MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji
(EWURA), imesema bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini zimeshuka
katika mwezi huu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka uliopita.
Imesema bei hizo mpya za jumla na rejareja kwa mafuta
ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, zitaanza kutumika rasmi kesho, maeneo yote
ya nchi kwa viwango vya sh. 79
kwa lita, sawa na asilimia 4.01, sh. 76 kwa lita, sawa na asilimia 4.20 na sh.
66 kwa lita, sawa na asilimia 3.73.
Vilevile
kwa kulinganisha na bei za Desemba, mwaka jana, EWURA imesema bei za jumla kwa
mafuta ya petroli, dizeli na ya taa nazo zimepungua kwa sh. 79.19 kwa lita,
sawa na asilimia 4.23, sh. 76.49 kwa lita, sawa na asilimia 4.45 na sh. 65.86
kwa lita, sawa na asilimia 3.97.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi,
ilisema kupungua huko kwa bei
za mafuta, kwa kiasi kikubwa kumetokana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia na pia
kushuka kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa za mafuta kuja nchini.
Taarifa
hiyo ilisema kulingana na Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za
mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, hivyo EWURA itaendelea
kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta kwa
lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa
hizo.
Kupitia
taarifa hiyo, Ngamlamgosi alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za
mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei
kikomo kama ilivyokokotolewa na mfumo uliopitishwa na EWURA na ambayo ilichapwa
kwenye Gazeti la Serikali Na. 405/2015 la Julai, 2015.
Aidha,
taarifa hiyo imevielekeza vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za mafuta
katika mabango, ambayo yataonyesha bei, vivutio vya biashara au promosheni
zinazotolewa na kituo husika na kwamba pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja
wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa
bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani.
Taarifa
hiyo ilitahadharisha kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei
inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika.
Pamoja na
hayo, wateja wameshauriwa kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha
jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
Stakabadhi
hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo
kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo
ama endapo utakuwa umeuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
No comments:
Post a Comment