Friday 16 October 2015

HUU NI USALITI MWINGINE WA KINGUNGE NA SUMAYE





Na Julius Mapunda

MARA zote, Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, amekuwa akijinasibu kama mfuasi mkubwa wa sera za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hasa katika suala zima la kuhakikisha kuwa misingi ya amani, umoja na mshikamano iliyoasisiwa na kusimikwa ndani ya Taifa hili na mwasisi huyo wa Taifa hili haivunjwi wala kuchezewa.

 Hata katika miaka ya hivi karibuni tu, baada ya Rais Jakaya Kikwete kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya, Kingunge alisimama kidete kuanzia mwanzo hadi mwisho katika kuhakikisha kwamba mchakato huo haubomoi misingi hiyo ya amani, umoja na mshikamano ndani ya Taifa hili.

Kingunge alikuwa miongoni mwa Watanzania waliosimama kidete kupinga pendekezo la Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, lililotaka muundo wa Muungano wenye serikali tatu badala ya muundo wa sasa wenye serikali mbili, ambayo ndiyo sera kuu ya CCM inayosimamia na kuaminika kuwa ndiyo imeimarisha Muungano wa nchi mbili hizi za Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tangu 1964 hadi sasa, ikiwa ni zaidi ya miaka 50, sawa na nusu karne.

Mara kadhaa, katika kipindi chote hicho cha mchakato wa kuandika Katiba Mpya, Kingunge aliitisha mikutano na waandishi wa habari nyumbani kwake, kuelezea msimamo wake kuhusu umuhimu wa Taifa hili kuendelea kuongozwa ndani ya mfumo wa Muungano wenye serikali mbili, badala ya serikali tatu zilizokuwa zinatakiwa na viongozi walio wengi wa vyama vya upinzani.

Hoja ya Kingunge katika msimamo wake huo, mara zote hizo ilikuwa kwamba yeyote anayekubaliana na pendekezo la Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, maana yake alikuwa anakubali na kubariki kuvunjwa kwa Muungano huu uliopo kwa sasa.

Hoja kuu ya Kingunge ilikuwa ni kwamba katika muundo huo wa Muungano wa serikali tatu, serikali mbili za Tanganyika au Tanzania Bara zitakuwa na ardhi yake, jambo ambalo ndiyo msingi mkuu wa uwepo wa Taifa lolote lile, lakini hiyo serikali ya tatu itakayoitwa Jamhuri ya Muungano, haitakuwa na ardhi yake, hivyo itakuwa inaelea hewani tu, hali itakayoifanya ikose msingi endelevu wa uimara wake.

Kingunge alikuwa mmoja wa Watanzania waliobahatika kuteuliwa na Rais Kikwete kuwa miongoni mwa wajumbe zaidi ya 300 waliounda Bunge Maalumu la Katiba (BMK).

Ndani na nje ya Bunge hilo la Katiba, Mzee huyo alihakikisha kwamba misingi yote iliyoufikisha Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar, ambao hatimaye ulizaa Taifa jipya kabisa la Tanzania, haivunjwi wala kuchezewa na yeyote katika mchakato mzima huo wa Katiba Mpya.

Kwa mfano, nakumbuka Oktoba 14, 2013, Kingunge huyu alifanya mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha ITV, ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia umuhimu wa Watanzania kuenzi amani katika kipindi hicho cha mchakato huo wa Katiba Mpya.

Kingunge, wakati huo akiwa bado ana akili na ufahamu wake, kabla ya kuvurugwa na mchakato wa uteuzi wa mgombea urais ndani ya CCM mwaka huu, alipata fursa hiyo ya kuzungumza na chombo hicho Oktoba 14, hiyo siku ambayo ni maalumu kwa kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Kwa hiyo, Kingunge alifuatwa na ITV kutaka kupata maoni yake kuhusu jinsi Taifa na viongozi wa nchi wanavyomuenzi Mwalimu, tangu aliache Taifa hili, Oktoba 14, 1999.

Katika maoni yake hayo, Kingunge alisema: “Suala la udini na mabadiliko ya Katiba mpya visipoangaliwa kwa umakini mkubwa, mambo haya mawili yanaweza kusambaratisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa ulioachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Tusifike mahali tukazungumzia nchi, bali tungumzie Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali mbili zinatosha, hatuna sababu yoyote ya kuwa na serikali tatu kama kweli tunataka kuendelea katika umoja na mshikamano wetu kwa sababu umoja huo na mshikamano wetu ndivyo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kujenga Taifa imara na lenye amani na utulivu barani Afrika na dunia kwa ujumla wake.”

