Friday, 25 November 2016
JPM AFICHUA MADUDU TRA
RAIS Dk. John Magufuli, ameweka hadharani sababu za kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Aliweka hadharani sababu hizo jana, kwenye mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), kwenye makao makuu yake, yaliyoko Bungo, wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Rais Dk. Magufuli alisema alifia uamuzi wa kuivunja bodi hiyo, baada ya kukubali TRA kuweka fedha za maendeleo, kiasi cha sh. bilioni 26, kwenye akaunti za muda maalumu katika benki tatu za biashara.
"Sifahamu kama Chuo Kikuu Huria na nyinyi mmekuwa mkiweka fedha za maendeleo katika 'Fixed Deposit Account', lakini huo ndio umekuwa ni mchezo. Juzi, tumekuta fedha kiasi cha sh. bilioni 26, zilizokuwa zimetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya matumizi ya TRA, zikapelekwa kwenye benki tatu kama 'Fixed Deposit Account' na Bodi ya TRA ikapitisha, ndio maana nilipozipata hizo taarifa, fedha nikachukua na bodi kwaheri," alisema Rais Dk. Magufuli.
Aliwaonya viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali, ambao wamekuwa wakitumia vibaya fedha za umma, ikiwemo kuweka fedha nyingi za serikali katika akaunti za muda maalumu kwenye benki za biashara, ambako hujipatia fedha kupitia faida ya akiba bila kujali kuwa vitendo hivyo husababisha serikali kukosa fedha na kulazimika kukopa kutoka benki za biashara, ambako hutozwa riba kubwa.
"Hata sasa hivi, waziri upo hapa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), ambayo ilianzishwa kwa sababu maalumu, inachangiwa fedha wakati kuna fedha zao wameziweka kwenye 'Fixed Deposit Account', waziri hiyo ni 'message sent and delivered'," alisisitiza Rais Dk. Magufuli.
Kuhusu elimu, Rais Magufuli alisema suala la ubora wa elimu nchini halina siasa wala mjadala na hakuna njia ya mkato kuipata elimu bora.
Rais Dk. Magufuli alisema kutokana na kutaka kuhakikisha elimu inatolewa kwa ubora, hata wale wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), walipohakikiwa, walikutwa wenye sifa za kuwa pale ni wanafunzi 322 tu kati ya 7,500.
“Tumeamua kuhakikisha elimu inayotolewa ni bora, ambapo wanafunzi hao wa UDOM tuliwahamishia vyuo vingine kulinga na sifa zao, hivyo tungependa kila mtu asome kwa sifa aliyonayo na sio vinginevyo. Tungependa sifa ya elimu yetu iwe juu na ni bora kuwa na wanafunzi wachache kuliko kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wasio na sifa,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Alisema serikali ilipoamua kufanya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, kulijitokeza changamoto nyingi, ambapo wanafunzi wa shule za msingi waliongezeka kutoka milioni moja na kufikia milioni mbili, ambapo idadi iliongezeka kwa asilimia 84, kwa shule za msingi na sekondari kidato cha kwanza iliongezeka kwa asilimia 26.
“Ziliibuka changamoto za madarasa, ambapo madawati tumepambana na sasa imefikia asilimia 98, ambapo mikoa michache inamalizia zoezi hilo. Pia, kuliongezeka wanafunzi hewa 65,000, kwa shule za msingi na sekondari, ambao walikuwa wakilipwa malipo hewa kwa kuongezwa majina ya uongo,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza: “Changamoto zilizidi kuongezeka kwani bajeti ya mikopo iliongezeka kutoka bilioni 340 na kufikia bilioni 473, kutokana na ongezeko la wanachuo 98,000 hadi kufikia 124,389, ambapo wanafunzi waliokuwa wanapewa mikopo hewa kwenye vyuo hadi sasa imefikia kiasi cha shilingi bilioni 3.5.”
Rais Magufuli alisema Chuo Kikuu Huria, nacho kina sifa kama vyuo vikuu vingine, ambavyo vinatoa elimu ya moja kwa moja, hivyo nacho kinatakiwa kudahili wanafunzi wenye sifa kwani wanapokwenda kwenye ajira, haiangaliwi amesoma chuo gani.
Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema chuo hicho kinasaidia kuongeza wasomi nchini, ambapo kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wanaojiunga, ambapo asilimia 90 wanaosoma ni watumishi.
Ndalichako alisema kuwa vyuo vikuu vyote vina malengo sawa, hivyo OUT wasitake kutumia vigezo dhaifu kudahili wanafunzi kwani kinachotakiwa ni kuwa na watu wenye sifa ili kuboresha elimu ya juu nchini.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda, alisema wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu bora, ambapo wameweza kuwapatia elimu baadhi ya viongozi wengi, ambao kwa sasa ni viongozi wa ngazi za juu.
Bisanda alisema wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu hiyo ya huria na ya masafa kwa gharama nafuu, ambapo kwa sasa wamejitanua kwenye baadhi ya nchi kama vile Rwanda na Kenya.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inaonyesha kuwa elimu inayotolewa na chuo hicho, ambacho kina tawi kwenye kila mkoa, kuwa ina ubora unaotakiwa.
Hata hivyo, alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha, ikiwa ni pamoja na kukosa fedha za maendeleo kwa kipindi cha miaka saba, huku zile za OC nazo zikipungua mwaka hadi mwaka na kufikia asilimia sifuri, ambapo kwa matumizi yao ya TEHAMA kwa mwezi, wanatumia karibu sh. milioni 80.
Awali, Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Profesa Samwel Wangwe, alisema kuwa moja ya changamoto ni miundombinu ya barabara kutokuwa na lami na upungufu wa fedha kwa ajili ya wataalamu.
Wangwe alisema pia kuna upungufu wa wataalamu waliobobea, wadhamivu ni wachache na baadhi ya viongozi kutokuona umuhimu wa chuo hicho kinachotoa masomo kwa huria, ambapo watu wanasoma huku wakiwa kazini.
Wahitimu 4,027, walitunukiwa shahada mbalimbali na mkuu wa chuo hicho, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria mahafali hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment