Tuesday, 13 October 2015

FAMILIA YA MWALIMU NYERERE YATOA WOSIA KWA WATANZANIA



Na Rashid Zahor

MIAKA 15 imepita sasa tangu Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alipofariki kwa ugonjwa wa kansa ya ini baada ya kuugua kwa muda mrefu na kulazwa katika Hospitali ya  St Thomas mjini London, Uingereza.

Kifo cha Mwalimu Nyerere kilizua majonzi makubwa kwa Watanzania kwa vile alikuwa alama muhimu ya mapambano ya kuleta uhuru, amani, umoja na mshikamano.

Mwalimu Nyerere ndiye aliyepigania Uhuru wa Tanganyika uliopatikana mwaka 1961. Na baada ya mapambano hayo kumalizika, aliendelea kupigania umoja, ambapo aliwaunganisha watu wa makabila zaidi ya 120 na kuwafanya wawe kitu kimoja licha ya tofauti zao za dini na makabila.

Aidha, Mwalimu Nyerere alipigania sana uwepo wa amani Tanzania na nchi za jirani, akiwa na imani kwamba, bila ya kuwepo na amani, maendeleo hayawezi kupatikana. Pia alikuwa akisisitiza sana umoja na mshikamano, ambavyo hadi leo vimeifanya Tanzania iwe nchi ya kutolewa mfano na nchi zingine duniani.

Mwalimu Nyerere pia alikuwa kiboko ya wanasiasa wa Tanzania kutoka vyama vya TANU na Afro Shirazi, ambavyo baadaye viliungana na kuunda CCM, waliojaribu kutoka nje ya mstari. Alikuwa mkali kila alipoona viongozi wa CCM na serikali wanafanya hivyo. Aliwakemea na walimuoga.

Huu sasa ni mwaka wa 15 tangu Mwalimu Nyerere alipofariki dunia. Mengi ya aliyokuwa akiyazungumza katika hotuba zake kuanzia alipokuwa rais hadi alipostaafu mwaka 1985, ndiyo yanayotokea hivi sasa. Alikuwa kama nabii kutokana na maono yake.

Kutokana na umuhimu wa siku hii, familia ya Mwalimu Nyerere imewataka wananchi kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuweka mbele utaifa, amani, umoja na mshikamano miongoni mwao.

Familia hiyo imesema haitakuwa na maana kumuenzi Mwalimu Nyerere, huku baadhi ya watu wakihubiri machafuko na uvunjifu wa amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Kauli hiyo ilitolewa wiki hii na msemaji mkuu wa familia ya Baba wa Taifa, Chifu Japhet Wanzagi, alipokuwa akizungumzia maadhimisho ya miaka 15 tangu kufariki kwa Mwalimu Nyerere.

Mwalimu Nyerere, ambaye alizaliwa mwaka 1922, kijiji cha Butiama mkoani Mara, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 nchini Uingereza, alikokwenda kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa kansa ya damu.

Chifu Wanzagi alisema Baba wa Taifa alikuwa akipenda kusisitiza umuhimu wa kuitunza amani nchini huku akikemea tabia za baadhi ya watu kuwagawa wananchi kwa misingi ya dini na ukabila.

"Ndio sababu Baba wa Taifa hakuwahi kusimama kwenye itikadi za vyama vya siasa. Japokuwa ndiye mwasisi wa Chama cha TANU na baadaye CCM. Hakuwahi kuvaa gwanda la kijani, linalotumiwa na viongozi, wanachama na wapenzi wa chama hicho,"alisema.

Alisema katika maisha yake yote, Mwalimu Nyerere alisimama kama Baba wa Taifa na hata ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, hakuweza kujipambanua.

Chifu Wanzagi amewaasa Watanzania katika kuelekea uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, waweke mbele utaifa bila kushabikia vyama vya siasa au wagombea wa urais.

"Hicho ndicho kiwe kipaumbele chetu. Vinginevyo itakuwa kazi bure kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kutaja jina lake ama sifa zake bila kuonyesha yale aliyoyahimiza kwa vitendo,"alisema Chifu Wanzagi, ambaye kwa sasa ndiye kiongozi mkuu wa kabila la Wazanaki, ambalo makao makuu yake ni katika kijiji cha Butiama, kilichoko wilayani Musoma Vijijini mkoani Mara.

