Tuesday, 1 November 2016
WATAHINIWA 408, 442 KUFANYA MITIHANI YA KIDATO CHA NNE
MTIHANI wa kidato cha nne na maarifa (QT), unaanza leo hadi Novemba 18, mwaka huu, ukihusisha jumla ya watahiniwa 408,442 waliosajiliwa, ambapo wananchi wametakiwa kuheshimu vituo vya mitihani kwa kutoingia maeneo ya shule.
Aidha, Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), limeonya kuwa halitasita kumchukulia hatua yeyote atakayejihusisha na udanganyifu wa aina yoyote katika mitihani kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma na sheria za nchi.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, akizungumza jana, jijini Dar es Salaam, alisema maandalizi yote yalishakamilika kwa kusambazwa kwa mitihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote Bara na Visiwani.
“Tunatoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zote kuhakikisha utaratibu wa uendeshaji mitihani ya taifa unazingatiwa ipasavyo, mazingira ya vituo vya yapo salama, tulivu na kuziba mianya yote ya udanganyifu,” alisema.
Dk. Msonde aliwaasa wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu, kwa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu, kwa kuwa baraza litachukua hatua kwa watakaobainika kukiuka utaratibu wa uendeshaji wa mitihani ya taifa.
Alisema watahiniwa 355,995, ni wa shule, ikilinganishwa na 448,382 wa mwaka jana na wa kujitegemea ni 52,447, miongoni mwa 408,442 waliosajiliwa, ambapo wa shule za wasichana ni 182,572, sawa na asilimia 51.28 na wavulana ni 173,423, sawa na asilimia 48.72.
“Miongoni mwao watahiniwa 59 ni wasioona na 283 ni wenye uoni hafifu, ambao makaratasi ya mitihani yao hukuzwa. Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,447, waliosajiliwa, wavulana ni 25,529, sawa na asilimia 48.64 na wasichana ni 26,918, sawa na asilimia 51.32, wakiwemo saba wasioona, wavulana watatu na wasichana wanne,” alisema.
Alisisitiza kuwa mtihani wa kidato cha nne ni muhimu kwa wanafunzi, wazazi na jamii kwa jumla kwa kuwa hupima uelewa wa wanafunzi kwa yote waliyojifunza kwa miaka minne na matokeo yake ni kiungo cha elimu ya juu ya sekondari na fani mbalimbali za utaalamu wa kazi ikiwemo afya, kilimo, ualimu na ufundi.
“Baraza linaamini wanafunzi wamejiandaa vema katika kipindi cha miaka minne waliyosoma elimu ya sekondari, hivyo wafanye mitihani yao kwa kuzingatia kanuni za mitihani ili matokeo yaonyeshe ujuzi wao halisi, tunawatakia kheri katika mitihani yao,” alisema.
Aliwaomba wadau wote kutoa taarifa katika vyombo husika, pindi watakapobaini mtu ama kikundi cha watu kujihusisha na udanganyifu wa aina yoyote ile wa mitihani.
Aidha, Dk. Msonde alisema kuanzia Machi, mwakani, baraza litaanzisha mfumo wa kielektroniki wa kuweka kumbukumbu ya wanafunzi wanaoanza shule kuanzia darasa la kwanza na wanaofanikiwa kumaliza ngazi mbalimbali zinazofuata.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment