Wednesday, 1 June 2016

WALIONYANYASA WATU WASAKWE-DK. SHEIN



RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amelitaka Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, kuhakikisha wote waliohusika na vitendo vya kunyanyasa wananchi na kuharibu mali, wanafikishwa mahakamani.

Dk. Shein alitoa agizo hilo jana, kwa nyakati tofauti, wakati alipotembelea maeneo mbalimbali kisiwani Pemba, ambako watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa chama kimoja cha upinzani, walifanya uharibifu mkubwa wa mali na kutishia uhai wa baadhi ya wananchi kwa kuwashambulia.

“Jeshi la polisi lazima litekeleze wajibu wake kwa umakini mkubwa na kwa haraka ili waliohusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na kesi hizo zitolewe uamuzi haraka ili haki itendeke,” alisema Dk. Shein.

Katika ziara hiyo, Dk. Shein alitembelea Tawi la CCM Tibirinzi, Wilaya ya Chake Chake, ambalo lilitiwa moto na kusababisha uharibifu uliokisiwa kufikia zaidi ya sh. milioni 9.5.

Pia alitembelea nyumba ya mwanakijiji wa Shengejuu, Shehia ya Pembeni, Wilaya ya Wete, Said Khamis, ambaye alivunjiwa nyumba yake, kuharibiwa na kuibiwa samani na mbao katika kiwanda chake hicho na kuharibiwa shamba lake la muhogo katika kijiji cha jirani cha Msimeni.

Pamoja na kufanya uhalifu huo, watu hao walimjeruhi kwa kumpiga mawe mama wa mwanakijiji huyo na kumsababishia maumivu na kulazimika kulazwa hospitali kwa siku kadhaa.

Katika Wilaya ya Micheweni, Dk. Sein alimtembelea Sheha wa Shehia ya Kiuyu Maziwa Ng’ombe, Asha Yussuf Hassan, ambaye mbali ya kukatiwa migomba yake na kuharibiwa kitalu cha migomba, alivunjiwa sehemu ya nyumba yake, kuchukuliwa matofali zaidi ya 400 na kutishiwa kuuawa na watu hao kwa kumshambulia yeye na familia yake kwa mawe na kujaribu kuchoma nyumba yake, wakiwa wamejifungia ndani.

“Matukio haya yangeweza kuleta dhahama kubwa nchini kama walioathirika na matukio haya wangeamua kuchukua hatua za kulipiza kisasi,"  Dk. Shein alitanabaisha na kusisitiza kuwa, Jeshi la Polisi halina budi kufanyakazi kwa uangalifu mkubwa ili kuepusha kuwatia makosani wananchi wasiohusika na vitendo hivyo.

Alivielezea vitendo hivyo kuwa ni kukosa ustaarabu na uungwana kwani hakuna sababu yoyote ya msingi ya kumshambulia mwananchi mwenzako na kumharibia mali zake.

“Nimehuzunishwa na vitendo hivi na sijaridhishwa na sababu za kumfanyia vitendo hivyo  kiongozi wa serikali,” alisema Dk. Shein na kusisitiza kuwa, vitendo alivyofanyiwa sheha wa shehia hiyo ni uharamia, ambao hauwezi kuvumiliwa, hivyo ni lazima hatua  za kisheria zichukuliwe kwa waliohusika navyo.

“Kitendo cha kumshambulia kiongozi wa serikali (sheha) au kumtishia, tafsiri yake ni kuishambulia au kuitisha serikali na serikali haitakubali vitisho hivyo,” alionya Dk. Shein.

Aliwaeleza wananchi waliokuwa wakimsikiliza kwa makini kuwa, vitendo vya kupingana na serikali bila ya sababu, haviwezi vikaachwa na kupita na kwamba, atafuatilia kwa karibu kufahamu mwisho wa matukio hayo.

Dk. Shein alitoa wito kwa wana CCM na wananchi kwa jumla kujiepusha kujichukulia sheria mikononi na kuwataka kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama mara vitendo kama hivyo vinapofanyika.


Aidha Dk. Shein aliwataka wananchi wa Kiuyu Maziwa Ng’ombe kuishi kwa kupendana na kushirikiana kwa kuwa wote ni watu wa nasaba moja na kuacha jazba za kisiasa katika maisha yao ya kila siku.

“Msiishi kwa kutishana, kugomeana na kudharauliana. Nyinyi ni watu wamoja,” aliasa Dk. Shein na kuviagiza vyombo husika kuwafutia leseni wafanyabiashara wote wanaofanya vitendo vya kibaguzi katika biashara zao.


Akitoa maelezo kwa Rais, Sheha wa Shehia ya Maziwa Ng’ombe, Asha alisema siku ya tukio watu hao walivamia eneo la nyumba yake na kuanza kukata ndizi na migomba, kuvunja sehemu za nyumba yake na kuchukua matofali yote yaliyokuwepo na kujaribu kuichoa moto nyumba yake hali akiwa ndani na familia yake.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, alisema  hadi sasa watuhumiwa 18, wamekatwa kwa tukio lililotokea Shehia ya Maziwa Ng'ombe, watu saba huko Mtambwe na watu tisa katika Shehia ya Pembeni.

Dk. Shein alimaliza ziara yake ya siku tatu kisiwani Pemba jana, leo mchana kwa kuzungumza na Kamati za Siasa za CCM wilaya na mikoa kisiwani hapa.

No comments:

Post a Comment