabu kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa tezi dume.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment