Friday, 25 November 2016

WANAOMKOSOA FK. SHEIN KATIKA MAFUTA, GESI WAMEZIDIWA-AFP

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

CHAMA cha Wakukima Tanzania (AFP), kimesema Rais Dk. Ali Mohamed Shein wa Zanzibar, hajavunja katiba wala sheria kwa kutia saini muswada wa uchimbaji mafuta kuwa sheria.

Kimesema wanasiasa wanaoeneza maneno hayo, wanaonyesha majuto yao baada ya kufungwa goli la kisigino.

Pia, chama hicho kimesifu msimamo wa rais huyo kwa kufanikiwa jina lake kuliingiza katika kurasa mpya za historia kutokana na hatua hiyo visiwani humo.

Mwenyekiti wa AFP, Said Soud Said, alitoa msimamo huo jana, katika ofisi ya jimbo ya chama hicho, iliyoko Chukwani, nje kidogo ya Unguja, na kusisitiza kuwa mafuta yatakapoanza kutafutwa na kuchimbwa, maisha ya Wazanzibari kiuchumi yatabadilika.

Soud alisema Rais Dk. Shein ametia saini Muswada wa Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia huku akionyesha msisitizo na kujiamini kwamba, Katiba ya Tanzania haikuvunjwa na suala hilo lina baraka zote kisheria.

"Sheria ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia wa mwaka 2016, utaratibu wote ulifuatwa wakati wa mchakato wa kutungwa kwa sheria, wanasiasa waonapiga mayowe wameachwa solemba na kufungwa goli la kisigino,"alisema.

Alisema masharti ya kifungu cha nne cha Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia 2015 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinataja shughuli za uendeshaji wa mafuta na gesi asilia utafanywa Zanzibar kwa kusimamia na kuendeshwa kitaasisi kwa mujibu wa Sheria za
Zanzibar, siyo vinginevyo hivyo hakuna kilichokiukwa.

“Nawaasa Wazanzibari wenzangu tusikubali kugawanywa na wanasiasa waroho wa madaraka waliokuwa na ndoto ya kuhodhi hisa na visima vya mafuta, wangepata madaraka na mpango wa kukomba mafuta wangefumba midomo yao, wanapaza sauti baaada ya kuzidiwa kete,” alisisitiza Soud.

Mwenyekiti huyo wa AFP aliwataka wananchi wasikubali kuyumbishwa wala wasibabaishwe na watu wasioitakia mema Zanzibar, kwa kuwa sheria hiyo itafungua fursa za kimaendeleo kwa kampuni nyingi kujitokeza kuanza kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi
asili visiwani humo.

Alisema wapo baadhi ya wanasiasa wa Zanzibar, hawapendi kuwaona wenzao wakifanya jambo jema na kutaka kila kitu waonekane wao ndiyo wajuzi wa mambo au wenye akili na maarifa, hivyo wanapoona wengine wanaleta maajabu kimaendeleo, hupotosha ukweli na
kuudanganya umma kwa maslahi yao.

Aidha, kiongozi huyo, ambaye pia ni Waziri Asiye na Wizara Maalumu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), alisema Rais Dk. Shein ana dhamira njema, mipango na malengo ya kuwaendeleza kiuchumi wananchi wa Unguja na Pemba, tofauti na wengine ambao hupigania maslahi ya waliopinduliwa.

"Tangu mwaka 1963, Zanzibar kulionekana dalili za kuwepo mafuta Unguja na Pemba, marais wote hawakushughulikia suala hilo, Dk. Shein sasa amethubutu na atafanikiwa kuiletea neema Zanzibar hata baaada ya kuondoka kwake madarakani,"alisema Soud

Aliwataka Wazanzibari kuwa makini, watulivu, wenye subira na matumaini kwa sababu utafutaji na uchimbaji wa mafuta, aghalabu huandamwa na fitina, majungu na mgawanyiko kama ilivyotokea Delta nchini Nigeria.

Pia, alisema pamoja na kuwepo kwa matumaini ya kupatikana mafuta, ni muhimu kuendelezwa kwa kilimo cha karafuu na minazi kwani mazao hayo yataisaidia Zanzibar kiuchumi na watu wake pamoja na kilimo cha matunda na manukato.

Rais Dk. Shein aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, Septemba, 2016, Sera ya Mafuta na Gesi ilisharidhiwa na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha rasmi Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta ya Zanzibar, ambayo sasa ameitia saini kuwa sheria na kuanza kutumika.

No comments:

Post a Comment