Wednesday 1 June 2016

MAUAJI YA KUTISHA TANGA, WATU WANANE WACHINJWA


WATU wanaoaminika kuwa majambazi, wamevamia duka moja lililoko katika mtaa wa Kibatini, Kata ya Mleni, jijini Tanga na kuwateka watu wanane wa familia mbili, kisha kuwachinja na kuiba mchele na biskuti.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Kamishina Mwandamizi wa Polisi (SACP), Leonard Paul,  alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 7:00 usiku, wakati watu hao ambao idadi yao haikutajwa, walipovamia nyumba hizo.

Kamanda Paul alisema watu hao walianza kuvamia nyumbani kwa Issa Hussein (50), mjumbe wa serikali ya mtaa huo, aliyekuwa na duka lililokuwa na vitu hivyo na kisha kuwachukua watu wengine, Mkola Hussein (40) na Hamisi Issa, ambao wote walichinjwa.

Baada ya hapo, kamanda huyo alisema watu hao walikwenda kwenye nyumba nyingine, ambako walifanikia kuwachinja Mikidadi Hassan (70), Issa Ramadhani (25) na watu wengine waliotajwa kwa jina moja moja la Kadir, Salim na Mahamudu, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40.

“Kwa kweli ni tukio la kusikitisha sana, ambalo limetokea kilometa 45. Watu wanaoaminika kuwa na mapanga na visu walivamia nyumba mbili na kuwachinjwa watu wanane na kuiba mchele na biskuti,” alisema kamanda huyo.

Aliongeza kuwa jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola vinaendelea kuwafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha wanawatia mbaroni wauaji wote na alimewataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.

Matukio ya uhalifu katika Jiji la Tanga yanaendelea kutokea katika mitaa mbalimbali, ambapo hadi sasa raia na askari, ambao wamepoteza maisha wanafikia 13, katika kipindi cha miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment