Wednesday, 17 August 2016

MKURUGENZI AMWAGA CHOZI AKIHOJIWA NA KAMATI YA BUNGE

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Agness Mkandya, amejikuta akimwaga chozi mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kutokana na kubanwa na maswali na wajumbe, kuhusiana na ubadhirifu wa fedha na madudu yanayofanyika katika halmashauri hiyo.

Agness, alidondosha kilio hicho jana, mjini hapa, katika ukumbi wa Pius Msekwa, wakati watendaji wa halamashauri ya wilaya hiyo wakihojiwa na kamati ya LAAC.

Tukio hilo lilitokea wakati mkurugenzi huyo alipoulizwa swali na Leah Komanya (Viti Maalumu - CCM), ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, aliyetaka majibu kuhusiana na ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri ya Gairo.

“Kamati ielewe kwamba Halmashauri ya Gairo imeoza na ni chafu, halmashauri yangu ina ubadhirifu mkubwa, nimewasimamisha kazi wakuu tisa wa idara, lakini kumbukeni na mimi ni mgeni, sina muda mrefu,” alisema na baada ya kumaliza kutoa kauli hiyo, aliangua kilio, hali iliyomfanya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vedastus Ngombale Mwiru, kumtaka kuwa mtulivu.

Kutokana na mkurugenzi huyo kuangua kilio, Ngombale alimtaka mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo kujibu swali hilo.

"Kwanza wewe mgeni hapa, si yupo mkaguzi wa ndani, hili ni la kwako naomba unyanyuke ujibu," aliagiza mwenyekiti huyo.

Aliposimama mkaguzi wa ndani, alisema tatizo lililopo katika halmashauri hiyo ni mfumo wa ukusanyaji mapato kutotumia njia ya kielektroniki.

Kutokana na majibu hayo, Mwenyekiti wa kamati hiyo alimnyanyua Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk. John Ndunguru, kujibu swali hilo.

Akijibu, Dk. Ndunguru alisema viongozi wengi ni wageni na watajitahidi kufuata maagizo watakayopewa.

Mbunge Leah aliuliza Halmashauri ya Gairo imekuwa na ubadhirifu mkubwa, ambao hauko kwenye mapato peke yake, kwani watendaji wamekuwa wakifanya wizi kwa kutumia stakabadhi za kughushi, hivyo kuikosesha halmashauri mapato.

Pia, aliuliza watendaji jinsi walivyojipanga katika kuweka ulinzi kwenye madawati yanayotolewa hivi sasa kwa halmashauri ili yasije yakatumika vibaya, kama viti au meza kwenye nyumba za walimu.

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi huyo alisema suala la stakabadhi za kughushi lilijitokeza na mwezi huu walimkamata mtendaji mmoja na sasa wanaendelea na kufunga mashine za kukusanya mapato (EFD’s) na Shirika la Simu (TTCL) linafanya taratibu za kuwaunganisha.

“Nilikuwa natoa angalizo, nataka mkurugenzi ajibu kama  nilivyouliza sitaki maelezo mengi,” alisema Leah.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Abdallah Chikota, alimsihi mkurugenzi huyo kuondoa hofu ili aweze kujibu maswali kwa ufasaha.

Alisema kazi ya kamati sio kumuonea mtu bali ni kuhakikisha inapata majibu sahihi na ya kina, yatakayowezesha halmashauri hapa nchini kusonga mbele katika maendeleo yake.

“Tangu mwanzo tulikwambia uondoe hofu na kutoa majibu ya kamati ukiwa unajiamini na sasa umeendeleza hofu,”alisema Chikota.

Kamati hiyo inaendelea na vikao vyake kwa kuzihoji halmashauri mbalimbali, kabla ya mkutano wa bunge kuanza Septemba 6, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment