Friday, 16 October 2015

POLEPOLE AWACHANA SUMAYE NA KINGUNGE

NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
WATANZANIA wametakiwa kumpuuza Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye  na Kingunge Ngombale Mwiru, kwani ni viongozi ambao hawaamini na kusimamia kauli wanazotoa mbele ya umma.

Imeelezwa viongozi hao walikuwa vinara wa kumpinga Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, ambapo Kingunge alidai wanaomwuunga mkono Lowassa wanastahili kupimwa akili.

Kauli hiyo ilitolewa na aliyekuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Humphrey Polepole, wakati akijibu hoja na maswali mbalimbali aliyoulizwa na washiriki wa mdahalo wa kumbukumbu ya miaka 16, ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, uliofanyika jana mjini Mbeya.


Alisema wakati wa mchakato wa Katiba, waliamua kumtafuta Kingunge kwa ajili ya kupata ushauri, ambapo katika kikao hicho kulikuwa na wawakilishi kutoka UKAWA, Jaji Joseph Warioba, Joseph Butiku na wajumbe wengine wa tume.

Polepole alisema katika kikao hicho, Kingunge aliwashaure wajumbe kuheshimu mawazo ya tume.

Alisema Kingunge alikwenda katika Bunge Maalum la Katiba na kuwaeleza wajumbe kuwa Lowassa na kundi lake wanastahili kupimwa akili kwa kutaka rasimu ibadilishwe, lakini hivi sasa wanadai wanataka mabadiliko.

Hata hivyo, alisema Sumaye alitumikia nafasi ya uwazi mkuu kwa miaka kumi mfululizo, lakini ndiye aliyepingwa na Watanzania wengi kupewa nafasi hiyo ya juu.

Alisema Sumaye kupitia gazeti la Mawio la Juni 4-10, mwaka huu, alinukuliwa akiahidi kujiuzulu uanachama wa CCM, iwapo Lowassa atateuliwa na chama kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.


“Kaka na rafiki yangu Said Kubenea, ambaye ndiye aliyeandika habari hiyo ikiwa na kichwa cha habari ‘Sumaye atikisa urais’,  ambapo aliandika CCM, kitapoteza mmoja wa viongozi wake muhimu, iwapo kitateua mtuhumiwa wa wizi na matumizi mabaya ya madaraka kuwa mgombea wake wa urais,” alisema.

Alisema Sumaye ndiye waziri mkuu aliyepingwa zaidi na wananchi asipewe hiyo kazi, lakini Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, alimvumilia kwa vipindi vyote viwili.


Alisema Mkapa aliwaeleza Watanzania kuwa hana neno zuri la kuwaita watu aina ya Sumaye zaidi ya kuwaita wapumbavu.

Sumaye alisema nafasi ya urais ni nafasi kubwa nchini na kwamba ina kazi nyingi na lawama kubwa, hivyo anayegombea nafasi hiyo ni lazima awe amejiangalia na amejiandaa kiafya, kiakili, kisaikolojia na kidhamira.

Watakiwa kuchagua viongozi wenye hofu ya Mungu

WATANZANIA wameaswa kuwachagua viongozi wenye hofu ya Mungu, kwani wakiingia madarakani wanaweza kuingiza nchi kwenye machafuko na kumwagikaji wa damu.

Pia viongozi watakaochaguliwa kama wawakilishi wa Watanzania ni wale ambao wataleta mabadiliko ya kweli na siyo kuwatenganisha kikabila, wala kidini.

Kiongozi wa Waislam dhehebu la Shia Ithnashar Tanzania, Sheikh Hemed Jalala, alisema hayo juzi, wakati wa maadhimisho ya mwaka mpya 37 wa Kiislamu.

“Tunataka viongozi ambao tukiwachagua kwenda Ikulu au bungeni hawatatugawa kidini, kikabila wala ubaguzi wa rangi, kwani Watanzania tumezoea umoja, kusikilizana na maelewano,’’ alisema.

Alisema sifa za kiongozi wa nchi ni yule ambaye anawapenda Watanzania wote na yeye kupendwa.

Sheikh Jalala alisema  aliwataka wananchi kumuenzi hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye ameacha tunu ya amani.


No comments:

Post a Comment