SERIKALI imesema imeshapokea ripoti kutoka kwa wakuu wa
mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, kuhusu kuondolewa kwenye malipo watumishi hewa.
Waziri wa
TAMISEMI, George Simbachawene, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa,
kuwasilishwa kwa ripoti hizo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Dk.
John Magufuli, kutaka watumishi hewa waondolewe kwenye mishahara ya wafanyakazi
wa serikali.
Simbachawene alisema jana ilikuwa siku ya mwisho ya
utekelezaji wa agizo hilo na kwamba, wakuu wote wa mikoa wamelitekeleza kama
ilivyoagizwa.
“Taarifa za watumishi hewa tayari zimewasilishwa kwa
maandishi Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuanzia mwishoni mwa wiki.
“Kwa sasa taarifa hizo zinafanyiwa kazi na zitakapokuwa
tayari kwa matumizi ya umma, zitatolewa kwa vyombo vya habari kwa lengo la
kuufahamisha umma,”alisema.
Waziri huyo wa TAMISEMI alisema kwa sasa taarifa hizo
zinakusanywa kwa pamoja ili kupata idadi kamili.
Wakati huo huo, mkoa wa Kilimanjaro umebaini kuwepo na watumishi hewa 111, ambao
wanalipwa mishahara, akiwemo mtumishi aliyeko gerezani na wengine waliofariki.
Hali hiyo imeisababishia serikali
kupata hasara ya sh. milioni 281.5, kutokana na kulipa mishahara hewa, ambapo
idadi kubwa ni waalimu.
Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Sadiki,
alitoa taarifa hiyo Dar es Salaam, jana, kufuatia agizo la Rais Dk. John
Magufuli, la kuhakiki watumishi hewa, ambao wamekuwa wakilipwa mishahara.
Alisema mkoa huo una watumishi
21,134 na wakati wanapita kuhakiki, walioukutwa katika vituo vya kazi ni
19,516, waliopo masomoni 1,056, na waliohama lakini bado wapo kwenye orodha ya
mishahara ni 247.
Sadiki alisema watumishi sita walifariki,
mmoja anatumikia kifungo na wengine waliokutwa watoro ni 79, waliostaafu 25,
waliohama bila kuwepo kwenye ordha ya mishahara ni 25, waliopewa likizo na
ruhusa ni 137, wagonjwa 30, waliosimamishwa kazi tisa.
Alisema uchunguzi walioufanya umebaini
kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa haina mtumishi hewa, lakini Halimashauri ya Wilaya
ya Rombo inao watumishi hewa 11, ambao wametia hasara ya sh. milioni 61.5 na Manispaa
ya Moshi wapo 18 waliotia hasara sh. milioni33,4.
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi inao
watumishi hewa 15, walioitia hasara serikali sh. milioni 46.3, Halmashauri ya
Wilaya Hai inao watumishi hewa 31 na kusababisha hasara ya sh. milioni 88.7.
Nyingine ni Hamashauri ya Same yenye watumishi hewa tisa,
walioitia serikali hasara ya sh. milioni 43.1 na Halmashauri ya Mwanga yenye watumishi
hewa 26, huku ikiwa imetia hasara sh. milioni 119.1
Sadiki alisema kwa sasa mkoa huo
hauna tena watumishi hewa baada ya kufanyika kwa uhakiki huo na kuonya kuwa,
atakayefanya kosa hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu.
Alisema watatumia vyombo vya usalama,
ikiwemo Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wakaguzi wa
hesabu za serikali ili kuhakikisha kila aliyehusika anachukiliwa hatua na kwamba
fedha za serikali zinarudishwa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, ambaye amesema serikali mkoani hapa inao jumla ya wafanyakazi 24,716, waliopo katika utumishi kwenye idara za serikali kuu na halmashauri, lakini baada ya kufanyika uchunguzi wiki iliyopita, 84 walibainika kuwa hewa.
Shigela alisema wilaya inayoongoza kwa kuwa na watumishi hewa ni Lushoto, yenye watumishi 46, ikifuatiwa na Muheza (11), Mkinga (7), Tanga Jiji (7), Pangani (5), Bumbuli (5), Korogwe Vijijini (2) na Kilindi (1).
“Kama nilivyoagiza mara baada ya kukabidhiwa ofisi,nilitoa wiki moja niwe nimeletewa orodha ya wafanyakazi hewa na leo (jana) imebainika kuwa 84 ni wafanyakazi hewa, lakini idadi kamili ya watumishi wa serikali mkoani hapa ni 24,716,” alisema Shigela.
Mkuu huyo wa mkoa alisema katika orodha hiyo, wapo watumishi hewa waliokuwa wakilipwa mishahara kila mwezi, licha ya kwamba walishastaafu muda mrefu na wengine walishafariki huku baadhi yao wakiwa wameachishwa kazi kwa makosa mbalimbali.
Je, na wale walioko masomoni bila ya ruhusa nao pia ni hewa? pia, je, watakaporudi watapokelewa kama watumishi wa wilaya hiyo au mpaka waombe tena kazi upya?
ReplyDelete