Friday, 16 October 2015

MAGUFULI AAHIDI KUTEUA MAWAZIRI NGANGARI



Na Rashid Zahor


MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema atahakikisha Baraza la Mawaziri atakaloliunda baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linakuwa na mawaziri wanaofanana na yeye kiutendaji.

Amesema hatakuwa tayari kuwateua mawaziri ambao kazi yao itakuwa ni kukaa tu ofisini na kuandika madokezo, badala yake atateua mawaziri wachapakazi na atakuwa akifuatilia utendaji wao wa kazi kwa karibu.

“Kabla sijamteua mtu kuwa waziri, nitamwuuliza kwanza utaweza kazi hii? Akisema nitaweza, ndipo nitamwambia tiasaini hapa. Kama hawezi aseme mapema.
"Nataka kama ni waziri wa maji, atembelee miradi ya maji, sio kukaa ofisini. Na kama ni waziri wa elimu, atembelee wanafunzi aone matatizo yanayowakabili. Serikali yangu itakuwa ya kazi tu," alisema Dk. Magufuli.

Aidha, Dk. Magufuli alisema amebaini mbinu chafu zinazofanywa na baadhi ya mafisadi nchini, kuwahonga wananchi ili asichaguliwe kuwa rais, lakini amesisitiza kuwa mbinu hizo hazitaweza kufanikiwa.

Dk. Magufuli alisema hayo jana, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni wa uchaguzi mkuu, uliofanyika katika Jimbo la Kisarawe, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani.

Mgombea huyo alisema atakuwa mkali kwa watu wachache wanaotumia madaraka yao vibaya na kuwanyanyasa watu wa chini yao, kwa vile amebaini kuwa wapo watu wachache, ambao wamekuwa wakitumia ofisi zao kuwanyanyasa  wengine.

Dk. Magufuli alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiichukia serikali yao kwa sababu ya watu wachache, hivyo atakapochaguliwa kuwa rais, hawezi kuwavumilia watu wa aina hiyo.

"Mimi siyo mkali kama baadhi ya watu wanavyosema, isipokuwa ni msimamizi makini," alisisitiza.

Alisema mafisadi wanaotumia pesa kutaka kuwahonga wananchi siku ya kupiga kura ili asichaguliwe kuwa rais, wamechelewa, kwa vile wananchi wameonyesha kuwa na imani kubwa kwake na ana uhakika mkubwa wa ushindi.

"Ukipewa fedha zipokee kwa sababu ni za kifisadi, walituibia, lakini pesa kula, kura yako mpe Magufuli," alisema mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi.

Alisema athari ya kununuliwa kwa pesa ni maisha ya mateso baadaye, kwa vile watu wa aina hiyo hawana dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi zaidi ya kuwatumia na kuwanyonya.

Aliwapongeza vijana waliopiga deki barabara wakati mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa, alipofanya ziara mkoani Mara hivi karibuni, kwa vile barabara hiyo imejengwa na serikali ya CCM chini ya usimamizi wake akiwa Waziri wa Ujenzi.

"Huwezi kupiga deki barabara ya vumbi au mlimani. Nawaomba vijana hawa waendelee kupiga deki barabara zilizojengwa na CCM hata baada ya uchaguzi ili ziendelee kuwa safi," alisema mgombea huyo.
Katika mkutano huo, ulioanza saa 2.30 asubuhi, Dk. Magufuli aliwaahidi wakazi wa Kisarawe kuwa atahakikisha barabara ya Kisarawe/Mlandizi na ile ya Kisarawe/ Manerumango, zinajengwa kwa kiwango cha lami.

Alisema lengo la serikali yake litakuwa kuufanya mkoa wa Pwani, hasa wilaya ya Kisarawe, ifanane na mkoa wa Dar es Salaam, kutokana na mikakati iliyobuniwa na uongozi wa Halmashauri ya Kisarawe.

Aliwapongeza viongozi wa halmashauri hiyo kwa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu na viwanda 250. Alisema miradi hiyo miwili itasaidia kuongeza ajira kwa vijana na hivyo kujikwamua kimaisha.

"Nawapongeza sana viongozi wa halmashauri kwa kutenga eneo la viwanda kwa sababu uchumi wa nchi unakuzwa na viwanda. Nchi kama Marekani na China, uchumi wake unategemea zaidi viwanda," alisema.

Dk. Magufuli pia aliahidi kuongeza bei ya zao la korosho ili liweze kuwanufaisha wakazi wa wilaya hiyo, kwa vile ni miongoni mwa mazao yao makubwa ya kibiashara.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Moshi Bara, ulioko Mombasa, katika Jimbo la Ukonga, Dk. Magufuli aliwashangaa baadhi ya wanasiasa wanaobeza maendeleo yaliyoletwa na CCM.

Alisema watu wanaobeza maendeleo hayo, yakiwemo ujenzi wa barabara, usambazaji wa huduma za maji na umeme, wana matatizo na wanaota ndoto mchana.

"Ukimwona mtu anaota mchana, ujue ugonjwa wa kichaa unamkaribia. Ni sawa na yule anayeahidi kumaliza msongamano wa magari Dar es Salaam kwa siku 100. Huyu hayuko sawasawa," alisema mgombea huyo.
Mkutano huo ulioanza saa 4.30 asubuhi na kumalizika saa 5.40, ulihudhuriwa na mamia ya wananchi, ambao muda wote Dk. Magufuli alipokuwa akiwahutubua, waliimba  'rais...rais....rais.'

"Ukonga mmenikonga moyo wangu. Nimefurahi sana kwa mapokezi mliyonipa kuanzia njia panda hadi hapa. Watu wamenisindikiza kwa maandamano. Mapokezi niliyoyapata siwezi kuyasahau," alisema Dk. Magufuli.

Awali, msafara wa Dk. Magufuli ulizuiwa mara nne na wananchi wakati ukiingia njia panda ya kutokana barabara ya Nyerere, ambapo alilazimika kuwahutubia na kunadi sera.

Kutokana na kufurahishwa na mapokezi hayo, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi hao kwamba ataijenga barabara ya Ukonga/ Mombasa na ile ya Banana/Kitunda hadi Kivule kwa kiwango cha lami, ahadi iliyoamsha shangwe na vifijo kwa wananchi.


Dk. Magufuli pia aliahidi kuimarisha usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam, ili upunguze tatizo la usafiri. Pia aliahidi kufikisha umeme katika maeneo yote ya Dar es Salaam, ambayo hayajafikiwa na nishati hiyo.

Aliwataka wananchi hao wamwamini kwa sababu si kawaida yake kusema uongozi, lakini ili aweze kutekeleza ahadi hizo, aliwaomba kumpa kura nyingi siku ya uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment