Friday 16 October 2015

MWAPACHU ALISHAHAMA CCM KIMYA KIMYA, KINACHOFANYIKA NI GHILIBA



Na John Kiroboto

"ANGEHAMA Kinana (Abdulrahman) au Mangula (Phillip), kweli CCM kungekuwa na mtikisiko, lakini huyu Mwapachu (Juma), aah ni sawa tu na mwanachama mwingine yeyote tena wa kawaida, hivyo ni kumtakia kila la heri amfuate salama huyo anayemfuata huyo wala asituumize kichwa."

Hiyo ni kauli ya Mzee Johnson Malimi, mkazi wa Mbagala Kuu, Dar es Salaam, akizungumzia taarifa za kuhama kwa Balozi Mwapachu juzi, akisema hakuridhishwa na mchujo uliofanywa na CCM dhidi ya Edward Lowassa katika kinyangíanyiro cha kuwania urais.

Kauli ya Malimi ina uzito wake, hasa kwa kuzingatia mchango wa Mwapachu ndani ya CCM, ambao si mkubwa kiasi cha kuitikisa CCM na hasa akilinganishwa na makada wengine wa zamani waliomo ndani ya chama na waliokwishaondoka.

Hivi sasa wanasiasa kuhama vyama inaonekana kama ëdilií kwa kuitisha wanahabari au kuandika taarifa ndefu wakijieleza, ili kupata fursa ya kutangazwa na vyombo vya habari nchini na kujionyesha kana kwamba ni watu muhimu katika jamii kuliko wengine. Lakini hasa wanapokuwa ëwametowekaí kisiasa.

Balozi Mwapachu ni maarufu, lakini si kwa kiasi kikubwa hata akilinganishwa na kaka yake, Harith Mwapachu, ambaye alipata kuitumikia nchi hii kwa njia ya kutukuka zaidi kuliko mdogo wake huyo, ambao wote kwa kiasi kikubwa waliingizwa serikalini kwa fadhila za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa sababu za kihistoria alizokuwa nazo mzazi wao (baba).

Ni dhahiri kwamba Juma aliendelea kukumbatiwa na serikali na chama kutokana na sababu hizo za kihistoria na ndiyo sababu hata alipomaliza muda wake wa ubalozi nchini Ufaransa na kurudi nchini, hakuonekana tena kwenye medani za kiutawala serikalini na hata chamani.

Hilo lilitokea baada ya serikali kubaini kuwa wapo Watanzania wengi wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi zilizopo za kusaidia wananchi kujiletea maendeleo yao binafsi na ya Taifa kwa jumla, hivyo naye kujiona kama mtu aliyetelekezwa na hivyo kujenga chuki dhidi ya serikali na chama, kwa kuwa mambo hayakuwa yanakwenda anavyotaka yeye.

Hiyo ndiyo siri kubwa iliyomfanya ajiunge na kambi ya Lowassa, ambaye siku zote amekuwa na uchu wa madaraka na hata kuweka mikakati ya kuhakikisha anakuwa na watu ambao watamsaidia kutimiza azma yake ya kuwa kiongozi mkuu wa nchi hii, akiwamo Juma.

Katika harakati zake za kutaka ateuliwe kupeperusha bendera ya CCM katika kutafuta urais wa nchi, Lowassa aliwatumia kina Juma na wenzake kupanga mikakati hiyo na ndiyo sababu kuu ya kulalamika kuwa mchujo haukufanyika kwa haki na kwenda kinyume na demokrasia na ndiyo sababu kauli hii inaikariri ile ya mwanasiasa mwingine mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru.

Wawili hawa wanajifanya kusahau kabisa jinsi Lowassa alivyoibuka kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CHADEMA, akiungwa mkono na UKAWA na wanajisahaulisha kuwa hakuna demokrasia iliyotumika katika hilo, hasa baada ya wajumbe wa mkutano mkuu kuhojiwa kwa kutazamwa machoni kana kwamba ni wanafunzi darasani.

Kwa ujumla, wana CCM wanaomfuata Lowassa hawatafuti kingine bali ni maslahi waliyokwishaahidiwa kama Lowassa angetokea au atatokea kupewa ridhaa ya wananchi kuongoza nchi. Kwa maneno mengine, hilo likitokea kuna hatari ya kuundwa serikali ya marafiki.

Kwa kauli yake, Juma anasema alipiga kambi Dodoma kuhakikisha kuwa Lowassa anateuliwa kupeperusha bendera ya CCM, matarajio yake yalipokwenda kinyume akaichukia CCM na kuihama akitangaza hadharani akiamini kwamba pengine CCM itatetereka.

