Tuesday, 5 January 2016

MAHAKAMA KUU YASITISHA BOMOABOMOA KINONDONI



NA WAANDISHI WETU
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi, imetoa zuio la muda kwa serikali kusitisha bomoa bomoa kwa wakazi 681 wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, waliowasilisha maombi mahakamani hapo.
Aidha, imewaagiza mawakili wa wakazi hao kuwasilisha jana mahakamani hapo, majina ya wateja wao na anuani, hususan za makazi ili zuio la kutovunjwa nyumba zao litekelezwe kwa urahisi.
Pia, mahakama hiyo imesema serikali kwa kupitia Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), haizuiwi kutambua, kuweka alama na ikibidi kuvunja nyumba za wale ambao hawahusiki katika maombi hayo.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Panterine Kente, baada ya kusikiliza maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo juzi na wakazi saba wa manispaa hiyo na wenzao 674, kupitia mawakili wao.
Wakazi hao Ally Mishindo, Agnes  Machalila, Sanura Abeid, Sultan Ally,  Mussa Digumbi, Godwin Cathbert, Irene Duma na wenzao  674, waliwasilisha maombi namba 822 ya mwaka jana, wakiomba kupewa kibali cha kufungua kesi dhidi ya  Manispaa ya Kinondoni, NEMC na AG.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Kente alisema wakati wa kusikilizwa kwa maombi hayo, wakazi hao saba waliomba mahakama itoe amri ya kuizuia serikali kuvunja au kubomoa nyumba zao na wenzao 674, hadi hapo shauri lao litakaposikilizwa.
Jaji huyo alisema pia wakazi hao walikuwa wakiomba kupewa kibali cha kufungua shauri hilo.
Alisema hata hivyo, maombi hayo yalipingwa na upande wa serikali, wakidai kwamba mahakama haiwezi kutoa mari hiyo kwa sababu hakuna kesi iliyofunguliwa.
Jaji Kente alisema serikali ilidai mahakama ikitoa amri hiyo, itakuwa imetoa kwa watu ambao hawawafahamu.
“Katika kesi za uwakilishi kama  hizi, inafunguliwa pale tu mtu anapowasilisha maombi ya kuomba apewe kibali cha kufungua kesi, kwani amekuwa anaonyesha nia.
“Hivyo sio sahihi kusema bado kesi haijafunguliwa, hatua za awali tayari tunayo maombi  namba 822 ya mwaka 2015, bado mahakama ina mamlaka ya kuona kama inafaa kuingilia na kutoa amri,” alisema.
Alisema kwa mazingira ya shauri hilo, mahakama inaweza kutoa zuio la muda kwa kupitia wajibu maombi (NEMC, Manispaa ya Kinondoni na AG).
“Suala hili limekuwa gumu kwangu, lakini mwisho wa yote niseme naamini na sina shaka, hatua zinazochukuliwa na serikali kupitia wajibu maombi, zina lengo jema kwa wananchi kuhakikisha wamekaa sehemu salama kwa ajili ya maisha yao,” alisema.
Jaji huyo aliongeza: “Hatua zote zinazochukuliwa na serikali zinaongozwa na sheria na utawala bora. Pamoja na yote hayo, jambo la wazi ni kwamba wote tunakubaliana hakuna yoyote anayeitwa serikali, bali linalofanywa linafanywa na maofisa wake, ambao wanaweza kukosea na ukizingatia aina ya zoezi lilivyo, hasara inayojitokeza inaweza kuwa kubwa kwa mhusika.”
Alisema mahakama kuingilia kati suala hilo inaonekana ni muhimu na kwamba hana ushahidi, ambao ungemwezesha kutoa zuio hilo na kuamua mambo yabaki kama yalivyo na hana ushahidi wa pande mbili, nyumba ngapi zimevunjwa na nani kavunjiwa.
Jaji Kente alisema upande wa waombaji hawakuleta mahakamani hapo majina ya watu 674, bali imeletwa idadi na anuani, hali ambayo inaiweka mahakama katika ukingo wa amri, ambayo inaweza kugusa watu wasiojulikana au dunia nzima.
“Kosa la kutokuwepo kwa orodha hiyo haliondoa uzito wa shauri hili. Nimeridhika shauri la msingi bado haliko, lakini bado kuna watu wanastahili kusikilizwa kupitia waombaji wachache,” alisema.
Baada ya kueleza hayo, Jaji Kente alitoa zuio  hilo kwa serikali na maelekezo kwa mawakili wa waombaji hao na serikali.
Jaji huyo alisema maombi hayo yatatajwa Jumatatu wiki ijayo, ili kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.

