Tuesday, 22 March 2016

DK. KEBWE AZUIA UINGIZAJI MIFUGO MOROGORO, AMTUMBUA JIPU MHANDISI WA WILAYA



MKUU wa mkoa Morogoro, Dk. Steven Kebwe, amepiga marufuku uhamishaji wa mifugo kutoka mikoa mingine kuingia mkoani Morogoro, hadi mchakato wa mpango wa matumizi bora ya ardhi utakapokamilika.
Dk. Kebwe alitoa agizo hilo jana, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa tarafa ya Ngerengere, mkoani hapa.
Mkuu wa mkoa alikwenda Ngerengere kuipongeza kamati  iliyofanikisha upatikanaji wa ng'ombe walioibwa Februari, mwaka huu, na kuzuia mapigano baina ya jamii ya wafugaji wa kimang'ati na wamasai katika kijiji cha Matuli, wilayani Morogoro.
Aidha, Dk. Kebwe alipiga marufuku uhamishaji wa mifugo katika wilaya na  vijiji vya mkoa wa Morogoro, hadi mpango huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni katika wilaya za Malinyi,Ulanga na Kilombero, utakapokamilika.
Dk. Kebwe pia  aliwaagiza wakuu wa wilaya zote za Morogoro, kulisimamia kikamilifu agizo hilo katika kipindi hiki ili kuepuka migogoro inayoweza kukwamisha mchakato huo.
"Lengo la agizo hili la kuzuia mifugo kuingia mkoani hapa kwa sasa ni kuwezesha zoezi la upimaji liweze kufanikiwa bila vikwazo na hatimaye kumaliza kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani hapa,"alisema.
Dk. Kebwe alitoa wiki mbili kwa jeshi la polisi mkoani hapa, kuukamata mtandao mzima ulioshiriki katika wizi huo na kuagiza kukamatwa mara moja kwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Lamba, kilichoko kijiji cha Matuli, kata ya Ngerengere, Cosmas Kidebe.
Mwenyekiti huyo anatuhumiwa kutochukua hatua dhidi ya watu waliongia na kuishi kitongojini kwake, bila kufuata utaratibu na ambao ndio  wanaosadikiwa kuwa waliiba ng'ombe hao.
Aliishukuru kamati iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Muhingo Rweyemamu, kwa kuweza kuzuia mapigano baina ya kabila la wamasai na mang'ati na kufanikisha kukamatwa kwa ng'ombe walioibwa.
Aliishauri kamati hiyo kujiimarisha na kujitanua kwa kujumuisha wakulima na wafugaji wa makabila yote, ili kukomesha kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani hapa.


Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, amemsimamisha kazi Mhandisi wa Wilaya ya Morogoro, ili kupisha uchunguzi wa matumizi mabaya ya sh. milioni 19.
Fedha hizo ni zile alizopatiwa mhandisi huyo kwa ajili ya matengenezo ya soko la Ngerengere, baada ya kuezuliwa na upepo.
Dk. Kebwe alimsimamisha kazi mhandisi huyo juzi, wakati alipofanya ziara ya kikazi katika tarafa ya Ngerengere,  ikiwa ni ziara yake ya kwanza baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo.
Mbali na kumsimamisha kazi mhandisi huyo,  Dk. Kebwe pia aliusimamisha uongozi wa Chama cha Kuweka na Kukopa   cha Ngerengere Saccos,  kwa kushindwa kukisisamia ipasavyo wakati walipewa dhamana ya kukiendesha.
Aidha, aliwataka viongozi wa saccos hiyo  kutoa maelezo kwanini imekufa na fedha zake zimepotelea wapi.
Dk. Kebwe alifikia uamuzi huo ili kupisha uchunguzi baada wananchi kutoa malalamiko kwake kuhusu kutoridhishwa na ukarabati wa soko hilo. 
Mkuu huyo wa mkoa aliamua kutembelea soko hilo ili kulikagua, ambapo alibaini  mapungufu kadhaa ya kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kujengwa chini ya kiwango.
Hata hivyo, Dk. Kebwe alibaini kuwa baadhi ya malalamiko yaliyotolewa na wananchi hayakuwa ya kweli, hivyo kuagiza wakamatwe mara moja ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia  ya kufanya mzaha kwa viongozi wa serikali.
Akiwa Ngerengere, Dk. Kebwe pia alifanya  kikao cha pamoja na wafugaji na kupiga marufuku kuingizwa kwa mifugo ya aina yeyote mkoani humo pamoja na upigaji wa muziki nyakati za usiku.
Alisema upigaji wa muziki nyakati za usiku umekuwa na athari kubwa, ikiwa ni pamoja na kuchangia kufeli kwa wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha nne.

No comments:

Post a Comment