Tuesday, 22 March 2016

WATUMISHI SITA BAGAMOYO WAFA AJALINI



 VILIO na simanzi vimetawala katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, baada ya watendaji wake sita kufariki dunia katika ajali iliyohusisha msafara wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa.
Katika ajali hiyo, watu sita wamefariki dunia na wengine wanane kujeruhiwa, baada ya magari matatu yaliyokuwa kwenye msafara huo kugongana na lori la mchanga katika eneo la Kerege CCM, wilayani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventure Mushongi, alisema magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo ni gari la halmashauri, gari la Mkurugenzi Mtendaji wa Bagamoyo na gari la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani hapo.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni pamoja na Mhandisi wa Maji Wilaya ya Bagamoyo, Juliana Msagaa, dereva wa mkurugenzi, Halid Hassan, dereva wa TASAF, Makame Ally (40), Ofisa Mipango na Uchumi, Hilda Msele (59), Mwanasheria wa Wilaya, Tunsiime Duncan na Mchumi, Ludovic Palangyo.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ibrahim Matovu, Mratibu wa TASAF wilaya, Dorothy Njelile, Mweka Hazina, George Mashauri (42) na Mshauri wa TASAF, Amedeus Mbuta (37).
Wengine ni Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Julius Mwanganda (55) na wakazi wa wilayani humo, Tauliza Halidi na Amari Mohammed.
Mushongi alieleza kuwa majeruhi hao walikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Ofisa Utumishi na Utawala, Grace Mbilinyi, ambaye ni mmoja wa waliojeruhiwa, alitibiwa katika hospitali ya wilaya ya Bagamoyo na kuruhusiwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utawala Bora na Serikali za Mitaa (OR-TAMISENI), Suleiman Jaffo, aliyekuwa kwenye msafara huo alinusurika.
“Msafara huu ulikuwa ukienda kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Bagamoyo, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Naibu Waziri OR-TAMISEMI,”alisema Mushongi.
Chanzo cha ajali hiyo kinatajwa kuwa ni lori la mchanga, lililokuwa kwenye mwendo kasi, kuingia upande wa msafara bila kujali.
Kwa upande wake, Jafo alitoa pole kwa ndugu na jamaa wa marehemu na majeruhi wote na kusema yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.

SPIKA ATOA POLE
Spika wa Bunge,  Job Ndugai, ametuma salamu za pole kwa ndugu wa marehemu pamoja na majeruhi kutokana na ajali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  kwa vyombo vya habari, jana, na  Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge, ajali hiyo ilihusisha msafara wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Ilisema lori la mchanga lilikuwa lilikotokea Bagamoyo kuelekea Bunju, Dar es Salaam, na kuparamia magari mawili yaliyokuwa kwenye msafara wa kamati hiyo.
“Wajumbe wa kamati hiyo walikuwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani, kukagua miradi inayotekelezwa na TASAF na kabla ya ajali hiyo, walikuwa wakielekea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kabla ya kuanza kwa kazi yao,”ilieleza taarifa hiyo.
Kutokana na ajali hiyo, Kamati ya Bunge imeahirisha ziara yake mkoani Pwani na kwamba, wajumbe wote wa kamati waliokuwa katika msafara huo wapo salama, ikiwa ni pamoja na maofisa wengine walioambatana nao.
Taarifa zaidi kuhusiana na ajali ikiwa ni pamoja na vifo na majeruhi wa ajali hiyo, zitatolewa na Jeshi la Polisi.
Katika hatua nyingine, Christopher Lissa anaripoti kuwa, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana ilipokea  maiti ya mtu mmoja na majeruhi watano wa ajali hiyo.
Taarifa iliyotolewa na  Ofisa Habari  wa Hospitali hiyo, Neema Mwangomo,  ilisema,  maiti iliyopokelewa ni ya   Juliana Msaga, ambaye alikuwa Mhandisi wa Maji  wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, ambaye alifariki    dunia  wakati  akipelekwa katika hosipitali hiyo  kwa matibabu.
“Majeruhi waliopokelewa ni pamoja na Mkurugenzi wa Halmshauri  ya Bagamoyo,  Ibrahim Matovu, Ofisa  Maendeleo ya Jamii, Julius Mwanganda, Mweka Hazina , Geroge Mashauri,  Mratibu wa TASAF, Doroth Njitile  na Tanwira Khalid, ambaye ni raia,”alisema Neema.
Alieleza  kuwa, kati ya majeruhi hao, Doroth amefanyiwa upasuaji baada ya kuumia kifua, sehemu za miguu na tumbo.
“Majeruhi wengine wanne wameumia sehemu za miguu na kuhamishiwa  Taasisi ya Tiba ya Mifupa
(MOI),”alieleza Neema.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia  , Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,  alifika jana,  kuwajulia hali majeruhi  hao  hospitalini hapo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dk. Shukuru Kawambwa alitoa pole kwa familia na ndugu wa marehemu na majeruhi .
Alisema amesikitishwa na msiba huo na kwamba, inatia simanzi kuondokewa na watendaji watano wa halmashauri moja kwa wakati mmoja.
Dk.  Kawambwa alieleza kuwa kipindi hiki ni kigumu kwa watendaji waliobaki, lakini wote kwa pamoja wanapaswa kukabiliana na hali hiyo kwani kilichotokea ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

No comments:

Post a Comment