Friday, 25 November 2016

MAKONDA AAGIZA MWENYEKITI SERIKALI YA MTAA KUKAMATWA


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amemwagiza Kamanda wa Polisi, Mkoa  wa Ilala, Salum Hamduni, kumkata  Mwenyekiti wa Serikali  ya Mtaa wa Gongolamboto,  Bakari Shingo  kwa tuhuma   za kughushi stakabadhi za malipo  katika ukusanyaji wa mapato.

Makonda alitoa agizo hilo juzi wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Kukamatwa kwa Shingo kulitokana na uamuzi uliotolewa na Makonda, baada ya mjumbe wa  serikali ya mtaa huo, Pili Said kutoa malalamiko yake  juu ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili Shingo.

Pili alisema Shingo amekuwa akiendesha utawala wa kimabavu, kuandaa mikutano ya kikanuni wakati wa usiku na kutokusoma mapato na matumizi.

 Alisema tangu Septemba, mwaka jana hadi sasa, Shingo hajawahi kusoma mapato na matumizi ya mtaa na amekuwa akitumia nguvu ya kutokuitisha vikao  vya kikanuni kutokana na kuogopa kuulizwa kuhusu fedha anazokusanya.

Kutokana na tuhuma hizo, Makonda alimwita Shingo na kumtaka ajibu tuhuma zinazomkabili.

Hata hivyo, Shingo alikana kupokea fedha zozote za mapato katika mtaa huo na kwamba kama mwenyekiti hazuiwi na kanuni yoyote ya kufanya vikao vya ulinzi na usalama katika mtaa wake.

Kutokana na majibu hayo,Makonda alimwita Pili na kumtaka athibitishe kuhusu  mapato katika mtaa huo, ambapo alieleza kwamba  mwenyekiti huyo amekuwa akikusanya na kutoa  stakabadhi ambazo anatengeneza mwenyewe.

“Amekuwa akitengeneza stakabadhi binafsi na kukuanya fedha kwenye vyanzo vya mapato. Stakabadhi hizo tunazo na tumeziwasilisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmshauri ya Manispaa ya Ilala,ofisi ya mkuu wa wilaya na tutazileta ofisi ya mkoa,”alisema Pili na kuwafanya wananchi washangilia.

Makonda alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala,Palela Nitu, athibitishe tuhuma hizo, hata   hivyo  alithibitisha kupokea  stakabadhi zinazotolewa na mwenyekiti huyo.

“Nimepokea stakabadhi hizo na kiutaratibu zinatakiwa stakabadhi za kielektroni,”alisema.

Kufuatia hali hiyo, Makonda alimuagiza Kamanda Hamduni kumkamata papo hapo Shingo na kumweka rumande mpaka pale tuhuma zake zitakapochunguzwa.

“Kamanda mkamate mwekyekiti huyu na umweke ndani hadi itakapothibitika tuhuma dhidi yake,”alisema Makonda hali iliyowafanya wananchi kushangilia.

Kamanda Hamduni alitekeleza amri hiyo na kumkamata mwenyekiti huyo.

No comments:

Post a Comment