Na Rashid Zahor
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema kutiwa saini kwa mkataba wa ujenzi wa barabara za juu zitakazoanzia eneo la TAZARA, Dar es Salaam ni ishara kuwa kazi imeanza.
Dk. Magufuli amesema amefarijika kuona kuwa mkataba huo umetiwa saini akiwa Waziri wa Ujenzi na hiyo ni ishara kwamba rais ajaye atakuwa kazi tu.
Amesema ujenzi wa barabara hizo za aina yake ni mwanzo mzuri wa jitihada za serikali katika kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Dk. Magufuli alisema hayo jana, kabla ya kutia saini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kati yake na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo ilifanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Japan (JICA), Toshio Nagase, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Joseph Nyamhanga, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Injinia Patrick Mfugale na Meneja Mkuu wa Kampuni ya SUMIMOTO ya Japan, itakayosimamia ujenzi wa barabara hizo.
Dk. Magufuli aliishukuru serikali ya Japan kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya ujenzi na zinginezo na kuongeza kuwa, huo ni uthibitisho wa wazi wa uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo.
"Watu walisema haitawezekana kwa barabara za Tanzania kujengwa flyovers, lakini sasa imewezekana," alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, ujenzi wa barabara hizo utagharimu sh. bilioni 100 na kwamba fedha hizo zimetolewa na serikali ya Japan, JICA na Tanzania.
Alisema ujenzi wa barabara hizo unatarajiwa kuchukua miezi 35 na kwamba unatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao.
"Naishukuru sana serikali ya Japan kwa sababu imekuwa ikituunga mkono katika miradi mbalimbali hapa nchini," alisema.
Aliongeza kuwa serikali ya Japan pia imejitolea kusaidia ujenzi wa barabara ya Mwenge/Tegeta, unaotarajiwa kugharimu sh. bilioni 38. Barabara zingine, ambazo Japan imeahidi kusaidia ujenzi wake ni Mwenge/Morocco na Rangitatu/TAZARA.
Dk. Magufuli alisema ujenzi wa barabara hizo utakapokamilika, zitakuwa za kwanza za aina yake nchini na kwamba lengo la serikali ni kuendelea kujenga barabara hizo katika maeneo ya Chalinze na Morogoro.
"Lengo la kwanza la serikali lilikuwa kuunganisha nchi nzima kwa mtandao wa barabara za kiwango cha lami na tayari hilo limefanyika. Baadaye tukaanza ujenzi wa madaraja, ambapo 12 makubwa yameshamalizika na tunaendelea na mengine, likiwemo daraja la Kigamboni," alisema.
Dk. Magufuli alisema atakapochaguliwa kuwa rais, atafuatilia ujenzi wa barabara hiyo ya flyover, ili iweze kumalizika kwa haraka kwa vile hakuna sababu ya ujenzi wake kuchelewa huku fedha zikiwepo.
"Natamani kuimba na kushangilia kwa sababu mradi huu ni muhimu sana. Utasaidia kupunguza msongamano wa magari Dar es Salaam," alisema.
Aliwataka Watanzania waiamini serikali yao na kuitaka TANROADS iendelee kusimamia miradi ya barabara kwa umakini na kuhakikisha inajengwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Aliwashukuru balozi wa Japan nchini na mwakilishi wa JICA, ambao alisema licha ya ugeni wao, wameanza vizuri kazi zao.
Awali, Balozi wa Japan nchini, Masaharu aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kutumia vizuri misaada wanayopewa na nchi hiyo.
Naye Mwakilishi wa JICA, Toshio alisema shirika hilo lilianza kusaidia ujenzi nchini mwaka 1984, wakati wa ujenzi wa Salender na kwamba, ipo tayari kuendelea kuisaidia serikali ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment