RAIS wa Zambia, Edgar Lungu, anatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa kwa ziara ya siku tatu, kufuatia mwaliko wa Rais Dk. John Magufuli, ambapo atatembelea maeneo muhimu ya ushirikiano wa kiuchumi na kutia saini mikataba minne.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni ule wa usafiri wa reli kupitia Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Ujio Rais Lungu ni fursa pekee katika kukuza uchumi wa nchi hizo kwa sababu Zambia ni miongoni mwa washirika wa kimkakati kwenye nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika, kwa kupitisha mizigo pamoja na mafuta kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Mbali na ushirikiano wa kiuchumi, Tanzania na Zambia zimekuwa kwenye mahusiano ya kipekee tangu Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Keneth Kaunda, walipoanzisha harakati za ukombozi wa uhuru kwa nchi za kusini mwa Afrika, kupitia muungano waliouita Mulungushi Club.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alisema Rais huyo wa Zambia atatembelea bomba la mafuta linalosafirisha nishati hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Zambia kisha kufanya mazungumzo na Rais Dk. Magufuli.
“Bomba hilo licha ya kusafirisha mafuta ghafi, lakini kwa teknolojia ya kisasa, tutafanya mazungumzo kuangalia uwezekano wa kutumika kusafirishia mafuta yaliyosafishwa pamoja na gesi kwenda kwenye mikoa ya Kusini mwa Tanzania hadi Zambia, kwa kutumia bomba hilo hilo au kufanya upanuzi.
“Lakini pia baada ya kutembelea bomba hilo, Rais Lungu atatembelea Bandari ya Dar es Salaam, katika eneo linalotumika kuhifadhia mizigo ya Zambia na kushuhudia namna, ambavyo serikali ya awamu ya tano ilivyofanya maboresho ya utoaji huduma,” alibainisha.
Balozi Mahiga alifafanua kuwa, kiongozi huyo akiwa na mwenyeji wake Rais Dk. Magufuli, watatia saini mikataba minne ya ushirikiano baina ya nchi hizo, ikiwemo usafiri wa reli kupitia TAZARA, mafuta pamoja na huduma za bandari kisha ataondoka nchini Oktoba 29, mwaka huu.
MABORESHO TAZARA
Tayari Tanzania na Zambia zimeanza mkakati wa kuboresha muundo wa TAZARA, ikiwemo kufanyia mabadiliko sheria iliyounda mamlaka hiyo ili kuendana na wakati.
Aidha, kupitia makubaliano yaliyofanyika baina ya Rais Rungu na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, mwaka jana, walipokuwa nchini Zambia, walikubaliana kubadili namna ya kufanya uteuzi wa nafasi za mkurugenzi mtendaji na naibu wake.
Kupitia utaratibu mpya, nafasi hizo zitatangazwa na waombaji kufanyiwa tathimini kwa mujibu wa sifa na taaluma katika uendeshaji kwenye sekta ya usafiri wa reli.
Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Grace Mujuma, alisema bado nchi hizo zinakabiliwa na changamoto katika uchangiaji fedha za kuendesha shirika hilo, lakini baada ya kufanyika maboresho katika uendeshaji, TAZARA imeanza kuimarika.
“Zamani ilikuwa inachukua hata wiki mbili kwa mizigo au abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Zambia, lakini sasa ni siku nne pekee ndizo zinazotumika.
“Tatizo la TAZARA lilikuwa ni udhaifu kwenye menejimenti, sasa uteuzi wa wakuu wa shirika hilo utajikita kwenye weledi na ndio maana menejimenti iliyopo, inafanyakazi vizuri baada ya kuanza utaratibu mpya wa uteuzi,” alieleza.
Reli hiyo ni miongoni mwa reli za mwanzo Afrika, kuwa kwenye kiwango cha standard gauge, ambayo ilijengwa kwa msaada na serikali ya China, miaka ya 1970.
Ujenzi wake ulifanyika ili kurahisisha shughuli za uchukuzi wa mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia, baada ya serikali za kikaburu za Afrika Kusini pamoja na Southern Rhodesia (Zimbabwe), kuiwekea vikwazo Zambia, kutokana na kushiriki kwenye harakati za ukombozi.
Reli hiyo, maarufu kwa jina la reli ya ukombozi au uhuru, imekuwa kiunganishi cha kipekee kwa mataifa ya Kusini mwa Afrika, kwani kupitia reli hiyo, abiria au mizigo inaweza kusafirishwa kutoka Tanzania hadi Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment