Tuesday, 31 May 2016
VIGOGO WALIOSIMAMISHWA TCU WAVUNJA UKIMYA
VIONGOZI wanne wa ngazi ya juu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), waliosimamishwa kazi, wamekanusha kupinga hatua hiyo, badala yake wamesema wanaunga mkono kwa dhati hatua ya serikali ya Rais Dk. John Magufuli ya kuinua kiwango cha ubora wa elimu nchini.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kuivunja tume hiyo na kuwasimamisha viongozi hao, akiwemo Katibu Mtendaji, wakurugenzi wawili na ofisa mwandamizi mmoja, kufuatia tuhuma za kuwepo mapungufu ya kiutendaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, jana, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, alieleza kusikitishwa na taarifa zilizotolewa na vyombo mbalimbali vya habari kwamba, mchakato wa maamuzi ya kuwasimamisha kazi haukuzingatia sheria na kanuni.
Aliongeza kuwa taarifa hiyo ilieleza kupata maoni kutoka kwa mmoja wa viongozi hao waliosimamishwa kazi, jambo ambalo halina ukweli wowote.
“Sisi hatuna maoni juu ya hilo, wala hakuna yeyote kati yetu aliyezungumza na vyombo vya habari juu ya hatua hiyo. Nikiwa miongoni mwa watumishi hao waliopumzishwa kazi, nasema tunaunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano kwa kuimarisha ubora wa elimu nchini ili kukidhi viwango stahiki vya kitaifa na kimataifa,” alisema.
Aidha, Profesa Mgaya alisema anaunga mkono jitihada za rais za kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata elimu bure na kwamba, hilo ni jambo jema linalopaswa kuungwa mkono na si vinginevyo.
“Namuomba waziri aendelee na jitihada hizo za kuhakikisha anainua ubora wa elimu katika ngazi zote, sawa na dhamira ya rais, ili kuwa na taifa lenye watu walioelimika vizuri na watakaotoa mchango katika kuendeleza nchi,” alisema.
Waziri Ndalichako alichukua hatua hiyo ya kuivunja TCU na kuwasimamisha kazi watumishi hao, wiki iliyopita, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment