Wednesday, 24 August 2016

MWANAFUNZI WA KITANZANIA AVUTIA WAWEKEZAJI UJERUMANI


KIJANA Petro Magoti kutoka Shirikisho la Vyuo
vya Elimu ya Juu-CCM, aliyeko Ujerumani kwa
masomo ya uongozi na uhusiano wa kimataifa,
akiagana na mmoja wa wamiliki wa viwanda
vikubwa duniani, Profesa Karl Knoop, baada ya
kuzungumza naye, mjini Berlin, Ujerumani, juzi.
Kushoto ni Meya  wa mji wa Bugermeister,
David Osthotlhoff.

MWAKILISHI pekee wa Tanzania, aliyeko Ujerumani kwenye mafunzo ya uongozi na uhusiano wa kimataifa, Petro Magoti,  amekutana na mmoja wa wamiliki wa viwanda vikubwa duniani, Profesa Karl Heinz Knoop na kufanya mazungumzo naye ili kumshawishi kuja kuwekeza nchini.

Akizungumza kutoka Ujerumani, Magoti alisema Profesa Knoop, ambaye anamiliki viwanda katika nchi 17 barani Ulaya na katika nchi nne za Afrika, katika mazungumzo yao, ameonyesha dhamira ya kuwekeza Tanzania katika maeneo ya Himo mkoani Kilimanjaro na Kilindi, Tanga.

Magoti alisema tajiri huyo amefikia dhamira hiyo baada ya kumweleza kwa kina fursa za kiuchumi zilizoko Tanzania na namna nchi ilivyojipanga kuwapokea kwa ukarimu wawekezaji kutoka nje, ikiwemo Ujerumani, lengo likiwa kuifikisha nchi kuwa ya viwanda, hivyo kuwezesha wananchi wengi, wakiwemo vijana kupata ajira za uhakika.

"Katika mazungumzo yetu, Profesa Knoop ameeleza kuwa ana dhamira ya kuwekeza Tanzania ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuondoa umasikini. Hata hivyo, alisema aliwahi kuonyesha azma hiyo, lakini alikumbana na changamoto lukuki," alisema Magoti.

Alisema katika mazungumzo yao, alimsihi na kumwomba bilionea huyo, kutokata tamaa katika dhamira yake hiyo ya kujenga viwanda Tanzania, kutokana na changamoto ya awali aliyokumbana nayo ya kupata eneo la uwekezaji, badala yake afike Tanzania ili kuonana na Rais Dk. John Magufuli, ambaye kwake viwanda ni kipaumbele.

"Nilimweleza kuwa Rais Dk. Magufuli anavutiwa na wawekezaji walio tayari kuijenga Tanzania ya viwanda ili kukuza uchumi na kupunguza tatizo la ajira, hasa kwa vijana, ambalo sasa ni kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali," alisema.

Aliongeza: "Nimemshauri tajiri huyo akifika nchini kwetu, aombe kujenga viwanda vyake katika mikoa ya Iringa na Morogoro, ambayo ina maeneo mengi na mazuri kwa kilimo."

"Baada ya mazungumzo yetu, tumekubaliana kati ya Oktoba 17 hadi 22, mwaka huu, bilionea huyo atafika Tanzania kwa ajili ya kuonana na rais ili kujadiliana naye juu ya uwekezaji huo wa viwanda na ameahidi kutembelea mikoa ya Iringa na Morogoro ili kujiridhisha na maeneo," alifafanua.

Katika kuhakikisha kuwa anaitumia vyema fursa ya kuwepo kwake Ujerumani, Magoti pia alitafuta nafasi na hatimaye akaipata ya kukutana na wabunge wastaafu na viongozi wa serikali ya Ujerumani, wakiongozwa na Profesa Hemker, anayetokana na Chama cha SPD.

Magoti, ambaye anatoka katika Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu-CCM, yupo Berlin, Ujerumani kwa wiki ya pili sasa, akiendelea na masomo ya uongozi na uhusiano wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment