JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE
LA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Pili
wa Bunge la Kumi na Moja unatarajia
kuanza kesho Jumanne tarehe 26 Januari, 2016 na kumalizika tarehe 5 Febuari
Mjini Dodoma.Shughuli zitakazokuwepo katika Mkutano huo ni kama ifuatavyo:
1. SHUGHULI ZA SERIKALI
Hoja za Serikali
(i)
Kujadili Hotuba ya
Rais
Kwa mujibu wa Kanuni ya 23
(1) (i) ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016, Bunge litajadili Hotuba ya
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoitoa wakati wa Ufunguzi
Rasmi wa Bunge jipya la Kumi na Moja tarehe 20 Novemba, 2015
Mjadala kuhusu hotuba ya
Mheshimiwa Rais unatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 26 hadi
28 Januari, 2016.
Aidha, kwa kuwa, Bunge la Kumi
na Moja mpaka sasa lina idadi ya Wabunge 380,
ni wazi kuwa kwa siku tatu zilizotengwa Wabunge wote hawataweza kupata
nafasi ya kuchangia. Hivyo katika Kikao cha Kwanza tarehe 26 Januari, 2016
itawasilishwa Hoja ya kutengua Kanuni za Bunge ili:-
(a)
badala kila
Mbunge kuchangia kwa dakika 15 sasa iwe
dakika 10 tu:
(b)
badala
Kipindi cha Jioni kuanza saa 11.00 sasa kianze saa 10.00 jioni.
Hii itawezesha kuongeza
idadi ya wachangiaji kutoka 63 ambao
wangepatikana kwa utaratibu wa kawaida hadi 114 baada ya Kanuni husika
kutenguliwa. Aidha, Utaratibu utaandaliwa ili Spika aweze kuchagua Wabunge
watakaochangia kwa kuzingatia uwiano wa vyama na vigezo vingine.
ii.
Kujadili na Kuridhia
Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
Kwa mujibu wa masharti ya Ibara 63(3)(c) ya Katiba, Bunge litajadili na
kuidhinisha Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5
unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpango huu ni
wa Mwaka 2016/17 – 2020/21 na itakumbukwa kuwa kila mara tunapoanza Bunge jipya
Serikali huwasilisha Mpango huo Bungeni ili uweze kujadiliwa na Bunge. Kabla ya
Mkutano huu, siku ya Jumatatu (leo) tarehe 25 Januari, 2016 tutakuwa na Mkutano
wa Wabunge wote ili Serikali itupe maelezo ya Mpango huo kabla ya kuujadili
rasmi Bungeni.
(ii)
Bunge kukaa kama Kamati ya Mipango
Itakumbukwa kuwa kwa
kawaida na chini ya masharti ya Kanuni ya 94(1) ya Kanuni za Bunge Mpango huu
ulipaswa kujadiliwa na Bunge katika Bunge ambalo hufanyika mwezi Novemba ya
kila mwaka. Hata hivyo kwa kuwa Mkutano uliopita wa Mwezi Novemba, 2015 ulikuwa
ndio Mkutano wa Kwanza wa Bunge jipya na ni mahsusi kwa ajili ya Ufunguzi wa
Bunge tu hivyo tukalazimika kuhamishia katika Mkutano huu wa Pili, ambao
kimsingi hushughulikia Taarifa za Mwaka za Kamati za Bunge.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 94
ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016 Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango
katika Mkutano huu wa Pili, ili kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya
Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa Fedha
unaofuata.
Aidha, kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 94(3) Mpango huo
utawasilishwa kwanza kwenye Kamati ya Bunge
ya Bajeti ili iweze kuuchambua kabla ya kuwasilishwa Bungeni kwa mjadala wa
Wabunge wote.
