Tuesday, 1 November 2016
BUNGE KUANZA VIKAO VYAKE LEO DODOMA
VIKAO vya Bunge la 11 vinaanza leo mjini hapa, ambapo shughuli mbalimbali zinatarajiwa kufanyika, ikiwemo uwasilishwaji wa miswada miwili.
Moja ya mambo yanayotarajiwa kuwavutia wengi na kusubiriwa kwa hamu kubwa ni kuwasilishwa kwa Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari wa Mwaka 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema miswada miwili inatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano huo wa tano wa Bunge la 11, ukiwemo Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari wa Mwaka 2016.
Aliutaja muswada mwingine utakaowasilishwa kuwa ni Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Huduma Mbalimbali wa mwaka 2016.
Katika bunge hilo, Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa tasnia ya habari, utasomwa kwa mara ya pili na ya tatu na baadaye kupitishwa kuwa sheria, ambapo baada ya hatua hiyo, utapelekwa kwa rais kwa ajili ya kutiwa saini na kuanza kutumika kama sheria.
Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya kamati za bunge vilivyofanyika mjini hapa, ambapo kamati mbalimbali zilitekeleza majukumu yake, ambapo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, pamoja na mambo mengine, ilipata nafasi ya kuujadili muswada huo.
Sambamba na hilo, kamati hiyo ilikaribisha wadau ili waweze kutoa maoni yao kabla ya kuuingiza Bungeni.
Itakumbukwa kuwa kamati hiyo ilikutana na wadau wa habari kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kutoa maoni yao Oktoba 20, mwaka huu, ambapo wadau waliomba kuongezewa muda kwa madai kuwa waliokuwa wameongewa hautoshi, ambao kamati ilikubali na kuwaongezea muda wa wiki moja.
Hata hivyo, wadau hao walishindwa kutoa maoni yao na kutaka waongezewe muda hadi Januari, mwakani, ambapo ombi hilo lilikataliwa na kamati.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, kamati ilitekeleza jukumu lake la kutunga sheria hiyo kwa kutoa maoni yao kwa kuwa wabunge ni wadau wa kwanza.
Jukumu lingine lililotekelezwa na kamati hiyo ni kufanyakazi ya kupitia kifungu kwa kifungu, wakishirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwanasheria wa Ofisi ya Bunge, wabunge pamoja na serikali.
Pia alisema kamati hiyo ilipokea maoni kutoka kwa baadhi ya wadau wa habari, kikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambayo yalijadiliwa kifungu kwa kifungu na kamati hiyo kwa ajili ya kuboresha muswada huo.
Aidha, alisema kamati hiyo ilipata nafasi ya kupitia maoni ya wadau wengine yaliyowasilishwa kwa njia ya barua na barua pepe, ambayo yalijadiliwa na kujumuishwa kwenye mapendekezo ya kamati kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi.
Hata hivyo, ilipofika Oktoba 29, mwaka huu, ambayo ilikuwa siku ya wadau kufika mbele ya kamati hiyo kutoa maoni, hilo halikufanyika.
Waliotakiwa kutoa maoni ni Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), MISA Tan na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Serukamba alisema kimsingi kanuni za Bunge zinabainisha kuwa muswada unaposomwa kwa mara ya kwanza bungeni, kila mwananchi au mdau anayehitaji kuusoma anaupata kirahisi, hivyo tangu uliposomwa Septemba, mwaka huu, wadau hao walikuwa na muda wa kutosha kuupitia na kutoa maoni yao
Alisema mara baada ya kusomwa kwa muswada huo, siyo kazi ya bunge kuwaita wadau na kuwashawishi wausome muswada huo, bali ni utashi wao ndio unaosukumu kuutafuta, kuusoma na kutoa maoni yao kwa kamati ya bunge kwa mujibu wa taratibu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment