CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Morogoro, kimewavua uanachama wanachama 29 na kuwaondoa
kwenye uongozi wengine 21, katika
ngazi mbalimbali mkoani hapa, baada ya kubainika walikisaliti Chama wakati
wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Katibu
wa CCM mkoa wa Morogoro, Rojas Romuli, alisema hayo jana, wakati akitoa taarifa
ya kikao cha kamati ya siasa ya mkoa kilichoketi Machi 13, mwaka huu, mjini
hapa.
Alisema
adhabu hiyo ni miongoni mwa zilizotolewa kwa wanachama mbalimbali wakati
wa kikao hicho, baada ya kamati ya siasa ya CCM mkoa, kupokea na kujadili
tathmini ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Romuli
alisema kikao hicho kiliamua kuwaondoa kwenye uongozi baadhi ya wanachama na
wengine kuwavua uanachama huku baadhi yao wakipewa onyo kali.
Alisema
viongozi waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na waliokuwa makatibu wa kata,
wenyeviti wa kata, wenyeviti serikali za vijiji, makatibu uenezi wa kata na
wenyeviti wa vitongoji.
Wengine
ni wajumbe wa halmashauri za vijiji, wajumbe wa serikali za vijiji, mabalozi wa
shina, wajumbe wa kamati za siasa za kata na wanachama wa kawaida.
Alisema
wanachama na viongozi hao walikiuka taratibu za CCM na kufanya makosa
mbalimbali, ikiwemo usaliti, uzembe na kutowajibika.
Aidha,
alisema kikao hicho pia kilijadili na kubaini mapungufu kadhaa kwa baadhi ya
wanachama na kuwavua uanachama wanachama 29 na wengine 42 kupewa onyo kali
wakati wengine 13 walipewa onyo la mdomo.
Katibu
huyo alisema kamati hiyo ya siasa pia imewafutia adhabu wanachama watano,
kutokana na tuhuma zao kutothibitika.
Hata
hivyo, alisema vikao vya mkoa na taifa
vinatarajia kufanya maamuzi ya mwisho kwa viongozi 11 wanaotuhumiwa kwa makosa
mbalimbali, baada ya kujiridhisha juu ya ukweli wa tuhuma zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment