Thursday, 1 September 2016

KUANGUKA KWA UKUTA,,,,SIRI NZITO YAFICHUKA


HATUA ya kusitishwa kwa maandamano ya UKUTA, yaliyoitishwa na viongozi wa CHADEMA, yaliyopangwa kuyafanya leo, kumeibua mengi mazito, yaliyokuwa yamejificha hadi kuwafanya viongozi hao kufikia uamuzi huo.

Imebainika kuwa, chama hicho kilipanga maandamano hayo kama mkakati wa kutaka kujenga taswira mbaya kimataifa, kwa kuichafua Serikali ya Awamu ya Tano kwamba, inakandamiza misingi ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.

Katika kufanikisha mkakati huo, baadhi ya vyombo vya habari na mashirika mengine ya kimataifa, vinadaiwa viliweka kambi nchini kwa zaidi ya mwezi mmoja, kwa kile kilichoelezwa kufuatilia namna ambavyo maandamano hayo yatatekelezwa.

Uchunguzi umebaini kuwa, lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kuchukua matukio ya wafuasi wao watakaokumbana na mkono wa dola ili kuchora taswira mbaya dhidi ya serikali kimataifa.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, vilivyopo ndani na nje ya CHADEMA, chama hicho kinadaiwa kutoa mamilioni ya shilingi kuwapa  vijana wakataokuwa tayari kuandamana.

Makundi yaliyolengwa yalikuwa ni madereva wa bodaboda, vijana wa mitaani, makundi yanayojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya 'mateja', ambapo kati ya sh. 10,000 hadi 40,000, zilipangwa kugawiwa kwa vijana hao.

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya wanaodaiwa kuwa watu wa  CHADEMA, katika eneo la Kivukoni, wakiwashawishi vijana wanaotumia dawa za kulevya, kuwaandikisha majina kisha kupewa sh. 15,000, kama kianzio ili wajitokeze katika maandamano hayo, ambapo waliwaahidi kuwapa kiasi kingine cha fedha leo asubuhi.

"Walikuwa wakishawishi kutoa fedha za kianzio sh. 10,000, kwa ahadi kuwa, siku ya maandamano watamaliziwa fedha nyingine na kupewa fulana," kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo, vijana hao walionyesha kutokubaliana kwa kuhofia usalama wao  na kutelekezwa, endapo wangekumbana na mkono wa dola.

"Si kama hatutaki fedha zao, ila CHADEMA wana tabia ya kututumia kama walivyofanya kwenye uchaguzi mkuu, mwaka jana, lakini tukipata matatizo, wanatutelekeza, hivyo hatuwezi kuandamana,"  alisema mmoja wa vijana hao, aliyejitambulisha kwa jina la Issa Kizzo.

Pia, ilifahamika kuwa, sababu nyingine ya kusitishwa kwa maandamano hayo ni upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho, ambao hawakutaka yafanyike kwa msisitizo kuwa hayana maslahi wala tija kwa maendeleo ya taifa.

Kutokana na kushikilia msimamo huo, baadhi ya viongozi waandamizi wa CHADEMA, walidaiwa kutoa vitisho vya kuwaondoa kwenye nafasi zao kwa kile walichokieleza kuwa ni usaliti.

"Baadhi ya viongozi wenzetu hawakutaka kufanyika kwa maandamano hayo, ambayo makatibu wa CHADEMA kila mkoa na wilaya, walitakiwa kuandaa  watu kwa ajili ya kutimiza lengo hilo," kilisema chanzo kingine.

"Kutokana na hali hiyo, ndio maana makatibu wa chama chetu katika baadhi ya mikoa, wametangaza kuwa wapo tayari kuachia ngazi," kiliongeza kusema chanzo hicho na kwamba, mpango wa maandamano umekibomoa badala ya kukijenga chama.

MCHEZO MCHAFU WABAINIKA
Pia, alisema mvutano mkubwa uliibuka baada ya wazo la kuwavalisha watoto wadogo fulana zenye maneno ya uchochezi ya UKUTA, kupingwa vikali.

Alidai wazo hilo lilitolewa kwa sababu ni vigumu kwa polisi kuwakamata watoto wadogo wakikutwa wamevalia fulani hizo, hivyo walipanga kuzigawa bure mitaani.

BODABODA WAWAGOMEA
Jingine lililosababisha mpango wa CHADEMA kukwama ni kukataliwa na waendesha bodaboda, ambao ilipanga kuwatumia kwa kiasi kikubwa.

Hilo lilidhihirishwa baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda na Bajaji wilayani Kinondoni, Almano Mdede, ambaye alisema badala ya kufanya maandamano, watafanya shughuli nyingine za kila siku kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi.

"Sisi kama viongozi wa vyama vya bodaboda, tunatoa tamko kwamba hatutashiriki maandamano, badala yake tutalijenga taifa letu ili kuepuka athari zinazoweza kutugharimu na familia kwa ujumla," alisema.

Mdede alisema katika mikoa mingine, kupitia viongozi wao, waendelee na shughuli za kuwaongezea kipato ili kukidhi mahitaji yao.

HATIMAYE MBOWE AUFYATA
Baada ya mbinu hizo kugongwa mwamba, hatimaye Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alitangaza kusitisha maandamano hayo, akidai kupisha mazungumzo baina ya viongozi wa dini  na serikali.

