KATIKA
kuthibitisha kuwa serikali haina mzaha kwenye suala la kodi, hatimaye imeidhinisha
mali za mfanyabiashara bilionea, Said Lugumi, zipigwe mnada wa hadhara.
Hatua hiyo
imekuja ili kufidia deni la  sh. bilioni
14, anazo daiwa mfanyabishara huyo, ambalo linatokana na malimbikizo ya kodi na
riba katika  kampuni yake ya Lugumi
Enterprises.
Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), tayari imetoa 
idhini kwa Kampuni ya Udalali ya Yono, kuziuza mali za mfanyabishara
huyo  kwa njia ya mnada wa hadhara.
Mali hizo ni
nyumba tatu za  kifahari, ambazo zilianza
kushikiliwa tangu  Aprili, mwaka huu,
baada ya bilionea huyo kushindwa kulipa 
kiasi hicho cha kodi TRA.
Yono
imethibitisha kupata idhini hiyo kutoka TRA na kwamba, tayari imepanga mali hizo  kuuzwa kwa mnada wa hadhara Septemba 9, mwaka
huu.
Akizungumza na
Uhuru, Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Yono, Scholastica Kevela,
alisema kwa idhini iliyotolewa na TRA, mali za Lugumi zinazotarajiwa kuuzwa
ni  nyumba iliyoko katika kiwanja  namba 701, yenye CT  namba 18173/35.
“Nyumba ipo
eneo la Upanga, wilayani Ilala na ni nyumba ya kifahari,”alisema Scholastica.
Aliongeza: “Pia
tutauza nyumba mbili zingine za  Lugumi, ambazo
zipo Kata ya Mbweni (JKT). Moja ipo katika kiwanja namba  47, kitalu 
namba 2, yenye CT namba 72456 
na  nyingine ipo kiwanja namba 57,
kitalu namba 2, yenye CT namba 11839, wilayani Kinondoni.”
MKurugenzi
huyo alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kumpa Lugumi muda mrefu ili aweze
kulipa deni hilo TRA, lakini alishindwa.
“Kwa muda wa
miezi minne tulikuwa tunashikilia mali hizi za Lugumi na alikuwa na maongezi na
TRA, kuona uwezekano wa kulipa kodi hiyo. Lakini  hadi TRA inatupa idhini ya kuziuza kwa mnada,
inaonyesha kwamba ameshindwa kulipa,”alisema Scholastica.
Alisema
umefika wakati Watanzania kulipa kodi bila shuruti ili fedha hizo zitumike
katika shughuli za maendeleo.
Ripoti ya
CAG chanzo cha sakata
Kupigwa
mnada kwa mali za Lugumi, kunakuja miezi michache baada ya ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi  Mkuu wa Hesababu za Serikali (CAG),
Profesa Mussa Assad,  kukabidhi
ripoti  ya mwaka 2015/16 kwa Rais Dk.
John Magufuli kisha kuwasilishwa bungeni Aprili 13, mwaka huu.
Katika
ripoti hiyo, CAG alibainisha kuwa uchunguzi uliofanyika katika Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi,  kutokana na zabuni ya
ununuzi ya Immigration System, kwa ajili ya Idara ya Uhamiaji, ulibaini kuwa
mzabuni Lugumi  Enterprises Limited,
aliwasilisha makabrasha mawili tofauti ya zabuni zenye thamani ya sh. bilioni
37.164 na sh. bilioni 39.518, hivyo 
kushindwa kuthibitika kwa makabrasha sahihi kati ya hayo mawili.
Katika
ripoti hiyo, CAG alisema amebaini wajumbe 
wawili wa kamati ya tathmini hawakutia saini ripoti  ya tathmini wala kujaza fomu za agano, kinyume
na kifungu cha 37(6) cha  Sheria ya
Manunuzi ya Umma (PPRA) ya mwaka 2011.
“Kamati ya
tathmini ilishindwa kubaini makosa yaliyowasilishwa na mzabuni Lugumi
Enterprises. Hatua hii  ilisababisha Bodi
ya Zabuni kuidhinisha  bei ambayo haikuwa
halisi, hivyo kusababisha  mabadiliko ya
gharama za mkataba kutoka sh. bilioni 37.163, kwenda sh. bilioni
41.475,”inaeleza ripoti hiyo.
Ilisema
Mzabuni Lugumi Enterprises alishindwa 
kufunga  ofisi katika vituo 36,
kati ya 152. Mkataba  kati ya Lugumi na
Wizara  ulikuwa na baadhi  ya vitu vyenye mchanganuo/vipengele  sawa, lakini vya bei tofauti, hatua
iliyosababisha hasara ya sh. 656,779,032.
“Jumla ya sh.
bilioni 1.029 zililipwa kama gharama ya mafunzo, lakini hayakufanyika. Pia,  sh. bilioni 3.304, zililipwa kama gharama za
matengenezo , lakini hayakufanyika,”ilisema ripoti hiyo ya CAG.
Ilisema hapakuwa
na uthibitisho wa mzabuni kama alilipa kodi TRA, yenye thamani ya sh. bilioni
2.251, kati  ya sh. bilioni 5.757,
zilizopaswa kulipwa licha ya mzabuni kupata msamaha wa kodi kutoka TRA wa sh. bilioni
3.506, katika mkataba wa sh. bilioni 37.743.
Ripoti hiyo
iliendelea kubainisha kuwa, baadhi ya gharama 
za vifaa  kwenye mkataba  zilikuwa juu ya bei ya soko, hali
iliyosababisha hasara  ya sh. bilioni
5.964.
CAG ilipendekeza
kuwa Idara ya Uhamiaji na TRA zifanye tathmini 
ya kina kama Lugumi alilipa kodi zote zinazostahili katika mkataba.
 
 
No comments:
Post a Comment