Chifu Wanzagi amewataka Watanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo kwa kuwa tangu alipoanzisha harakati za kupigania uhuru, alikuwa akipigania amani.

"Pasipo na amani, hakuna maendeleo. Kukitokea vurugu, kila kitu kitaharibika. Hakuna vita mbaya kama ya wenyewe kwa wenyewe. Ni vita ya hatari,"alisema msemaji huyo wa familia ya Mwalimu Nyerere.

Mbali ya wadhifa wa kuwa chifu wa wazanaki, Wanzagi, ambaye jina lake halisi ni Japhet Kizulila Wanzagi, pia ni Askofu Mkuu wa kanisa la Last Church of God Tanzania, cheo alichokipata mwaka 2007.

Alirithi cheo cha uchifu wa kabila hilo Machi, 1997, baada ya kufariki kwa baba yake, Chifu Edward Wanzagi Nyerere, ambaye alikuwa kaka mkubwa wa Mwalimu Nyerere. Ni mtoto wa 37 kati ya watoto 57 wa Chifu Edward Wanzagi, ambaye naye alirithi cheo hicho kutoka kwa baba yake Nyerere, Chifu Burito Nyerere.

Huyu ndiye aliyeachiwa siri nzito na Mwalimu Nyerere, siku chache kabla hajaondoka kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kupatiwa matibabu na hatimaye kufariki dunia. Inasemekana kuwa Mwalimu Nyerere alimweleza Chifu Wanzagi siri nzito kuhusu wanasiasa na viongozi wa serikali ya Tanzania wakati huo.

Katika hilo, inasemakana Mwalimu Nyerere alimtajia Chifu Wanzagi majina ya wanasiasa na viongozi, ambao hawafai kupewa madaraka ya kuiongoza Tanzania. Mbali na hilo, inasemekana pia kuwa, Mwalimu Nyerere alimweleza kiongozi huyo wa Wazanaki ni kwa njia zipi Tanzania itaweza kuendesha siasa ya vyama vingi bila kuvuruga amani, umoja na mshikamano uliopo miongoni mwa Watanzania, mambo aliyoyaasisi kwa kushirikiana na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.

Hata hivyo, siku zote Chifu Wanzagi hayupo tayari kueleza siri hiyo nzito aliyoachiwa na Mwalimu Nyerere. Sababu kubwa anayoitoa ni kwamba, siasa ya Tanzania kwa sasa imekaa pabaya.

Chifu Wanzagi alisema si viongozi na wanasiasa wote wa Tanzania waliopenda mawazo ya Mwalimu Nyerere. Alisema baadhi ya wanasiasa hao wamediriki kutamka waziwazi kwamba Mwalimu Nyerere aliwaonea.

“Alikuwa mwalimu kwa watu wengine, hasa wale waliomzunguka kama jina lake lilivyokuwa. Lakini kwa wakati huu tulionao, ukiwafundisha wenzako kupitia mafundisho yake (Mwalimu Nyerere), utaonekana hujui kitu. Pia unaweza kusababisha matatizo makubwa, ndio sababu sipendi kuzungumza lolote kuhusu wosia nilioachiwa na Mwalimu,”alisema.

Chifu huyo wa Wazanaki alisema anasikitika kuona viongozi wengi wa serikali wameacha kufuata mstari wa uadilifu aliochora Mwalimu Nyerere, badala yake wamekuwa wakinyakua raslimali za nchi kwa maslahi yao binafsi.

Kutokana na kasoro hiyo, amewashauri viongozi wa serikali kutumia siku ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere kutafakari ni jambo lipi wanaweza kujisifu kwamba wamelifanya kwa lengo la kumuenzi mwasisi huyo.

“Hii ni siku muhimu sana kwa watanzania kumkumbuka kiongozi wao wa kwanza. Kila mtanzania, mzalendo na anayeipenda nchi yake, anapaswa kutafakari na kujiuliza amefanya kitu gani kumuenzi kiongozi huyu. Lazima kuwe na kitu kwamba bila yeye, kisingekuwepo na je, hicho kitu bado kipo na kina hali gani?” Alisema.