Akitangaza msimamo huo jana, mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Mbowe alidai wamepata wakati mgumu kufikia uamuzi huo, kwa kuwa sio kila wakati viongozi watafanya mambo yatakayowapendeza wanachama.

Alisema viongozi wa dini, awali walikwenda na ajenda moja ya kuomba wabunge wa UKAWA warejee bungeni na Kamati Kuu ya CHADEMA ilipokea kwa heshima wito wa viongozi hao.

"Ni matumaini yangu kuwa wana- CHADEMA watatuelewa kamati kuu, asanteni sana kwa kunisikiliza,''alisema Mbowe katika mkutano aliozungumza kwa muda mfupi sana.

Katika mkutano huo, Mbowe alionekana kulalamika huku akishindwa kujibu maswali ya waandishi wa habari, waliomtaka atoe ufafanuzi wa maswali, hasa kuhusiana na kesi walizoshindwa mahakamani.

"Mimi ni miongoni mwa watu tuliotamani kesho (leo) watu wawe barabarani, wanachama wetu, ambao watakwazika UKUTA si CHADEMA, UKUTA ni mchanganyiko wa makundi ya Watanzania, sasa hayo makundi yamekuja kutushauri tuwe pamoja,"alisema.

Kwa mujibu wa Mbowe, miongoni mwa watu waliowafuata na kuzungumza nao ni Taasisi ya Mwalimu Nyerere huku akidai kuwa, mgombea wao wa Urais, Edward Lowassa, amezungumza na Mama Maria Nyerere na amewasihi wasifanye maandamano, hivyo wamefikia uamuzi wa kusitisha maandamano hayo.

Hata hivyo, gazeti hili limepata taarifa za kuaminika kuwa, baadhi ya viongozi wa chama hicho wamemshushia lawama Mbowe kwa kuwa na maamuzi ya kukurupa na baadaye kushindwa kuyasimamia.

Walisema hata maamuzi ya kufanya maandamano nchi nzima, hayakuwa uamuzi wa chama bali ni uamuzi wa watu wachache, ambao wamekuwa wakifanya mambo bila kufuatilia msingi.

VIGOGO CHADEMA WAITWA POLISI J'NNE

Wakati huo huo, viongozi wakuu wa  CHADEMA, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, wametakiwa kufika kituo  cha polisi  cha kati  Jumanne ijayo kwa ajili ya kuhojiwa.

Kamishna wa  Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro,   alisema amewataka viongozi hao kutoripoti polisi leo kama walivyopangiwa, kutokana na masuala ya  upelelezi  kutokamilika.

Viongozi hao walikamatwa Jumatatu wiki hii, katika Hoteli ya Giraffe, jijini Dar es Salaam, wakiwa wanapanga mikakati ya maandamano.

Wengine wanaotakiwa kuripoti polisi ni Mbowe, Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar, Saidi Issa Mohammed, Katibu Mkuu, Vincent Mashinji na Mbunge wa jimbo la Kibamba, John Mnyika.

NCCR-MAGEUZI WARUKA KIMANGA
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi ya NCCR-Mageuzi, Faustin Sungura, alisema chama hicho hakijawahi kuunga mkono oparesheni hiyo na kwamba, kinachowaponza ni maamuzi binafsi ya Mwenyekiti wake, James Mbatia.

Sungura alisema hali hiyo inaleta mgogoro ndani ya chama.

Aidha, ameliomba Jeshi la Polisi na CHADEMA, kuwaambia wananchi ni barua ngapi za taarifa ya maandamano ya UKUTA zilikuwa tayari zimeandikwa na kuwasilishwa polisi.

Sungura alimtaka Mbowe, kuwaomba radhi wananchi waliopoteza mali na kuhofia usalama wao kwa ajili ya oparesheni hiyo, ambayo haikuwa na tija.

Alisema ni wazi CHADEMA walikuwa wanatingisha kiberiti na kuwa picha ya CHADEMA, inaweza kuchafua taswira ya upinzani, hasa ikitiliwa maanani muda uliopotezwa na watu kutafuta suluhu na watu kukamatwa hovyo.

"Haiwezekani mnatishia usalama wa nchi na wanachama kisha unachukulia rahisi tu. Wapo watu wamekimbia makazi yao, wengine wapo ndani wamekamatwa na wengine wanaishi kwa hofu...Ukuta ni msimamo wao na Mbatia,"alisema.

KATIBU CHADEMA AHAMIA CCM
Wakati huo huo, vyama vya upinzani vinaelekea kupoteza mwelekeo kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. Magufuli.

Aliyekuwa Katibu wa CHADEMA mkoani Mwanza, John Nzwalile, ambaye juzi alikitosa chama hicho na kuhamia CCM na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa, Anthony Diallom, alisema huko kumejaa udikteta.

Alisema CHADEMA wanapaswa watoe boriti kwanza kwenye jicho lao ndiyo watoe kibanzi kwenye jicho la wenzao.

Katibu huyo wa zamani alitoa mfano na kueleza kushangazwa na Lowassa, kujitangaza kuwa mgombea urais mwaka 2020.

“Kama siyo udikteta, anajitangazaje kuwa mgombea urais ? Vikao gani vilivyompitisha kuwa mgombea ?” Alihoji Nzalile na kudai viongozi 12, wa chama hicho wamebaki kukaa na kutoa maamuzi peke yao, na kusisitiza hiyo sio demokrasia, bali ni udikteta.

No comments:

Post a Comment