Na Mwandishi Wetu
SIKU kadhaa baada ya kuenguliwa kuwania nafasi ya ubunge wa Masasi, mkoani Mtwara, kwa njia ya ‘mahakama za wananchi’, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Dk. Emmanuel Makaidi (74), amefariki dunia kutokana na shinikizo la damu.
Makaidi alifariki dunia jana, kwenye hospitali ya Nyangao, wilayani Lindi, alikolazwa kutokana na tatizo hilo ambalo hata hivyo halijathibitishwa na madaktari, ila na wanafamilia.
Taarifa zinasema Dk. Makaidi alikumbwa na matatizo ya kiafya baada ya kupandishwa jukwaani na mgombea wa urais wa CHADEMA, Edward Lowassa na kumpambanisha na mgombea wa CUF, Ismail Makonde, maarufu kama ‘Kundambanda’, hali inayoonyesha alipatwa na mshituko.
Mgombea urais huyo wa CHADEMA anayeungwa mkono na UKAWA, alimwomba mwenyekiti mwenza huyo, Makaidi, kujitoa kugombea ubunge na kumwachia Makombe baada ya kukataliwa na wananchi.
Uamuzi huo ulifikiwa katika uwanja wa Bomani, mjini Masasi, baada ya Lowassa kuwasimamisha wagombea hao jukwaani kuwanadi, lakini akapata upinzani kutoka kwa wananchi alipompa nafasi Dk. Makaidi.
Hata hivyo, kabla Makaidi hajasema lolote, aliondoka kwenye mkutano huo na meza kuu ilijadiliana, ndipo mkewe, Modesta aliposhauri waachwe wote wawili wachuane, hoja ambayo ilikubaliwa na Lowassa, ambaye alitangaza tena kuwa wagombea hao kila mmoja atapambana kivyake.
Awali, Lowassa alipotoa uamuzi wa kumwomba Dk. Makaidi amwachie kijana huyo, uwanja mzima ulilipuka kwa nderemo na vifijo, huku wananchi wakinyoosha mikono kukubaliana na uamuzi huo. Lakini, alipobadilisha uamuzi huo, umati ulionekana kutomwuunga mkono.
Dk. Makaidi alipopewa nafasi ya kuzungumza, wananchi walipiga kelele, huku wakinyosha mikono juu kumkataa na kukatisha hotuba aliyokuwa ameanza kuitoa.
Lakini aliposimamishwa Kundambanda, alishangiliwa, huku akimweleza Lowassa kuwa kura zake za urais anazo mfukoni kwa kuwa ndiye wananchi wanayemkubali.
Mgombea wa CHADEMA katika jimbo hilo, Mussa Sakaredi aliamua kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho, ili kumuunga mkono mgombea aliyepitishwa na UKAWA.
Mapema kabla ya mkutano huo, wananchi walimkataa Dk. Makaidi, ambaye alikuwa amepitishwa na Kamati Kuu ya UKAWA, kwa madai kwamba si chaguo lao, huku wakimbeba juu juu Kundambanda, aliyewasili katika mkutano huo akiwa amevalia sare mithili ya zile zivaliwazo na askari wa kikosi cha usalama barabarani.
Polisi waliokuwa wakilinda mkutano huo, wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Masasi, baada ya kuona hali ya usalama kwa mgombea huyo inakuwa tete, walimzingira na kumwondosha uwanjani hapo, huku baadhi ya wanachama na wafuasi wa vyama washirika wa UKAWA wakiendelea kuimba.
Sakata la kuzomewa Makaidi, inadaiwa lilimkasirisha Lowasa kutokana na kutia doa mbio zake za urais kwa vile wafuasi wa CUF walikuwa wakiimba pia "hatumtaki Lowassa."
Kutokana na tukio hilo, Lowasa alimwagiza Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe awasiliane na Makaidi, ili aachie jimbo hilo na badala yake atangazwe Kundambanda ,ili kuwaridhisha wafuasi wa CUF.
