Tuesday 25 July 2017

JPM: TUMEWAMINYA VIGOGO


RAIS Dk. John Magufuli amesema uongozi wake umeamua kuwaminya vigogo waliokuwa wakijipatia fedha kwa njia ya rushwa na ujanja ujanja ili kutoa nafuu kwa wanyonge.

Wakati Rais Magufuli akisema hayo, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, amelipuka na kumuomba Rais Magufuli kuwashughulikia bila huruma wale wote wanaoiba rasilimali za Tanzania.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, baada ya kufungua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.

Alisema kwa muda mrefu kulikuwa na baadhi ya viongozi waliojigeuza miungu watu na kutumia fedha za umma kwa kufanya anasa huku wananchi wanyonge wakiendelea kuteseka.

"Kuna baadhi ya viongozi hapa nchini walikuwa wanalipwa mshahara hadi sh. milioni 40, wakichaguliwa wanaunda bodi kwa ajili ya kuwatengenezea mishahara na wao wanawapa wajumbe wa bodi safari ya kwenda nje kama asante," alisema.

Rais Magufuli alisema kutokana na tabia hiyo, serikali yake iliamua kusimamisha safari zote za nje hadi kwa kibali chake ili kuokoa fedha za Watanzania wanyonge.

Mbali na hilo, aliwaagiza viongozi wa ngazi mbalimbali kuhakikisha wanatatua kero za wananchi na iwapo watashindwa kufanya hivyo, atalala nao mbele.

Vilevile, Rais Magufuli alisema ataendelea kuwateua na kuwapa uongozi wale wote wenye akili kutoka kwenye vyama vya upinzani ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

"Kuna watu wana akili kwenye vyama vya upinzani, mimi nasema nitaendelea kuwapa uongozi, lakini wale vilaza watandelea kubaki huko huko," alisema.

Kuhusu wizi unaofanywa na baadhi ya wawekezaji, alisema serikali yake haitarudi nyuma na ataendelea kuwabana wale wote wanaoiibia Tanzania.

Pia, aliwaomba wabunge wa Tabora kukaa kwa pamoja na kutafuta wawekezaji, ambao watakwenda kujenga kiwanda mkoani humo.

"Wabunge wa Tabora mna uwezo mkubwa, naomba mnisaidie kwenye hili zao la tumbaku. Tushikamane pamoja na serikali yangu tulete kiwanda hapa, tusitupiane mpira.

"Mmenisikia wabunge wa Tabora, tafuteni wawekezaji waleteni kwangu na mimi nitawapa sapoti, wakihitaji umeme tutawapa," alisema.

Kwa upande wake, Bashe alisema: "Rais, nimekusikia ulipokuwa Nakanazi ukisema kuwa umeanzisha mapambanao ya uchumi na mapambano hayo yana gharama.

"Bungeni kulipelekwa sheria ya mabadiliko ya masuala ya rasilimali za nchi.Rais usisikilize kelele, watu wasiotoka maeneo yenye migodi hawajui dhuluma walizopata wananchi ambao wanaishi kwenye maeneo yenye dhahabu."

Bashe alisema Nzega kulikuwa na Kampuni inaitwa Resolute, hadi inaondoka, inadaiwa sh. bilioni 10 na wameleta madai yao ya kodi za VAT na mafuta, wakiitaka serikali iwarudishie fedha hizo.

"Nakuomba Rais, mwambie Kamishna Mkuu wa TRA, Waziri wa Fedha wasiwalipe mpaka watoe shilingi bilioni 10 za Halmashauri ya Nzega, miaka mitano ya aliyekuwa Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla, amepigwa mabomu kudai fedha hizo," alisema.

Pia, alimhakikishia Rais Magufuli kuwa, katika vita hiyo ya rasilimali, hayupo peke yake bali wapo pamoja naye.

"Wametuachia mahandaki Nzega na mimi nawaambia, wanasema Rais Magufuli mkali, nimejiuliza hivi huyu mzee ni mkali kweli?" Alihoji.

Alisema wawekezaji hao wanatakiwa kufungiwa migodi kwa sababu hakuna njia nyingine ya kujadiliana na mwizi wa rasilimali za Watanzania.

