Wednesday 2 November 2016

MPANGO WA MAENDELEO WAWASILISHWA BUNGENI


SERIKALI imewasilisha Bungeni mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/18, ambao pamoja na mambo mengine, utazingatia mradi wa magadi soda na kufufua kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre.

Mpango huo ia umeelekeza mipango ya ujenzi wa majengo na miundombinu ya serikali, iliyopangwa kujengwa Dar es Salaam, ihamishiwe Dodoma kunakohamishiwa shughuli za makao makuu ya serikali.

Akiwasilisha mpango huo bungeni mjini hapa jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema katika viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, serikali itazingatia miradi mbalimbali, ikiwemo miradi ya magadi soda (Bonde la Engaruka), kufufua kiwanda cha General Tyre na uendelezaji wa eneo la viwanda (TAMICO).

Miradi mingine ni uendelezaji wa maeneo ya viwanda vidogo (SIDO), katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mbeya, Mwanza, Arusha, Bandari Kavu (Pwani) na mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga.

Alisema sh. trilioni 32.946 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi cha mwaka huo wa fedha.

SERIKALI KUHAMIA DODOMA

Kuhusu serikali kuhamishia shughuli za makao makuu Dodoma, Dk. Mango alisema maofisa masuuli wameelekezwa kujumuisha mahitaji ya kuhamia mkoani humo katika mipango na bajeti kwa kuzingatia ratiba iliyotolewa.

Alifafanua kuwa mipango ya ujenzi wa majengo na miundombinu ya serikali iliyopangwa kujengwa Dar es Salaam, itahamishiwa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya  kuhamishia shughuli za makao makuu ya serikali mjini humo.

“Ujenzi wa majengo na miundombinu yote inayotegemewa kujengwa Dodoma ni lazima upate idhini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,”alisema.

Alieleza kuwa uchambuzi wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara, idara zinazojitegemea, taasisi na wakala za serikali, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, utafanywa kwa pamoja baina ya Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Msajili wa Hazina na wadau wengine.

“Taasisi zote za serikali zinaagizwa kuandaa na kuwasilisha mipango na bajeti zao wizara ya fedha na mipango kwa ajili ya uchambuzi kwa mujibu wa kifungu 22 (1) cha sheria ya bajeti Na. 11 ya mwaka 2015,”alisema.

Akizungumzia kiasi cha fedha kinachotarajiwa kukusanywa na kutumika katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, alisema kwa kuzingatia sera za uchumi  pamoja na misingi na sera za bajeti kwa mwaka huo 2017/18, sura ya bajeti inaonyesha sh. trilioni 32.946, zinatarajiwa kukusanywa na kutumika.

Dk. Mpango alisema kiasi hicho ni makisio ya awali, ambapo makisio ya mwisho yatapatikana baada ya kukamilika kwa tathmini ya nusu mwaka 2016/17, pamoja na taarifa ya kikosi kazi cha maboresho ya kodi kinachojumuisha wadau mbalimbali, wakiwemo sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Alisema mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa sh. trilioni 20.872, sawa na asilimia 63 ya mahitaji yote, ambapo kati ya hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya sh. trilioni 18.097, sawa na asilimia 87 ya mapato ya ndani.

Waziri alisema mapato yasiyo ya kodi ni sh. trilioni 2.022 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni sh. bilioni 753.3.

Alisema serikali inategemea kukopa Dola za Marekani milioni 900, (sawa na sh. trilioni 2.080), kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara na sh. trilioni 4.434, ni mikopo ya ndani kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva.

“Shilingi trilioni 1.859, sawa na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa, ni mikopo mipya ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Vile vile washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 3.700,”alisema.

Kati ya fedha hizo, alisema sh. bilioni 496.3, ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti (GBS), sh. trilioni 2.821, ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo na sh. bilioni 382.4, ni misaada na mikopo nafuu ya mifuko ya pamoja ya kisekta 43.

Kwa upande wa matumizi, katika mwaka 2017/18, alisema sh. trillion 32.946, zinazopangwa kutumika katika mwaka huo wa fedha zitatumika katika matumizi ya kawaida na maendeleo, ambapo kati ya fedha hizo, sh. trilioni 19.782, zitatengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

“Shilingi trilioni 7.206 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi za umma na sh. trilioni 9.723, kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa lililoiva.

“Matumizi ya maendeleo yatakuwa sh. trilioni 13.164, sawa na asilimia 40 ya bajeti yote, ambapo fedha za ndani ni sh. trilioni 9.960, sawa na asilimia 76, kiwango hiki ni sawa na ongezeko la sh. trilioni 1.343, ikilinganishwa na mwaka 2016/17,”alisema.

UTEKELEZAJI MPANGO NA BAJETI NA MIKAKATI

Alizitaja changamoto zilizojitokeza kuwa ni pamoja na uwezo wa kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi kwenye mipaka ya nchi, kuendelea kukua kwa sekta isiyo rasmi na ugumu wa kukusanya kodi na upatikanaji kwa wakati kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje.

Changamoto nyingine alisema ni kuongezeka kwa madeni ya ndani, kubadilika kwa masharti na sera za upatikanaji misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo na ushirika mdogo wa sekta binafsi, kutokana na mazingira yasiyo wezeshi kwa uwekezaji na uendeshaji biashara.

MABORESHO

Akizungumzia maboresho, alisema serikali imefanya maboresho mbalimbali katika mfumo wa kibajeti ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na uwazi.

“Maboresho makubwa yaliyofanyika ni pamoja na kuandaliwa na kupitishwa kwa Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na Kanuni za Bajeti za mwaka 2015.

“Hivyo, maofisa masuuli wote wanatakiwa kuendelea kuzingatia sheria ya bajeti pamoja na kanuni yake wakati wa uandaaji na utekelezaji wa mipango na bajeti. 46.

“Serikali imedhamiria kuandaa bajeti kwa kuzingatia programu (Programme Based Budget - PBB) ili kuwezesha utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia vipaumbele na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa umma,”alisema.

Aidha, alisema viwango vya ukomo wa bajeti kwa ajili ya maandalizi ya bajeti ya wizara, idara zinazojitegemea, taasisi na wakala za serikali, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, vitatolewa kwa kuzingatia vigezo vya ugawaji rasilimali na vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18 na Mwongozo huu.

“Hakutakuwa na nyongeza ya ukomo wa bajeti nje ya viwango vitakavyotolewa. Kwa msingi huo, maofisa masuuli wanatakiwa kuzingatia ukomo wa viwango vya bajeti vilivyoidhinishwa kwa mwaka 2017/18,”alisema.

No comments:

Post a Comment