Baada ya kupata taarifa za kusimamishwa na kuondolewa kugombea ubunge, inadaiwa alikaririwa akisema asingekubaliana na uamuzi huo, kwa vile wafuasi walioshinikiza Kundambanda atangazwe mgombea wa UKAWA walitumwa na viongozi wa CUF.
Hali ilikuwa hivyo hata Ndanda, ambako mgombea mmoja kati ya wawili wa UKAWA waliojitokeza kuwania ubunge, kukataliwa na wananchi mbele ya Lowassa na kumfanya akimbie jukwaa.
Hiyo ilijitokeza baada ya Meneja wa Kampeni wa CHADEMA, John Mrema kusema ana habari za kuwepo mgogoro wa nani agombee ubunge chini ya UKAWA kati ya NLD na CHADEMA, hivyo akatoa nafasi kwa kila mgombea kueleza matatizo ya jimbo hilo jipya.
Mgombea wa NLD, Angelous Gabriel, aliishia kumsifu Lowasa, jambo lililofanya wananchi kupiga kelele wakisema anapoteza muda.
Lakini mgombea wa CHADEMA, Cecil Mwambe, alishangiliwa, huku akieleza kuwa katika jimbo hilo kuna tatizo la bei ya mazao, hivyo Lowasa akiingia madarakani, serikali yake itatakiwa iwatatulie matatizo yao.
Baada ya Mwambe kusema hayo, wananchi walimshangilia na Lowasa alipopanda jukwaani aliwaita wagombea hao na kisha kuhoji wananchi wanamtaka nani kati yao, ambapo kwa sauti ya pamoja walijibu “Mwambe.”
Hatua hiyo ilimfanya Gabriel ashuke jukwaani na kuondoka. Alipoulizwa sababu ya kukataliwa alisema: “Kuna watu wameandaliwa na kununuliwa ili nisigombee Ndanda.”
Hata hivyo, wakazi wa Ndanda walisema hawamjui mgombea huyo na wanashangaa kwa nini anang’ang’ania kugombea huku akiwa hajajiandikisha kupiga kura katika jimbo hilo.
Makaidi alizaliwa Aprili 10, 1941, wilayani Masasi, Mtwara.
Mkewe Modesta azungumza
Akizungumza na gazeti hilo jana, Modesta alisema Dk. Makaidi alifariki baada ya kusumbuliwa na shinikizo la damu.
Alisema mumewe alianza kusumbuliwa na tatizo hilo Jumanne na kupelekwa hospitali kwa matibabu na kwamba baadaye aliruhusiwa kurejea nyumbani.
Hata hivyo, alisema jana asubuhi hali yake ilibadilika ghafla na kulazimika kupelekwa tena hospitalini, lakini ilipofika saa saba, Mwenyezi Mungu alimchukua.
“Juzi alishinda nyumbani vizuri, lakini leo (jana) asubuhi, alianza kutojisikia vizuri, hivyo tulimpeleka hospitali ya Nyangao kupatiwa matibabu, lakini alifariki wakati akiendelea na matibabu,” alisema Modesta, ambaye alikuwa akiangua kilio.
Utaratibu wa mazishi utafanyika baada ya kuwasili kwa mtoto wao aliyeko Arusha na kwamba wanatarajia kuhamishia msiba Dar es Salaam.
Magufuli atuma salamu za pole
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ametuma salam za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Dk. Makaidi.
Salamu hizo za Magufuli zimekwenda pia kwa viongozi, wanachama na wapenzi wa kundi la UKAWA, ambako marehemu alikuwa ni mmoja wa wenyeviti wenza.
"Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Mzee Makaidi. Huyu ni mwanasiasa wa muda mrefu ambaye Watanzania wengi walimheshimu na wamesikitishwa na kifo chake hicho cha ghafla.
"Kwa niaba ya CCM, napenda kutuma salamu za pole kwa wote walioguswa. Mwenyezi Mungu aipe familia yake moyo wa subira na uvumilivu katika wakati huu mgumu ," alisema Dk. Magufuli katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment