Wednesday 1 June 2016

JPM: SIWACHUKII WENYE VIWANDA


RAIS Dk. John Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kuwa, serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kwao na wenye nia ya kuanzisha viwanda vipya ili kufanikisha nia ya kuzalisha ajira nyingi, kukuza uchumi na kuiwezesha serikali kukusanya mapato zaidi.

Alitoa kauli hiyo jana, katika hafla ya kutoa tuzo ya Rais kwa wazalishaji bora wa mwaka 2015, iliyofanyika Hoteli ya Serena, jijini Dar es salaam.

Rais Dk. Magufuli alisema serikali yake inatambua umuhimu wa viwanda katika uchumi na aliwataka wenye viwanda na wenye nia ya kuanzisha viwanda, kupuuza kauli zinazotolewa na baadhi ya watu wanaodai anawachukia.

"Wekezeni kwenye viwanda na mimi nawaambia mkishindwa katika kipindi hiki cha awamu ya tano, hamtaweza tena...mimi siwachukii wenye viwanda na wala siwachukii matajiri," alisema Rais Magufuli.

Alisisitiza kuwa serikali itafanyia kazi changamoto zilizotolewa na wenye viwanda, zikiwemo miundombinu duni ya usafirishaji, nishati, mikopo na kodi.

Rais Magufuli pia alitoa wito kwa benki zinazoendesha shughuli zake hapa nchini, kujenga mazingira bora kwa wanaohitaji mikopo kwa ajili ya kuanzisha viwanda, ikiwemo kupunguza riba.

Rais Magufuli alisema licha ya serikali kuimarisha Benki ya Uwekezaji (TIB), inakusudia kuanzisha benki ya viwanda ili kuharakisha uanzishaji wa viwanda.

Aliwahakikishia wenye viwanda kuwa serikali itavilinda viwanda vya ndani na kuwataka wafanyabiashara wengi zaidi wajielekeza kuanzisha viwanda, badala ya kuendelea kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, licha ya malighafi nyingi kuwepo hapa nchini.

Katika hafla hiyo, Rais Dk. Magufuli alitoa tuzo kwa washindi wa uzalishaji bora wa bidhaa za viwandani, ambapo Kampuni ya Bia (TBL) iliibuka kuwa  mshindi wa jumla.

No comments:

Post a Comment