Friday, 25 November 2016
WAFUASI CUF WATWANGANA NGUMI NJE YA MAHAKAMA
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, jana, alitinga katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kufuatilia kesi aliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho.
Kabla ya Profesa Lipumba kutinga katika viunga vya mahakama hiyo, mapema asubuhi walionekana wafuasi wa chama hicho wakiwa katika makundi mawili, lile linalomuunga mkono Profesa Lipumba na lile lililoko upande wa wafungua kesi.
Wafuasi hao, ambao wengine walikuwa wamevalia sare za chama hicho, walionekana wakiwa wanarushiana maneno ya kejeli.
Jana, shauri hilo lililofunguliwa na Bodi hiyo ya CUF huku walalamikiwa wakiwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Lipumba na wanachama tisa wa chama hicho, lilipangwa kutajwa mbele ya Jaji Sekiet Kihiyo.
Baada ya shauri hilo kuitwa, wafuasi hao walianza kuongoza makundi kwa makundi kwenda katika chumba cha mahakama, ambapo kundi la wale wanaounga mkono bodi hiyo, lilikuwa la kwanza kuingia, hivyo kuanza kumzuia Profesa Lipumba na wafuasi wake.
Mmoja wa wafuasi wanaounga mkono bodi hiyo ya wadhamini, ambaye alikuwa kasimama mlangoni, alisikika akisema kwamba, hawezi kuingia mtu hadi mawakili wao watakapoingia.
Hali hiyo ilisababisha wafuasi waliokuwa wameambatana na Profesa Lipumba, kuanza kupiga kelele za kumtaka anayemzuia kiongozi huyo, kuingia katika chumba cha mahakama kuondoka mlangoni.
Mmoja wa wafuasi wa Profesa Lipumba, alimhoji mtu huyo, aliyekuwepo mlangoni, anatoa amri hiyo kama nani na kumtaka kuondoka kabla hawajamtoa.
Hata hivyo, wafuasi wa Profesa Lipumba, walishindwa kuvumilia hali hiyo, hivyo kuamua kumtoa mtu huyo mlangoni na kumbeba juu juu kisha kuanza kumpiga huku wakimtuhumu kwamba anataka kuharibu kesi.
Kitendo hicho kilisababisha pande zote mbili kuanza kushambuliana kwa kushikana mashati huku wengine wakirushiana makonde, mvutano ambao ulidumu kwa takriban dakika 45 na ulitulia baada ya Profesa Lipumba kuingia ndani ya chumba cha mahakama.
Baada ya Profesa Lipumba kuingia ndani ya chumba cha mahakama, askari waliokuwa wameitwa kwa ajili ya kutuliza mzozo huo, waliwataka wafuasi waliokuwa wamesimama katika korido kuondoka na kwenda nje ya jengo la mahakama.
MAMBO YALIVYOKUWA NDANI YA MAHAKAMA
Jaji Kihiyo alianza kuwalaumu wanachama hao wa CUF kwa kitendo walichokifanya, wakati shauri hilo limepelekwa kwa kutajwa.
“Nyie wote watu wazima tena na mawakili mpo, kwani hawa wafuasi ni wa upande gani? Mmesababisha fujo zote hizo wakati kesi yenyewe imekuja kwa kutajwa,” alihoji Jaji Kihiyo.
Alisema kesi yenyewe inatajwa kwa dakika tano tu, lakini alishangazwa na kitendo cha wafuasi hao hadi kufikia hatua ya kupigana.
Jaji Kihiyo aliwaeleza mawakili kwamba, siku nyingine wakiona wafuasi wamekwenda kwa wingi, watoe taarifa ili kesi iweze kuingia katika ukumbi wa wazi, hivyo aliwataka wafuasi wote watoke nje na wabaki mawakili na wateja wao tu.
Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa Bodi ya CUF, Juma Nassoro, alisema ndani ya chumba hicho cha mahakama, bodi imewasilisha maombi ya kumtaka Jaji Kihiyo, ajitoe na pingamizi juu ya majibu yaliyowasilishwa na mlalamikiwa Profesa Lipumba, kwa madai yana upungufu kisheria.
Alidai hati za viapo za majibu vya Profesa Lipumba na walalamikiwa wengine, vimewasilishwa vikiwa na upungufu kisheria kwa kutoa maelezo ya uongo na muapaji kuweka maelezo ya kuambiwa.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, ambaye anamwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), aliwasilisha pingamizi la awali, kupinga shauri hilo kwa madai kuwa, mahakama hiyo haijatoa kibali cha kufungua kesi na wadhamini hawajapewa idhini ya kufungua shauri hilo.
Jaji Kihiyo aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 6, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa mapingamizi ya awali na kwamba, ombi la kutakiwa kujiondoa katika shauri hilo, hajapokea barua rasmi ya kutakiwa kufanya hivyo na kusema, endapo ikiwasilishwa, atatoa majibu katika tarehe aliyoipanga kwa ajili ya kesi hiyo.
Bodi hiyo kupitia mawakili wake zaidi ya 10, akiwemo Hashimu Mziray na Twaha Taslima, walifanikiwa kufungua kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016, chini ya hati ya dharura.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment