Tuesday 13 October 2015

MAGUFULI: LAZIMA GESI IBORESHE MAISHA YA WANANCHI LINDI NA MTWARA


Na Rashid Zahor, Lindi

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewaahidi wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kwamba, atahakikisha gesi inayopatikana katika mikoa hiyo, inaanza kuwanufaisha wao.

Aidha, Dk. Magufuli amewaahidi wananchi wa Lindi kwamba atafanya upanuzi wa uwanja wa ndege wa mkoa huo ili uwe na hadhi zaidi kutokana na mji huo kwa sasa kuelekea kuwa wa kibiashara.

Mgombea huyo wa CCM pia ameahidi kuimarisha Bandari ya Lindi kwa lengo la kupanua wigo wa wafanyabiashara kusafirisha na kushusha bidhaa zao katika bandari yoyote wanayoitaka.

Dk. Magufuli alitoa ahadi hizo jana katika mkutano wake wa kampeni za kuwania urais, uliofanyika kwenye uwanja wa Mpilipili mjini hapa na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Mgombea huyo pia alisema hadi sasa ana uhakika wa ushindi katika uchaguzi mkuu kwa asilimia 90 na kwamba  iwapo atamaliza kampeni zake salama, atakuwa na uhakika wa ushindi kwa asilimia 99.

Alisema ahadi yake ya kuwapa kipaumbele wananchi wa Lindi na Mtwara kutokana na upatikanaji wa gesi, inatokana na ukweli kwamba, imeshaanza kuleta mafanikio kwa Watanzania.

Alisema tayari gesi hiyo imeshaanza kuleta mafanikio kutokana na kuzinduliwa kwa kiwanda cha saruji cha Dangote kilichoko Mtwara, ambacho kimewezesha bei ya saruji kupungua kutoka sh. 16,000 kwa mfuko mmoja hadi sh. 8,000.

"Tukishaanza kuwa na viwanda kama Dangote, tutaweza kupunguza bei za bidhaa mbalimbali kama vile saruji, mabati na misumari ili wananchi waweze kupata nafuu ya maisha,"alisisitiza.

Dk. Magufuli alisema kazi aliyoifanya katika utumishi wake wa miaka 20  serikalini kila mtu anaijua, hivyo aliwataka Watanzania wampigie kura kwa wingi ili aweze kuwaletea maendeleo.

Alisema serikali yake itaufanyia upanuzi uwanja wa ndege wa Lindi kwa kuwekewa lami kwa vile baada ya muda si mrefu, mkoa huo utaanza kutembelewa na wageni mbalimbali wa kimataifa.

Aidha, alisema hakuna ubaya kuiimarisha bandari ya Lindi kwa sababu hata kama zitakuwepo mbili pamoja na ile ya Mtwara, wafanyabiashara watakuwa na uwezo wa kushusha na kusafirisha mizigo yao katika bandari yoyote.

Aliwaeleza wananchi hao kuwa serikali zote kuanzia awamu ya tatu na ya nne, zimefanya mambo mengi ya kimaendeleo katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ikiwa ni pamoja na kujenga Daraja la Mkapa na barabara ya lami kutoka kwenye daraja hilo hadi Mingoyo.

"Wananchi wa Lindi na Mtwara walipata tabu sana ya usafiri. Safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi ilitakiwa kupangwa mwaka mzima. Na siku ukisafiri ni lazima ufungashe vyakula kwa sababu unaweza kukwama njiani wiki moja hadi mbili na wengine waliokuwa wakisafiri wakiwa wagonjwa, walikufa njiani,"alisema.

Hata hivyo, kutokana na jitihada kubwa za serikali, alisema usafiri katika mikoa hiyo umekuwa mzuri na mtu anaweza kunywa chai asubuhi akiwa Lindi na akala chakula cha mchana Dar es Salaam.

"Sasa kuna watu wanasema serikali haijafanya chochote kwa miaka 50, je hizi barabara, madaraja, na umeme vyote si chochote?" Alihoji mgombea huyo.

Aliwataka wananchi waache kuwasikiliza viongozi na wanasiasa waliotoka CCM na kukimbilia upinzani kwa vile hawana chochote cha maana cha kuwaambia.

Alisisitiza kuwa katika uongozi wake wa awamu ya tano, atahakikisha mafisadi hawatakuwa na nafasi na ndio sababu baadhi yao wameshaanza kumkimbia mapema.

Aliwaeleza wananchi kuwa hawapaswi kuwa na hofu kuhusu utendaji wake kwa vile uwezo na sifa zake zinajulikana na kila Mtanzania, hivyo alisisitiza kuwa kwake ni kazi tu.

Dk. Magufuli aliwaonya wananchi kwa kuwaambia wasifanye makosa katika kupiga kura. Alisema ni bora kukosea kuoa au kuolewa kwa sababu mtu anaweza kuo au kuolewa tena kuliko kukosea kupiga kura.

AVUNA WANACHA 133 WA UPINZANI

Dk. Magufuli alianza mikutano yake mkoani Lindi kwa kufanya mkutano mkubwa katika jimbo la Ruangwa, ambapo wanachama 133 kutoka CHADEMA, CUF na ACT Wazalendo walirejesha kadi zao na kujiunga na CCM.

Baadaye Dk. Magufuli alifanya mikutano Nachingwe na Mtama, ambako aliwataka wamchague kwa kura nyingi ili aweze kuwaletea maendeleo na kutahadharisha athari watakazopata iwapo watachagua upinzani.

Akiwa safarini kwenda Ruangwa kutoka Nachingwe, baadhi ya wafuasi wa CHADEMA walianza kutundika bendera za chama chao barabarani hadi kwenye uwanja alikofanyia mkutano.

Lengo la wafuasi hao wa CHADEMA lilikuwa kuanzisha vurugu kwa madai ya kushushiwa bendera na mabango ya mgombea wao wa ubunge katika jimbo la Ruangwa, Omar Makota.

Kwa kutumia busara, wanachama na wafuasi wa CCM waliamua kuweka bendera na mabango yao karibu na yale ya CHADEMA hadi kwenye uwanja wa  Likanja, ambako ndiko Dk. Magufuli alikofanyia mkutano wake.

Wakati akipita katika maeneo hayo na kwenye mkutano wake, Dk. Magufuli alisifia kuwepo kwa demokrasia ya vyama vingi na kusisitiza kuwa, iwapo atachaguliwa, atakuwa rais wa Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa.

No comments:

Post a Comment