2. SHUGHULI
NYINGINE:
A. KIAPO CHA UAMINIFU:
Kutakuwa na Kiapo cha Uaminifu kwa Waheshimiwa
Wabunge Kumi na Moja (11), ambao wamechaguliwa na wengine kuteuliwa na Rais
mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kwanza wa Bunge. Wabunge hao ni kama
ifuatavyo:-
i. Mhe. Goodluck Mlinga - Jimbo la Ulanga
ii. Mhe. Shaaban Shekilindi - Jimbo la Lushoto
iii. Mhe. Godbless Jonathan Lema -Jimbo la Arusha Mjini
iv. Mhe. Omar Abdallah Kigoda -Jimbo la Handeni
v. Mhe. Deogratias Ngalawa -Jimbo la Ludewa
vi. Mhe. Rashid Chauchau -Jimbo la Masasi
vii. Mhe. Dkt. Abdallah Posi -Kuteuliwa na Rais
viii. Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa - Kuteuliwa na
Rais
ix. Mhe. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako - Kuteuliwa na Rais
x. Mhe. Dkt. Philip Mpango -Kuteuliwa na Rais
xi. Mhe. Dkt. Augustine Mahiga - Kuteuliwa na Rais
Inategemewa kuwa Wabunge
hawa wataapishwa tarehe 26.1.2016 isipokuwa Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako
ambaye ameomba kuapa tarehe 27.1.2016 na Mhe. Dkt. Augustine Mahiga tarehe
2.2.2016.
B. MASWALI:
(i) MASWALI YA KAWAIDA:
(Chini ya
Kanuni ya 39(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016)
Itakumbukwa kuwa, nyakati za Mikutano ya Kawaida,
Maswali yanayowekwa kwenye orodha ni kumi na tano (15) kila siku, isipokuwa
siku za Alhamisi ambapo kuna kipindi cha Maswali ya Waziri Mkuu Maswali ya
Kawaida huwa ni kumi (10) kwa siku hiyo. Hivyo katika Mkutano huu wa Pili wa
Bunge, jumla ya Maswali ya msingi ya kawaida 125 yanategemea kuulizwa na
kujibiwa.
(ii) MASWALI KWA WAZIRI MKUU:
(Chini ya
Kanuni ya 38(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016).
Utaratibu wa kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu
Maswali ya papo kwa papo kila Alhamisi utaendelea. Hivyo kwa kufuata uzoefu
inakadiriwa kuwa, Maswali ya msingi kumi na sita yataulizwa na kujibiwa na Mheshimiwa Waziri
Mkuu.
C. CHAGUZI MBALIMBALI:
(Chini ya
Kanuni ya 12 ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016) na Nyongeza ya Pili na
ya Tano ya Kanuni za Bunge.Katika
Mkutano huu wa Pili wa Bunge kutakuwa na zoezi la chaguzi mbalimbali za
kuwapata Viongozi wa Bunge na Wawakilishi wa Bunge katika vyombo na Taasisi
mbalimbali kama ifuatavyo:-
i.
Uchaguzi
wa Wenyeviti watatu wa Bunge;
ii.
Uchaguzi
wa Wajumbe saba wa Tume ya Utumishi wa Bunge;
iii.
Uchaguzi
wa Wajumbe watano wa Bunge la Afrika (PAP);
iv.
Uchaguzi
wa Wajumbe watano wa Jukwaa la Wabunge wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC-PF);
v.
Uchaguzi
wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe kumi na mbili wa Kamati ya Utendaji
wa Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA);
vi.
Uchaguzi
wa Wajumbe watano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU);
Katibu wa Bunge atatoa maelezo kamili kuhusu
masharti kwa kila Taasisi na vigezo kwa Wagombea. Aidha, atatoa Taarifa rasmi ya nafasi hizo ambapo
Wabunge wenye nia ya kugombea wataombwa kufanya hivyo kwa kuzingatia vigezo
vitakavyoainishwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi za Bunge
DODOMA.
25 Januari, 2016.
No comments:
Post a Comment