Wednesday 2 November 2016

JPM AZINDUABARABARA YA SOUTHERN BY-PASS






NA MWANDISHI MAALUMU, NAIROBI

RAIS Dk. John Magufuli amempongeza Rais Uhuru Kenyatta na serikali yake kwa kujenga barabara ya Southern By-pass, iliyojengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi, nchini Kenya.

Amesema barabara hiyo haitawasaidia wananchi wa Kenya pekee bali na wana-Afrika Mashariki wanaotumia barabara zinazopitia Nairobi.

Sherehe ya uzinduzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 28 na inayounganisha maeneo mbalimbali ya Nairobi, ilifanyika katika eneo la Karen, nje kidogo ya jiji la Nairobi.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Magufuli pia aliishukuru serikali ya China, kupitia benki yake ya Exim, iliyotoa mkopo wa kujenga barabara hiyo, kwa kuendelea kuziamini nchi za Afrika Mashariki na kuzikopesha mikopo inayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.

"Wananchi wanahitaji maendeleo na haya ndio maendeleo, barabara hii itasaidia kuinua uchumi na itasaidia masuala ya kijamii,"alisema Rais Magufuli.

Dk. Magufuli alisema viongozi wa Afrika Mashariki wameamua kufanya kazi ya kuharakisha maendeleo na kuinua maisha ya wananchi na kwamba, ili kufanikisha hilo, wamedhamiria kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa barabara zinazounganisha nchi wanachama na kujenga vituo vya pamoja vya utoaji wa huduma za mpakani (One Stop Border Post).

Kwa upande wake, Rais Kenyatta alisema kujengwa kwa barabara hiyo kumesaidia kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Nairobi na kuboresha shughuli za maendeleo ya wananchi.

Kenyatta alimshukuru Rais Magufuli kwa kuungana naye kuzindua barabara hiyo na kusema, Kenya itaongeza juhudi katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara zinazounganisha Kenya na Tanzania, ikiwemo barabara ya Malindi kupitia Saadani hadi Bagamoyo na barabara ya Voi - Taveta- Holili-Arusha.

Sherehe za uzinduzi wa barabara ya Southern By-pass pia zilihudhuriwa na Naibu Rais wa Kenya, William Ruto.

Kabla ya kuzindua barabara hiyo, Rais Magufuli alitembelea kiwanda kidogo cha kusindika maziwa cha Eldoville, kilichoko katika eneo la Karen, ambacho kinamilikiwa na familia ya mkulima James Karuga.

Familia hiyo ilianzisha kiwanda cha kusindika maziwa mwaka 1985, kwa uzalishaji wa chini ya lita 1,000, kwa siku na hivi sasa imefikia uzalishaji wa lita 5,000, kwa siku na inatarajia kuongeza uzalishaji hadi lita 70,000 katika mwaka mmoja ujao baada ya kuongeza kiwanda cha pili.

Rais Magufuli aliondoka nchini juzi, kwenda Kenya, ikiwa ni ziara yake ya tatu nje ya nchi, tangu alipoapishwa kuwa Rais, Novemba 5, mwaka jana. Awali alitembelea nchi za Rwanda na Uganda.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake, Rais Magufuli aliipongeza Kenya kwa kuwa nchi inayoongoza kwa uwekezaji hapa nchini, ikilinganishwa na nchi zingine za Afrika.

Rais Magufuli alisema takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), zinaonyesha kuwa, Kenya inazo kampuni 529, zinazoendesha shughuli zake nchini, zikiwa zimewekeza Dola za Marekani bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56, 26.

Wakati huo huo, Rais Magufuli alitarajiwa kurejea nchini jana jioni, akitokea Kenya, ambako alikuwa na ziara ya siku mbili ya kiserikali,

No comments:

Post a Comment