Hivyo ndivyo wengi wetu tulivyokuwa tukimfahamu Mzee Kingunge huyu katika suala zima la kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika kusimamia misingi muhimu aliyoijenga katika Taifa hili, inayomhakikishia kila Mtanzania umoja na mshikamano wa kitaifa.

Mwingine, ambaye wengi wetu hatukuwa tukimtilia shaka yoyote juu ya uumini wake wa muundo wa Muungano wa serikali mbili, ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.

Kama ilivyokuwa kwa Mzee Kingunge, Sumaye alipambana huku na kule katika kuhakikisha kwamba pendekezo la Tume ya Jaji Warioba, la kuwa na muundo wa Muungano wa serikali tatu, haliungwi mkono na wajumbe wa BMK, lakini pia na wananchi kwa ujumla wakati watakapokuwa wanapiga kura za maoni za kuikubali au kuikataa.

Hoja na sababu za Sumaye kukataa muundo wa Muungano wa serikali tatu, zilikuwa sawa na zile zile za Mzee Kingunge, kwamba ujio wa serikali tatu hizo utavunja uhusiano wa kindugu kwa wananchi wa pande mbili hizo za Muungano.

Wakati fulani, Sumaye alikwenda mbali zaidi kwa kukejeli mchakato wenyewe huo wa kuandikwa kwa Katiba mpya, akijenga hoja kwamba Katiba, hata iwe nzuri kiasi gani, haiwezi kuwa mwarubaini wa matatizo ya nchi hii, bali kinachotakiwa na wananchi wenyewe kujitambua na kutambua wajibu wao kwa Taifa lao.

Kwa mfano, Julai 23, 2013, wakati mchakato wa kuandika Katiba mpya ukiwa umepamba moto, Sumaye alikutana na viongozi na wadau wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), mjini Morogoro, yeye akiwa ndiye mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwa mtandao huo.

Katika hotuba yake siku hiyo iliyowasisimua wengi wa wasikilizaji wake, mbali na kuzungumzia hofu yake kwa nchi yake ya Tanzania, ya kuwepo uwezekano wa kumpeleka Ikulu mtu mwenye fedha chafu zinazotokana na biashara chafu, kama vile za ufisadi na kuuza dawa za kulevya katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2015, Sumaye alizungumzia pia mchakato wa Katiba mpya.

Alisema: “Katiba mpya si mwarobaini wa matatizo yanayolikabili Taifa hili, bali utekelezaji na usimamizi wa sheria utakaotokana na serikali itakayosimamia na kutekeleza sheria ili kulinda yale yaliyoelekezwa katika Katiba.

“Katiba haiwezi kumzuia mwizi kwenda kuiba na sheria haitamzuia mwizi kwenda kuiba ila itatamka adhabu ya kupewa huyo mwizi. Kwa hiyo, ili vyote hivi viwe na maana, ni lazima awepo mtu au chombo cha kumkamata huyo mwizi na kumfikisha katika mikono ya sheria na chombo hicho ni serikali.

“Kama serikali haiwezi kufanya kazi hiyo kwa ukamilifu, tutaishia kulalamika tu na maonevu na maumivu yataendelea kuumiza jamii. Kwa hiyo, hata Katiba iwe nzuri kiasi gani, na ikatamka kuwa rushwa ni adui wa haki na hata ikatoa adhabu kali sana kwa kosa hilo, lakini kama tutaweka madarakani viongozi waliopatikana kwa njia ya rushwa, Katiba hiyo haitatusaidia kitu.

“Hivyo Katiba nzuri mpya, lazima iambatane na serikali safi yenye kusimamia maslahi ya umma. Huwezi kumweka madarakani mwenyekiti wa kijiji au diwani au mbunge au hata Rais kwa njia ya rushwa ya kuwanunua wapigakura, halafu tutegemee kwamba Katiba Mpya italeta majibu na suluhisho la matatizo ya jamii.

“Hivi kama mtu anaweza kuhonga sehemu kubwa ya wapigakura katika jimbo la uchaguzi au hata katika nchi kama nafasi anayoisaka ni urais; tumeshajiuliza swali kuhusu fedha nyingi hivyo anazipata wapi?

