Wednesday 9 September 2015

ASUMPTA AWATAKA WANANCHI WAIAMINI CCM




NA ABDALLAH MWERI, MBINGA
MBUNGE wa zamani wa jimbo la Nkenge (CCM), Asumpta Mshama, amewataka wananchi kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa hakina ubaguzi.

Asumpta alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika juzi, Maguu, Mbinga Mjini mkoani Ruvuma.

Alisema Watanzania watajuta endapo wataipigia kura CHADEMA katika uchaguzi huo kwa sababu chama hicho kinaundwa kwa misingi ya dini na ukabila.

Asumpta alisema kauli ya mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Edward Lowassa, aliyotoa mkoani Tabora wiki hii, kuwa ni zamu ya Walutheri kuongoza nchi, inapaswa kupuuzwa kwa sababu inawabagua Watanzania katika misingi ya dini.

"Ndugu zangu mimi nilikuwa mbunge si mnanijua, lakini safari hii wapiga kura wangu walimtaka mtu mwingine, mmeona nikilalamika na kwenye kampeni si nipo, hii ndio demokrasia ya CCM.

"Lakini ndugu zangu wapo watu wameshindwa katika kura za maoni wameamua kuhama CCM eti wameonewa, hakuna ukweli, hawa wameondoka kwa sababu ya uroho wa madaraka, kuweni makini na watu hao," alisema Asumpta.

Alisema CHADEMA ni chama cha wababaishaji wasiokuwa na ilani ikilinganishwa na CCM, ambayo imekuwa ikitekeleza ilani yake kikamilifu tangu ilipoingia madarakani.

Asumpta alisema CHADEMA ni SACCOS inayowanufaisha watu wachache kutoka kanda ya kaskazini na chama hicho kimeundwa kwa misingi ya ukabila.

Alisema CHADEMA ni kikundi cha watu wachache kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, ambacho kimekuwa kikinufaika kwa kuwahadaa Watanzania kuwa wakiingia madarakani wataleta maendeleo.

"Jamani kuweni makini sana na UKAWA, hawa jamaa ni wababaishaji, wamechaguana kuongoza CHADEMA kwa misingi ya ukabila, sera zao ni kumtoa Babu Seya gerezani, hivi kweli watu wa aina hii wanaweza kupewa nchi kuongoza?" Alihoji.

Mbunge huyo wa zamani, aliwataka wananchi kupuuza kauli hizo kwa sababu Babu Seya alifungwa kwa kosa la kuwanajisi wanafunzi na sheria ilichukua mkondo wake katika kutoa adhabu ya kifungo cha maisha.

"Huyu mtu aliwafanyia vitendo vibaya watoto wetu, leo UKAWA wanapanda jukwaani wakidai wakiingia madarakani watamtoa, hivi inaingia akilini kweli, UKAWA hanana sera wala ilani, muwapuuze," alisema Asumpta.

Alisema wanachama wa CCM waliojiunga na UKAWA walikuwa na ajenda ya siri ya kutaka madaraka na hawana lengo la kuwatumikia wananchi katika kuwaletea maendeleo.

Asumpta aliwataka wakazi wa Mbinga Mjini kumpigia kura ya ndio mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kwa kuwa ana rekodi nzuri ya utendaji kazi. Uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment