Wednesday 1 June 2016

MTANDAO HATARI WAFICHULIWA


SERIKALI imetangaza orodha ya majina ya watu wanaohusika na mtandao wa kimataifa wa biashara haramu ya binadamu, ambapo mawasiliano yameshafanyika na nchi zingine ili kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Mtandao huo umekuwa ukiwasafirisha wasichana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 24, kwenye mataifa mbalimbali, wakiwalaghai kuwatafutia kazi viwandani, madukani na kwenye migahawa, badala yake wanalazimishwa kujihusisha na biashara ya ukahaba.

Aidha, imesema Watanzania 408, wanatumikia vifungo mbalimbali huku wengine wakikabiliwa na adhabu ya kifo kwa makosa ya kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Watanzania wanaotumikia adhabu hizo wamefungwe kwenye magereza ya nchi za Brazili, China, Iran, India, Nepal, Oman, Thailand na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda, Waziri wa wizara hiyo, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alisema uchunguzi unaendelea kuwabaini watu wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu nchini.

Alisema mtandao huo wa biashara ya ukahaba, umekuwa ukiwalazimisha wasichana hao kurejesha kati ya dola 5,000 hadi 6,000, kiasi ambacho sio rahisi kukipata kwenye biashara hiyo, kwa sababu mapatano ya kazi hiyo hufanywa na madalali wa mtandao huo.

Aliongeza kuwa, madalali hao huwapokonya pasi za kusafiria hadi pale ambapo wasichana hao watakaporejesha fedha zilizotumika kuwagharamia.

“Kwa kuwa wasichana hao wanakuwa hawana namna nyingine ya kupata fedha hizo, hulazimika kujiingiza kwenye biashara ya ukahaba,”alisema  Balozi Mahiga.

Alifafanua kuwa baadhi ya wasichana waliofanikiwa kuutoroka mtandao huo, walikimbilia ofisi za ubalozi za Tanzania kutafuta msaada.

Alisema kutokana na kutokuweko kwa fungu maalumu la kuwasaidia, maofisa ubalozi wamekuwa wakitoa fedha zao kununua tiketi za ndege ili kuwasafirisha kurudi nchini.

Balozi Mahiga alisema katika jitihada za kukabiliana na tatizo hilo, wizara iko kwenye mazungumzo na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, ili liweze kuwasafirisha wasichana hao.

“Ni wazi kwamba vitendo hivyo vya kinyama vinakiuka haki ya binadamu kwa sababu usafirishaji binadam ni uhalifu kwa mujibu wa makosa ya kupangwa, kupitia azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2003.

“Azimio hilo ni la kuzuia, kukomesha na kuadhibu wasafirishaji binadamu, hasa wanawake na watoto, chini ya itifaki yake,” alisema.

Waziri huyo alibainisha kuwa, baada ya kupata ushirikiano  kutoka kwenye jumuia za Watanzania waishio Thailand na India pamoja na wahanga wa biashara hiyo, serikali imefanikiwa kupata orodha ya majina ya watu wanaojihusisha kwenye mtandao huo.

Alisema tayari mawasiliano na nchi hizo yameshafanyika ili kuwakamata na kuwafikisha vyenye mkondo wa sheria wahusika wa mtandao huo.

Aidha, alisema uchunguzi unafanyika kwa kuzihusisha balozi, ambazo wasichana hao wanapelekwa ili kuubaini mtandao huo, hususan wanaowezesha kupatikana kwa vibali vya kusafiria kwenye balozi hizo ili wakamatwe.

Balozi Mahiga aliwataka Watanzania wanaokwenda kufanyakazi nje ya nchi, kujisajiri kwenye ofisi za ubalozi na kutokubali kuweka rehani pasi zao za kusafiria.

DAWA ZA KULEVYA

Akizungumzia mwenendo wa biashara hiyo kimataifa, Balozi Mahiga alisema kuna baadhi ya Watanzania wamekamatwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara hiyo huku wengine wakikabiliwa na adhabu ya kifo.

Alizitaja nchi na idadi ya Watanzania waliofungwa ku ni Brazili 41, China 266, Iran 68, India 9, Nepal 4, Oman 3, Thailand 14 na Umoja wa Falme za Kiarabu wakiwa wamefungwa Watanzania watatu.

Aliwaomba wananchi kuacha kujihusisha na biashara hiyo kwa sababu athari zake ni kubwa na husababisha hasara kwenye familia zao na taifa.

TUHUMA KWA WANAJESHI

Waziri Mahiga alisema licha ya kazi nzuri zinazofanywa na askari kwenye kulinda amani, serikali imepokea tuhuma kwa baadhi ya askari wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya kuwadhalilisha wasichana huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Alisema serikali ilizichukulia tuhuma hizo kwa uzito, hivyo iliunda Tume Maalumu kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kufanya uchunguzi katika kipindi cha siku tano badala ya 10 zilizotakiwa na UN.

Balozi Mahiga alisema endapo tuhuma hizo zikithibitika, hatua kali dhidi ya waliohusika zitachukuliwa ili kuhakikisha vitendo kama hivyo havijirudii.

“Tanzania itajiunga na kusimamia kikamilifu 'Kigali Principles', ambazo ni muongozo wa jumla kwa nchi zinazopeleka askari wa kulinda amani kwenye vikosi vya UN,” Mahiga alisisitiza.

Akizungumzia biashara haramu ya silaha, alisema kwa kushirikiana na wadau, serikali imekuwa ikichukua jitihada za kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kuweka alama silaha zinazoingizwa nchini kisha kuzisajili.

Alizitaja jitihada zingine kuwa ni  kuchoma silaha haramu na kusaini mikataba ya kimataifa ya kudhibiti silaha haramu.

Katika hotuba hiyo, Waziri Mahiga aliliomba bunge kuidhinisha  sh. bilioni 151.3, ili wizara hiyo iweze kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwenye mwaka wa fedha 2016/17.

MAONI YA KAMATI

Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, katika maoni yake yaliyowasilishwa na Kanali mstaafu Masoud Ali Khamisi, ambaye ni Makamu Mwenyekiti, alisema wizara hiyo inapaswa kuangalia upya watumishi walioko kwenye balozi za Tanzania.

Alisema marekebisho yanapaswa kufanyika ili kuhakikisha wanapelekwa na kubakishwa watumishi wenye fani na uwezo wa shughuli za kibalozi ili kuleta ufanisi katika diplomasia ya uchumi.

Masoud alisema serikali inapaswa kutoa fedha kwenye balozi za Tanzania ili kueneza sera ya diplomasia ya uchumi, ambayo italiongezea taifa wawekezaji na watalii.

Pia, makamu huyo alisema fedha zinapaswa kutolewa ili kuwarejesha nchini maofisa wote waliomaliza muda wao katika balozi na kuacha kutoa barua za kuwarejesha nchini kama fedha za kugharamia kazi hiyo hazijapatikana.

No comments:

Post a Comment