“Kama anajihusisha na biashara chafu, akipata nafasi hiyo ya urais, watoto wetu watapona kweli? Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza tunapoelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.”

Hivyo ndivyo wengi wetu tunavyomfahamu Sumaye kuhusu misimamo yake juu ya rushwa ya uchaguzi, Katiba mpya na umhimu wa kuwa na viongozi wanaomuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuhusu misingi ya umoja na mshikamano, ambayo imeendelea kuwa nguzo kuu ya amani na utulivu wetu kama Taifa.

Huyo wa 2013, alikuwa Sumaye katika uhalisia wake, akiwa bado anatumia akili zake na ufahamu wake kuliko huyu wa sasa, hasa baada ya jina lake kukatwa na CCM mjini Dodoma.

Sumaye huyo wa miaka hiyo alikuwa na hofu kubwa juu ya uwezekano wa Taifa hili kumpeleka Ikulu kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, mtu ambaye atapata urais wa kununua kwa fedha chafu.

Sumaye huyo wa miaka hiyo, alikuwa anapita kila kona akiwahamasisha Watanzania pamoja na chama chake cha wakati ule, kuchukua tahadhari juu ya baadhi ya watu wanaosaka urais wa 2015 kwa kutumia fedha nyingi, ikiwa ni pamoja na kuwauliza ni wapi walikopata fedha hizo za kununulia urais wa Tanzania.

Mpaka hapa, tumeuona msimamo wa Kingunge kuhusu muundo wa Muungano wenye serikali mbili kama nguzo muhumu ya kuimarisha Muungano na uhusiano wa kindugu kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar katika Katiba mpya ijayo, kama mchakato huo utaendelezwa na rais ajaye wa awamu ya tano katika uongozi wa Taifa hili.

Tumeona pia misimamo miwili ya Waziri Mkuu wetu mstaafu, Sumaye, juu ya Katiba mpya pamoja na aina ya mtu anayepaswa kuogopwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Mtu anayetumia fedha nyingi kusaka urais, fedha ambazo wakati mwingine zilipatikana kutoka na biashara chafu inayozifanya fedha hizo kuwa chafu pia.

Je, ni kitu gani mpaka hapo kimeweza kuwasibu wanasiasa hao wawili hadi waweze kusaliti nafsi na dhamira zao?

Oktoba 3, mwaka huu, mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Edward Lowassa, ambaye anaungwa mkono pia na vyama vinavyounda UKAWA vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, alitangaza kwamba endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataanzisha upya mchakato wa Katiba mpya itakayoruhusu muundo wa Muungano wenye serikali tatu.

Kwa mujibu wa Lowassa, hatua yake hiyo inalenga katika kuipa mamlaka kamili Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wake katika masuala mazima ya uongozi wa visiwa hivyo, tofauti na ilivyo sasa katika muundo wa sasa wa Muungano wa serikali mbili.

Kwa tamko hilo la Lowassa, ambalo ni rasmi sasa tangu ajiunge na CHADEMA na hatimaye kusimamishwa kugombea urais kwa mwamvuli wa UKAWA, maana yake mgombea huyo analenga kuvunja Muungano huu ulioasisiwa na wazee wetu, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Muundo huo wa Muungano wenye serikali tatu, ambao unapigiwa chapuo leo na Lowassa, ndio ule ule ambao Kingunge na Sumaye walisimama kidete kuukataa baada ya Tume ya Jaji Warioba kupendekeza hivyo, wawili wote hao wakiamini katika nafsi na dhamira zao kwamba serikali tatu, kwa vyovyote vile, zitavunja Muungano, hivyo kuvuruga misingi ya umoja na mshikamano wa Taifa hili, vitu ambavyo ndiyo nguzo kuu ya amani na utulivu tangu Uhuru wetu.

Binafsi, kwa Lowassa kutamka hivyo, siwezi kushangaa kwa sababu hilo ndilo lililokuwa moja ya masharti ya kupokelewa na CHADEMA pamoja na UKAWA kwa ujumla. Kurejesha upya mchakato wa Katiba Mpya na kusimamia uwepo wa muundo wa Muungano wa serikali tatu, ambayo ndiyo msingi mkuu wa kuundwa kwa UKAWA.

