Tuesday 1 November 2016

WACHINA WALIOMTEKA MWENZAO KIZIMBANI


RAIA watatu wa China, wanaotuhumiwa kumteka Mchina mwenzao, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kujibu mashitaka ya kumteka na kumjeruhi kwa kumpiga.

Washitakiwa hao ni Chen Bao (34), dereva Wang Jian (37) na mfanyabiashara Zheng Pa Jian au Mr. Ping, ambao walifikishwa mahakamani hapo jana.

Baada ya kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Hellen Moshi, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, washitakiwa Bao na Jian walikiri kutenda makosa hayo.

Awali, akiwasomea mashitaka, Hellen alidai Oktoba 21, mwaka huu, katika maeneo ya Palm Beach, wilayani Ilala, Dar es Salaam, washitakiwa walimteka Liu Hong kwa nia ya kumweka kwenye hali ya hatari kwa mauaji.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, mkalimani alikuwa akiwatafsiria kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kichina, ambapo Bao alikiri kutenda kosa hilo huku wenzake wakikana.

Pia, washitakiwa hao wanadaiwa siku hiyo katika eneo hilo,   walimpiga Liu sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha mwilini. Bao na Jian walikubali kutenda kosa hilo huku Mr. Ping akikataa.

Wakili Hellen alidai upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa na kwamba, wamewasilisha hati ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Ilala, Salum Ndalama, ambayo muapaji ni ofisa huyo kupinga dhamana kwa washitakiwa.

Hellen alidai wamefaili hati hiyo ikiwa na sababu, zikiwemo za washitakiwa kuwa ni raia wa China, hawana kazi na anuani maalumu Dar es Salaam na kuna taarifa za kuaminika kupitia upelelezi wa kesi hiyo kwamba, washitakiwa na watuhumiwa wengine, ambao hawajakamatwa, bado wanapanga kujihusisha na vitendo vya kuteka watu katika jiji hilo.

Sababu nyingine ni kwamba kuna taarifa za kuaminika zilizokusanywa kutokana na upelelezi kuwa, washitakiwa na wenzao wana mpango wa kumdhuru Liu kwa lengo la kupoteza ushahidi wa kesi hiyo iliyoko mahakamani.

Pia, upelelezi unaendelea na kama wakipatiwa dhamana, wanaweza kuharibu upelelezi na kuna taarifa kwamba, Wachina wengine ambao ni ndugu wa Liu, wanapanga kulipiza kisasi dhidi ya vitendo vya washitakiwa kwa kusababisha madhara ya mwili.

Nyingine ni maslahi ya jamhuri kwamba, washitakiwa wabaki ndani hadi kesi itakapokwisha ili kulinda usalama wa Liu na wa kwao wenyewe na kurahisisha upelelezi.

Baada ya upande wa jamhuri kuwasilisha hoja hiyo, Hakimu Mkeha alisema washitakiwa wanatakiwa kuwasilisha hati kinzani ya majibu ili aweze kupatia usikilizwaji wa pingamizi hilo la dhamana.

Kwa upande wa washitakiwa, walidai wanahitaji wakili, hivyo hakimu aliahirisha kesi hadi Novemba 14, mwaka huu na washitakiwa walirudishwa rumande.

No comments:

Post a Comment