IDADI YA NYUMBA YAONGEZEKA
SERIKALI imeongeza idadi ya nyumba zinazotakiwa kubomolewa na kufikia 15,000, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 90, ikilinganishwa na awali.
Aidha, jana serikali iliendelea na bomoabomoa katika maeneo yaliyojengwa kinyume cha sheria kama ilivyoahidi, baada ya kusitisha shughuli hiyo kwa takribani wiki mbili.
Ofisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.  Charles Mkalawa, alisema hayo jana, jijini Dar es Salaam.
"Nyumba zilizotarajiwa kubomolewa awali zilikuwa 8,000, idadi iliyozigatia sensa iliyofanyika miaka mitatu iliyopita," alisema.
Alisema kulingana na tathmini mpya  iliyofanywa na wizara hiyo, mbali na zile zilizosahaulika, idadi  hiyo pia imeongezeka baada ya baadhi ya watu kujenga nyumba  zingine mpya katika maeneo hayo.
Changamoto zilijitokeza wakati wa shughuli hiyo ya ubomoaji ni pamoja na wakazi wa maeneo  hayo  kuendelea kuwepo katika nyumba zao na wengine kukutwa wakiendelea kufunga mizigo yao.
"Hii imekuwa changamoto kubwa kwa kuwa imesababisha zoezi letu  kutokamilika kwa wakati huku kukiwa na malalamiko mengi," alisema.
Uhuru ilihoji baadhi ya wkazi hao, ambao walisema kwamba, walidhani jana ilikuwa siku ya mwisho ya kukaa katika maeneo hayo na sio siku ya kuendelea rasmi na bomoa bomoa  hiyo.
"Isitoshe tulipata habari ya kusubiri hukumu ya mahakama dhidi ya suala hili," walisema wakazi hao.

SADIKI: HATUTAWAPA VIWANJA WALIOBOMOLEWA
SERIKALI imesema haitawapa viwanja wananchi wanaobomolewa nyumba zao, ambao walijenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.
Aidha, imesema ubomoaji wa nyumba kwenye maeneo hayo unafanywa kwa mujibu wa sheria ya mazingira na kwamba, unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya  Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadick, amewataka wananchi wasikubali kupotoshwa na wanasiasa kuhusu mchakato wa kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo yasiyoruhusiwa na hakuna atakayepewa viwanja.
Amewataka wananchi wasilifananishe zoezi linaloendelea sasa na la mwaka 2011, ambapo walioathiriwa na mchakato huo walihamishiwa na kupewa viwanja maeneo ya Mabwepande.
Sadick alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mwaka huo, waathirika 1,010, walipatiwa viwanja kutokana na agizo la Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Alisema viwanja hivyo viligawiwa kwa kaya 1,007, pekee ambapo kaya tatu zilikosa kutokana na makazi yaliyosalia kuwa katika mazingira hatarishi na kwamba orodha ya majina ya watu wote waliohusika katika zoezi hilo ipo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema wananchi waliokwenda kufungua kesi mahakamani ni haki yao ya kikatiba, ila aliwashauri wasiendelee kucheleweshwa na wanasiasa katika kujiletea maendeleo.
Aliwataka kuendelea kuhamisha mali zao na kwamba kama walivyoingia wenyewe ni vizuri wakaondoka wenyewe na kwamba watu hao wanaweza kuishi kwenye mikao mingine na sio Dar es Salaam pekee.
Alisema serikali ina huruma, lakini ina kiwango cha kufanya mambo yake na kwamba si rahisi kuwatafutia makazi zaidi ya watu 8,000.
Aliwaonya wananchi kuacha kuvamia maeneo ya watu, ambayo yamepimwa na aliyataja maeneo hayo kuwa ni Tegeta Goba, Kulangwa, Mabwepande, King’azi pamoja na shamba la aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Ritha Mlaki.
IMEANDIKWA NA FURAHA OMARY, RACHEL KYARA NA WINFRIDA EMMANUEL

No comments:

Post a Comment