Wednesday 9 September 2015

LOWASSA AMEFILISIKA KISIASA-SHAKA




Na Mwandishi Wetu, Njombe

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka amesema mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, ameonyesha udhaifu na kufilisika kisiasa kwa kuthububutu  kutumia nyumba za ibada ili achaguliwe kuwa Rais wa Tanzania.

Amesema hatua hiyo ya Lowassa inatokana na kushindwa kujenga nguvu ya hoja na matumizi ya sera zenye ushawishi zitakazowavutia Watanzania.

Shaka aliyasema hayo jana mjini Makambako, wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea urais wa  CCM, Dk. John Magufuli, wabunge na madiwani mkoani hapa.

Alisema hakutegemea kama siku moja Lowassa angesimama mbele ya Watanzania na kuwashawishi waumini ama wa kanisa au msikiti, kutaka achaguliwe kushika nafasi nyeti ya urais.
 
"Mzee wangu Lowassa amejifedhehesha na kuishangaza dunia ya leo, moyo na fikra zake anaonyesha ana ajenda hatari," alisema Shaka huku akishangiliwa na wananchi.

Alisema ukimuona mwanasiasa anatumia ukabila, udini au kujinasibu kwa uzawa na ukanda, huko ni zaidi ya kufilisika na kiongozi wa aina hiyo anapaswa kuogopwa kama maradhi ya ebola na ukimwi.
 
Shaka alisema kitendo cha Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, kusema tangu kuasisiwa taifa la Tanzania, hajapatikana Rais wa dhehebu la Kiluteri, ni jambo linalopaswa kulaaniwa na kupingwa kwa nguvu zote na Watanzania bila kujali tofauti za kisiasa.

"Dhamira ya Lowassa si njema, anataka kuiingiza Tanzania kwenye mitafaruku ya kiimani na kikatiba na kuwagawa wananchi. Ameiba sera zinazotumika Somalia, Eritrea na Afrika ya Kati," alisema.

Aidha, Shaka alisema tangu Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar, wananchi wameendelea kuwa wamoja na wenye upendo bila kuendekeza ukabila, udini wala nasaba, hivyo anachokihitaji Lowassa na CHADEMA ni kusababisha machafuko.

Akihutubia katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa, Seki Kasuga, aliwaomba wananchi kuipuuza CHADEMA kwa kuwa chama hicho na mgombea wake wa uarais wamepoteza dira.

Seki alisema vyama vingi vya upinzani kikiwemo CHADEMA na CUF kwa miaka mingi vimeonyesha ishara ya kupigania dini, ukanda na ukabila, hivyo havistahili kuungwa mkono na Watanzania waliolelewa kwa upendo, umoja na mshikamano.
 
"Tuliwahi kusema tangu mwaka 1992 kwamba CUF na CHADEMA sera zao zinahitaji kuangaliwa kwa umakini na tahadhari, Watanzania kuweni macho na chokochoko za udini anazotamani Lowassa na kundi la UKAWA," alisisitiza Seki.

Naye Mwenyekiti wa Mkoa wa Njombe, Deo Sanga (Jah People), alisema  anachokifanya Lowassa na UKAWA ni kutaka kuliingiza taifa katika janga la udini , hivyo ili kulikataa, wapigakura wawanyime kura wagombea wote wa CHADEMA na UKAWA.

Alisema matamshi aliyoyatoa Lowassa akiwa kanisani huko Tabora, yangepingwa vikali kama marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere angekuwa hai na huenda asingetamani kukutana naye kutokana na kauli hiyo.

"Mwalimu Nyerere katika maisha yake alipinga ukabila, udini na matabaka, alipigania uhuru na ukombozi Kusini mwa Afrika, hakubagua mtu kwa rangi, dini pia alilaani ukandamizaji wa haki mahali popote duniani," alisema.

No comments:

Post a Comment