Ni dhahiri kuwa amechelewa sana kutangaza  kutoka CCM kwani alitakiwa kufanya hivyo mara tu baada ya CCM kutangaza ëTano Boraí ya urais na kumfuata Lowassa. Leo wananchi wameshaamua wanataka nini na wanamtaka nani na si kweli kuwa Lowassa ni chaguo la wengi.

Inaeleweka wazi kuwa baada ya Lowassa kupewa bendera ya UKAWA (CHADEMA) kugombea urais, Juma akawa mmoja wa wanamkakati wa kuhakikisha kuwa anashinda katika uchaguzi huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, ndiyo sababu tunasema alichelewa kutangaza, kwani alishahama CCM kimyakimya.

Jambo la kupongeza ambalo pengine Juma anakuwa mtu wa kwanza kulifanya, ni la kurejesha kadi ya CCM alikoichukua tawi la Mikocheni, tofauti na wengine ambao wanabaki nazo au kuzichoma moto hadharani huku wengine wakijinasibu kuwa ni sawa na cheti cha ndoa au cha shule na hakirudishwi.

Lowassa kuwa chaguo la wengi ni kauli za jumla ambazo hazina mashiko na ambazo pia Juma angepaswa kuzitoa akisaidiwa na takwimu na matokeo ya utafiti alioufanya, hasa kwa kuzingatia kuwa ni mwanataaluma na mwanadiplomasia mwenye uwezo.

Hizi ni kauli za kumtia moyo Lowassa, ambaye anajua fika kuwa hana ubavu kwa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli, lakini pia ni za kulipa fadhila kutokana na jinsi alivyokwishawagharimia watu hao wanaojinasibu kuondoka CCM na kuhamia kwake, bila kutaja anahamia chama gani.

Tangu alipohama Frederick Sumaye, ambaye ni mpiga debe mkuu wa Lowassa, lakini pia Kingunge, hakuna kati yao pamoja na Juma, wanaosema kwa uwazi wanahamia chama gani ndani ya UKAWA na kudai wanabaki kuwa wana mabadiliko.

Ni wazi kuwa watu hawa wanapima upepo na kama kundi la UKAWA litashindwa watakuwa salama, kwa kuwa hawatakuwa wamejiingiza ndani ya chama mahususi kati ya vinne vinavyounda umoja huo, yaani CHADEMA, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, hivyo kuwa rahisi kuomba kurejea CCM.

Upo ushahidi wa viongozi waliopata kuhama CCM na kurejea kama vile Stephen Wassira na John Guninita na wakapokewa na CCM kutokana na kuwaona kuwa hawakuwa wanalijua walitendalo wakati huo, ingawa Guninita ameendelea kurukaruka kama kunguru na sasa yuko CHADEMA. Yakiharibika kama alivyozoea, ataomba kurudi CCM.

Hata hivyo, ni jambo la kushangaza kuwa hawa ambao walikuwa CCM kwa miaka mingi, wakitoa michango yao ya hali na mali, ndio hao leo wanaondoka na kuponda kana kwamba hawakushiriki kwa lolote kuifikisha CCM ilipo hivi sasa.

Kama alivyohoji Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku: ìKila anayetoka anasema chama kimeharibika, hivi mbona hawataki kutaja ni kina nani waliokiharibu, viongozi hao waliokiharibu ni akina nani? Kutoka ni sawa, lakini waeleze sababu za msingi.

ìVyama vina katiba zao, kama chama kimekushinda unasema kimekushinda utoke tu, ila tusihadae wananchi kwa maneno ambayo yanatuchanganya tukiyasikia.î

Kwa wanaojua mbinu za kisiasa, hasa nyakati kama hizi za uchaguzi, kinachofanywa sasa na UKAWA ni kuzungumza na wale wote waliokwishahama CCM kimyakimya na kujifanya bado wanachama, ili kutangaza kwa zamu kuhama chama na kujiunga nayo.

Hiyo ni mbinu wanayoitumia ili kuuhadaa umma kwamba viongozi wanaendelea kuihama CCM na hivyo inapoteza mwelekeo, hivyo hilo litarajiwe kutokea katika siku hizi za mwishomwisho kuelekea Oktoba 25, lakini ieleweke tu kuwa ghiliba zimeshafahamika na wananchi wameshaamua nani ni nani.

No comments:

Post a Comment