Chifu Wanzagi alisema japokuwa imepita miaka 15 tangu Mwalimu Nyerere alipofariki dunia, hali haijabadilika sana, japokuwa yapo maendeleo makubwa yaliyofikiwa. Alisema bado Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi katika maisha yao ya kila siku.

Akizungumzia kampeni za vyama vya siasa zinazoendelea nchini, alisema ameshangazwa na uamuzi wa baadhi ya wanasiasa wakongwe na waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, kuvihama vyama vyao na kujiunga na vyama vingine.

Amesema uamuzi uliofanywa na wanasiasa hao umedhihirisha wazi kwamba hawakuwa wazalendo kwa vyama na taifa lao, bali waliweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.

"Naomba nisieleweke vibaya, lakini huu ndio mtazamo wangu maana kila mtu ana mawazo yake, mimi nipo tofauti na wengine,"alisema.

Akitoa mfano wa wanasiasa hao, Chifu Wanzagi alisema wakati wa Mwalimu Nyerere, mtu kama Kingunge Ngombale Mwiru alionekana muhimu na pengine kufikiriwa kuvaa viatu vyake, lakini hali ilianza kubadilika mapema.

"Tulidhani Kingunge angeweza kuvaa viatu vya Mwalimu Nyerere, japokuwa visingeweza kumtosha, lakini tulishabaini mapema kwamba ameanza kupungukiwa na vitu fulani muhimu,"alisema.

Alisema kuondoka kwa mzee huyo ndani ya CCM, kumetoa ahueni kubwa kwa chama hicho na ni kama vile kimetua mzigo mzito uliokuwa ukikielemea.

Chifu Wanzagi pia aliweka wazi kuwa, aliyechangia kuivuruga CCM na kusababisha makundi ndani ya Chama ni mgombea urais kwa tiketi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa.

Alisema Lowassa ndiye mwasisi wa mtandao uliobuniwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005 na ndiye aliyekuwa akiufadhili mtandao huo kwa kushirikiana na wenzake.

"Hawa ndio waliokigawa Chama, lakini sasa wamekisalimisha. Kuondoka kwao hakuna madhara yoyote kwa CCM. Sanasana wamekisaidia Chama kuimarika,"alisema kiongozi huyo wa wazanaki.

Alisema ni kweli kwamba baadhi ya wanasiasa hao walikuwa na majina makubwa ndani ya CCM, lakini hata katika vyama vya upinzani, wapo wanasiasa maarufu walioamua kuhama na kubaki wakiwa hawana vyama.

"Waliohama hawako upande mmoja, wapo kote kote. Kuhama ni kuhama tu, hakuna aliyeumia wala aliyepata,"alisema na kutoa mfano wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Akizungumzia mwenendo wa kampeni, Chifu Wanzagi alisema hali ilivyo sasa inampa wasiwasi kuhusu mustakabali wa Tanzania katika kuelekea uchaguzi mkuu kwa vile baadhi ya kampeni zimelenga kuashiria vurugu na uvunjifu wa amani.

Chifu Wanzagi alisema tofauti na uchaguzi wa mwaka 2005 na 2010, uchaguzi wa mwaka huu unaelekea kuwa na ushindani mkali huku baadhi ya wanasiasa wakitoa matamshi ya kuhubiri vurugu.

"Unajua Watanzania wengi ni waoga, hawajui nini kitatokea. Wanamuomba Mungu yasitokee machafuko kama yanayotokea katika nchi zingine,"alisema kiongozi huyo wa kabila la Wazanaki.

Alisema inashangaza kuona kuwa baadhi ya vyama vya siasa havina jeshi, lakini vimekuwa vikitamka hadharani kwamba iwe, isiwe, lazima viingie Ikulu na kutwaa uongozi wa nchi.

"Hii haijakaa sawa kabisa. Uwepo wa Mwalimu labda ungesaidia. Lakini kwa sasa hakuna kiongozi anayeweza kuzungumza kitu akaogopwa na kusikilizwa,"alisema.

Ametoa mwito kwa Watanzania waliojiandikisha kupigakura, kujitokeza kwa wingi kuitumia haki yao hiyo ya kidemokrasia kwa kuwachagua viongozi wanaowataka.

Alisema ni vyema kila Mtanzania akampigia kura mgombea anayemtaka, badala ya  kukubali kulazimishwa kufanya hivyo kwa vile kura ni siri ya mpigaji.

