Tuesday 13 October 2015

KIAMA CHA MELI ZA NJE ZINAZOKUJA KUVUA NCHINI BILA KIBALI KINAKUJA-MAGUFULI


MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amezionya meli za uvuvi kutoka nje ya nchi zinazokuja kuvua nchini bila kufuata sheria kwamba kiama chao kimewadia.

Dk. Magufuli pia amewaahidi wananchi wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi kwamba. lazima wafaidike kutokana na mabaki ya mjusi mkubwa kuliko wote duniani, yaliyovumbuliwa jimboni humo na kupelekwa kuhifadhiwa Ujerumani.

Mgombea huyo alitoa ahadi hizo jana, alipokuwa akihutubia mikutano mawili ya kampeni iliyofanyika katika jimbo la Mchinga na Kilwa mkoani Lindi.

Alisema meli za uvuvi zinazokuja kuvua kutoka nje ya nchi, zimekuwa zikiikosesha serikali mapato makubwa, hivyo atakapochaguliwa kuwa rais, atahakikisha analivalia njuga suala hilo na kulikomesha kabisa.

Dk. Magufuli alisema iwapo aliweza kupambana na tatizo hilo wakati alipokuwa Waziri wa Uvuvi na Mifugo, hawezi kushindwa akiwa rais, na kwamba atakachokifanya ni kuongeza mapambano dhidi ya uvuvi huo haramu.

"Nadhani mnakumbuka wakati tulipoikamata ile meli ya wazungu iliyokuja kuvua nchini kinyume cha sheria. Wanavua samaki wetu wengi na hivyo kutupotezea mamilioni ya fedha. Samaki mmoja anaweza kufika hadi kilo 300. Hatuwezi kulivumilia jambo hili,"alisema.

Alisema uchumi wa nchi umekuwa ukitegemea zaidi sekta ya uvuvi, lakini samaki wanaotegemewa na kuiingizia nchi mapato ni wale wa Ziwa Victoria mkoani Mmwanza.

Alisema iwapo meli za uvuvi kutoka nje zitataka kuendelea kuja kuvua nchini, zitalazimika kufuata taratibu, ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba na serikali ili iweze kupata mapato.

Dk. Magufuli alisema mapato yatakayopatikana kutokana na sekta hiyo ya uvuvi, yataisaidia serikali kuboresha huduma za maji, umeme na barabara kwa ajili ya kuwaletea maendeleo  wananchi.

MCHINGA WAAHIDIWA NEEMA

Akihutubia katika mkutano uliofanyika Nangalu, jimbo la Mchinga mkoani Lindi, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwasaidia kupata mapato kutokana na ada inayilipwa na watalii wanaokwenda Ujerumani kutazama mabaki ya mjusi mkubwa kuliko wote duniani.

Alisema kwa kuwa mjusi huyo alipatikana Mchinga, wakati umefika kwa wananchi wa jimbo hilo kufaidika kutokana na ada inayolipwa na watalii ili kuyashuhudia mabaki hayo.

"Nitaongea na serikali ya Ujerumani ili iwalipe wananchi wa Mchinga fidia kutokana na kuhifadhi mabaki ya mjusi huyo na kuwatoza ada wanaokwenda kumuangalia,"alisema.

Aidha. Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi hao kujenga barabara ya Mtange-Nangalu kama alivyoombwa na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Saidi Mtanda.

Alisema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe utawasaidia wananchi wa jimbo hilo kuongeza mapato kutokana na usafirishaji wa zao la ufuta kuwa rahisi.

Dk. Magufuli alisema alikubali kwenda Mchinga kwa kupitia barabara ya vumbi ili aone hali halisi ilivyo na baada ya kuiona, atahakikisha ujenzi wake unaanza mara moja.

Alimpongeza Mtanda kwa kuitumia vizuri miaka yake mitano ya ubunge kwa kuwezesha umeme kuvifikia vijiji 43 vya jimbo hilo, maji ya kutosha na minara ya simu.

Mgombea huyo alisema jimbo la Mchinga limejaliwa kuwa na rutuba nzuri kwa ajili ya kilimo, hivyo wanapaswa kulitumia vyema kwa kilimo cha ufuta ili waweze kuongeza vipato na kuboresha maisha yao.

Aliwaahidi wananchi hao kuwa atajitahidi kuongeza bei ya ufuta kwa kuwa ndilo zao kuu la biashara mkoani Lindi na iwapo litatumiwa vizuri, hali za maisha za wananchi zitakuwa nzuri.

"Kwa sasa maji yapo, umeme upo, vijana acheni kukaa vijiweni na kutegemea kushushiwa riziki , barabara ikijengwa, wafanyabiashara watafurika kuja kununua ufuta, hivyo ongezeni bidii katika kilimo cha zao hili,"alisema.

Aliwataka wananchi wa jimbo hilo wasibabaishwe na wapinzani kwa kuwa ni matapeli na hawana uwezo wa kuwaletea maendeleo.

"Wakati wa maisha mazuri unakuja, jukumu lenu ni moja tu, ifikapo Oktoba 25, mwaka huu, ichagueni CCM ili iwaletee maendeleo,"alisema.

Katika mkutano huo, wanachama 10 wa vyama vya upinzani kutoka CUF na CHADEMA walirejesha kadi zao na kujiunga na CCM.

Akiwa njiani kwenda Kilwa, msafara wa Dk. Magufuli ulisimamishwa na wananchim mara kadhaa na kulazimika kusimama na kuwahutubia.

Dk. Magufuli pia alitumia fursa hiyo kuwaomba kura abiria nwaliokuwua wakisafiri kwa basi kwenda Tunduru mkoani Songea.

Akihutubia mkutano wa kampeni Kilwa, Dk. Magufuli aliahidi kuufanya mji huo uwe wa kitalii ili kuwawezesha wananchi kuongeza mapato na kupata maendeleo zaidi.

Mgombea huyo pia alifichua mpango wa UKAWA kununua kura kwa wananchi siku ya kupiga kura, ambapo aliwataka kupokea fedha hizo, lakini kura wampe yeye na wagombea wote wa CCM.

Msafara wa Dk. Magufuli uliendelea kusimamishwa katika maeneo ya Malendego, Muhoro na Ikwiriri, ambapo wananchi walifunga barabara ili kutaka kumuona na kusikiliza sera zake.

No comments:

Post a Comment