"Rais, tumekupitishia sheria, unaporejea Dar es Salaam, nikuombe, utakapomteua mtendaji mkuu, naomba umpe jukumu moja la kuanzisha masoko ya dhahabu katika maeneo ambayo kuna wachimbaji wadogo. Wachimbaji wetu wadogo wana uwezo wa kuendesha uzalishaji wa dhahabu na mchango wake ni mkubwa katika jamii," alisema.

Vilevile, Bashe alimpa taarifa Rais Magufuli kuwa, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Acacia, alizungumza Julai 21, mwaka huu, akisema kuwa mwanahisa wa kampuni hiyo hatapewa gawiwo mpaka mchanga uliozuiwa masuala yake yatakapoisha.

"Najiuliza walisema yale ni makapi, michanga tu haina maana, inakuwaje leo hawapati faida kama michanga ile haina maana, kila jambo lina mwanzo na mwisho. Tulifanya makosa sasa turekebishe," alisema.


JPM AZINDUA MIRADI

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji, Rais Magufuli aliishukuru serikali ya India kwa kuiamini Tanzania na kutoa zaidi ya sh. bilioni 600, ambazo zitahusisha kupeleka maji katika mkoa wa Tabora na vijiji vyake, mji wa Nzega na Igunga. 

"Hii ni historia kwetu, hasa kwa wana Tabora, ambapo tatizo la maji limekuwa ni kubwa, lakini kwa ushirikiano wa nchi ya Tanzania na marafiki zetu India, wameamua kutupa fedha katika miradi ya maji nasi tukaamua maji haya yaje Tabora," alisema.

Pia, aliwaomba makandarasi kutoka India na washauri, kusimamia vizuri mradi huo ili uweze kukamilika kwa muda muafaka.

"Nina imani kuwa, mtaumaliza huu mradi haraka ili watu wetu waanze kutumia maji haya," alisema.

Awali, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge alisema mradi huo wa maji kutoka Ziwa Victoria, unatekelezwa na Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya India.

Mhandisi Lwenge alisema mradi huo,  ambao utahudumia miji ya Tabora, Nzega na Igunga, umegharimu sh. bilioni 600.

Naye, Balozi wa India nchini Tanzania, Sandeep Arya, alifurahishwa na uzinduzi wa mradi huo, ambao utatatua kero ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo.

Alisema mradi huo ni kielelezo bora cha urafiki kwa Tanzania na India. "Tuna mipango mingine ya ushirikiano na serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya maji," alisema.

Kuhusu ufunguzi wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora, alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuongeza ukubwa wa jengo la kusubiria abiria ili liweze kuchukua watu 500 badala ya 50 kama ilivyo sasa.

"Nimeambiwa jengo lililopo hapa linachukua watu 50. Nataka mjenge jengo la kutosha watu 500. Na Waziri ikiwezekana uanze mwaka huu. Nafahamu kuna fedha za European Union kupitia benki yake ya uwekezaji , mzitumie fedha hizo za mkopo kujenga jengo kubwa," alisema.

Pia, alimuagiza waziri huyo kuongeza ukubwa wa uwanja huo na kuwa kilometa 2.5, badala ya 1.9, ili ndege kubwa na ndogo ziweze kuutumia uwanja huo.

"Huku ni kilomita 1.9 na upande mwingine ni kilomita 1.2, muongeze kuanzia kilomita 2.5, badala ya kilomita 1.9, ili ndege kubwa ziwe zinatua, tusitengeneze uwanja ambao unatua Bombadier," alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alizifungua barabara za kutoka Tabora-Nyaua, Nzega-Tabora (km 114.6) zilizojengwa kwa kiwango cha lami. 
Baada ya kufungua, Rais Magufuli, aliwaomba wananchi wa Tabora kuzitunza barabara hizo na madereva wasizidishe migizo ili zisiharibike.

Pia, aliwapongeza wananchi wa Tabora kwa kuwachagua wabunge wazuri ambao wanaendana na kasi yake.

No comments:

Post a Comment