"Watanzania wanapaswa kuwa makini sana katika kuchagua rais, wabunge na madiwani wao. Wasikubali kulazimishwa kuwapigia kura wagombea wasiowataka,"alisisitiza.

Aidha, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na wafuasi wao, kukubaliana na matokeo ya uchaguzi huo baada ya kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema ni vyema watanzania wawe wamoja kwa vile kiongozi yeyote atakayechaguliwa, atakuwa kiongozi wa watanzania wote na si wa chama kimoja.

Chifu Wanzagi pia alisema ni vyema watanzania wapuuze wito unaotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wa kuwataka wakae vituoni baada ya kumaliza kupiga kura kwa lengo la kulinda kura za vyama vyao.

Akizungumzia maisha ya Mwalimu Nyerere, Chifu Wanzagi alisema, alikuwa akichukia rushwa na vitendo vya kifisadi na siku zote alikuwa akiwapiga vita viongozi na wanasiasa wa aina hiyo.

“Nina hakina kama Baba wa Taifa angependa rushwa, familia yake ingekuwa mbali sana. Na hata sisi tunaomzunguka, tungekuwa tunaishi kivingine kabisa,”alisema.

Alisema mapenzi kwa nchi yake na taifa lake, ndivyo vitu vilivyomfanya Mwalimu Nyerere aishi maisha ya kawaida na familia yake na alifanya hivyo kutokana na kuona mbali.Alisema hakuna kiongozi mwingine wa wakati huo duniani na hata hivi sasa, ambaye angeweza kuishi maisha aliyokuwa akiishi Baba wa Taifa kutokana na wadhifa aliokuwa nao.

“Lakini kutokana na nafasi yake, aliona isingekuwa vyema kuishi maisha ya kifahari na hata watoto wake waliridhika. Alikuwa na dhamana ya nchi, hivyo asingeweza kufanya hivyo,”alisema.

“Ukishakuwa kiongozi wa nchi, hupaswi kufanya biashara na kujilimbikizia mali. Ukiwa mtu wa aina hiyo, ni rahisi kununuliwa. Ukiwa kiongozi wa nchi, unapaswa kufanana na Mwalimu. Hakutaka hata ndugu zake wajihusishe na biashara,”alisema.

“Hivyo tunapaswa kumuenzi Mwalimu kwa kuchukia rushwa na kuifanya ionekane kuwa adui wa kwanza mbaya kwa watanzania kuliko maradhi na umaskini. Hawa maadui wengine wawili wanapaswa kufuata baadaye,”aliongeza.

Chifu Wanzagi alisema wapo baadhi ya viongozi wa serikali wanaojaribu kukemea rushwa, lakini walio wengi hawafahamu wajibu wao kwa wananchi ndio sababu wanakumbatia vitendo hivyo na kuviona vya kawaida.

Kiongozi huyo wa Wazanaki pia alieleza kusikitishwa kwake na tabia ya viongozi wa siasa kulindana baada ya kufanya makosa. Alisema watu wanafanya makosa na kukabiliwa na tuhuma nyingi, lakini wanalindwa na kuendelea na kazi zao bila wasiwasi.

"Enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, watu wa aina hii wasingevumiliwa, angewatoa. Hakuwa anamwacha mtu anayetuhumiwa kuendelea kukalia ofisi wakati anachunguzwa. Hali ya sasa inasikitisha sana," alisema Chifu Wanzagi.

Chifu huyo alisema Mwalimu Nyerere alikuwa akiona mbali ndio sababu hotuba alizozitoa wakati nchini ilipopata uhuru hazichuji na kwamba mambo mengi aliyoyatabiri wakati huo ndio yanayotokea hivi sasa.

Akizungumzia siasa ya vyama vingi nchini, Chifu Wanzagi alisema wakati ilipoanzishwa, watu wengi hawakuwa wakifahamu iwapo itasababisha wananchi wasigane na kutokea matukio ya kuhatarisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwao.

Hata hivyo, aliwataka watanzania kujipa moyo na kuendelea kumuomba Mungu ili nchi yao iepuke kuingia katika janga na  matatizo na uvunjifu wa amani unaoweza kusababisha umwagaji wa damu.

No comments:

Post a Comment