Friday, 25 November 2016

MAJALIWA: TUTAHAKIKISHA HAKI ZA WAFANYAKAZI ZINALINDWA




WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali chini ya Rais Dk. John Magufuli, itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa.

Pia, amewaagiza viongozi wa kisiasa nchini katika wizara mbalimbali, mikoa, wilaya, idara za serikali, halmashauri na taasisi zote za serikali, kuzingatia utawala wa sheria katika kushughulikia masuala yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi.

Alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), ambao pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angelah Kairuki.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwaasa wafanyakazi kote nchini kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika maeneo yao ya kazi ili kuleta tija kwa taifa na wananchi kwa ujumla.

Alisema ni dhahiri kuwa hivi sasa nidhamu ya kazi imeporomoka kidogo kutokana na watumishi kutotimiza wajibu wao kikamilifu huku wengine wakifanya ubadhirifu wa mali za serikali.

Majaliwa alisema kamwe serikali haitawafumbia macho, badala yake itaendelea kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.

Akizungumzia mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, Waziri Mkuu Majaliwa alitoa maagizo kwa waajiri wote nchini kutoa mikataba hiyo mara moja kwa wafanyakazi wao.

Pia, aliwaagiza maofisa wa kazi nchini kuhakikisha kila mwajiri anafikiwa na hatua stahiki anazijua ili kumpa mwajiriwa wake.

No comments:

Post a Comment