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba wakati wote wa mchakato wa Katiba Mpya inayosubiriwa kupigiwa maoni ya wananchi kwa lengo la kuikubali au kuikataa, msimamo wa Lowassa ulikuwa ni serikali mbili, na hata wakati Katiba hiyo inapitishwa na BMK, mwanasiasa huyo alipiga kura ya NDIYO.

Aidha, kwa waliohudhuria hafla yake ya chakula na vinywaji katika mkesha wa kukaribisha mwaka mpya wa 2014, nyumbani kwake Monduli, watakuwa wanakumbuka pia msimamo wa Lowassa katika hili la serikali tatu au mbili.

Katika hafla hiyo, Lowassa aliweka wazi msimamo wake akisema hakubaliani na msimamo wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba, kuhusu serikali tatu kama ilivyopendekezwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Katiba.

Ni kwanini Lowassa amebadili gea ghafla akiwa angani na kuanza kuwa muumini wa serikali tatu? Jibu la swali hilo liko wazi. Yeye anachokisaka kwa sasa ni urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lolote ambalo anaona linaweza kumuongezea kura akilitamka majukwaani, analazimika kulitamka.

Ndiyo maana Lowassa huyu hakuona tatizo la kuwaachia huru watuhumiwa wa vitendo vya ugaidi wanaokabiliwa na kesi katika mahakama mbalimbali nchini, kwa sababu aliona hilo linaweza kumwongezea kura kutoka kwa jamii ya Waislamu wa Bara na Visiwani, wanaoguswa na watuhumiwa hao wa ugaidi, suala linalopigwa vita duniani kote.

Kwa hiyo, Lowassa kutamka kutaka muundo wa Muungano wa serikali, siwezi kumshangaa. Ninaowashangaa ni kina Kingunge na Sumaye. Itakumbukwa kwamba Kingunge alitangaza kujivua uanachama wa CCM, Oktoba 4, mwaka huu.

Tarehe hiyo ilikuwa ni siku moja tu baada ya Lowassa kutangaza rasmi mchakato wa Katiba mpya yenye muundo wa Muungano wenye serikali tatu. Wengi wetu tulidhani kwamba busara ya Kingunge, ingemwelekeza kwenda kumpatia ushauri swahiba wake huyo wa sasa madhara ya kauli yake hiyo ya kutaka serikali tatu, kwake yeye mwenyewe kama rais kama atabahatika kushinda au kwa mstakabali wa ustawi wa Taifa hili.

Badala ya Kingunge kumfuata Lowassa kumshauri madhara ya tamko lake hilo, yeye kesho yake, baada ya Lowassa kutoa tangazo hilo, aliitisha mkutano wa waandishi wa vyombo vya habari nyumbani kwake na kutangaza kujivua uanachama wa CCM, kabla ya siku nne baadaye kuibukia kwenye mkutano wa kampeni za Lowassa mjini Arusha.

Huu ndio unaoitwa unafiki na usaliti wa Kingunge kwa Taifa hili na kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Ni kwa vipi Kingunge anaweza kuungana na mtu aliyetangaza hadharani kutaka kuvunja Muungano huu ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Muungano ambao ndiyo nguzo ya umoja na mshikamano wetu wa kitaifa?

Nimkumbushe Lowassa kwamba Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jaji Warioba hiyo anayosema atairejesha kama wanavyotaka UKAWA, inazungumzia pia umuhimu wa Taifa hili kuwa na Tunu zake. Tunu hizo zinahimiza Utu, Uzalendo, Uadilifu na Uwazi, vitu ambavyo naamini Lowassa hatataka wala kupenda kuvisikia kabisa chini ya utawala wake, ambao naamini ufisadi utakuwa wa hali ya juu sana.

Tunamsubiri Sumaye na Kingunge nao watamke hadharani kwamba nao wanataka muundo wa Muungano wenye serikali tatu, halafu wawambie Watanzania hatima yao ya Muungano na Taifa lao.

 Ni muhimu Kingunge na Sumaye wakawaambia Watanzania kama serikali hiyo ya tatu itakayoletwa na Lowassa, haitakuwa inaelea tena angani tu kwa sababu ya kutokuwa na ardhi yake kama walivyowaaminisha wananchi wakati wa mchakato ule wa Katiba mpya. Ama kweli, Mungu huwaumbua wanafiki. Nahitimisha.

0713 707699

No comments:

Post a Comment