Tuesday 25 July 2017

DK. MAHIGA: HATUJAINGILIA UCHAGUZI MKUU WA KENYA


ZIKIWA zimesalia siku 13, kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Kenya, Serikali ya Tanzania imekanusha kuingilia kwa namna yoyote uchaguzi huo kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa kwenye vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alisema jana, mjini Dar es Salaam, kuwa Tanzania haijawahi na haitajihusisha kuingilia uchaguzi wa nchi yoyote duniani, ikiwemo Kenya, ambayo ni majirani na marafiki wa muda mrefu.

Alisema tofauti na inavyoripotiwa na kuelezwa kupitia baadhi ya vyombo vya habari vya Kenya, Tanzania inaliombea taifa hilo kufanya uchaguzi kwa amani na kwamba, inasubiri kwa hamu kubwa matokeo yake.

Waziri Dk. Mahiga alisema hakuna kituo wala mitambo ya kunasa matokeo ya uchaguzi wa Kenya hapa nchini na kwamba, anachukua dhamana  ya Serikali ya Tanzania katika suala hilo na kama kuna baadhi ya watu wana mpango wa kufanya utundu kutoka Tanzania, watawanasa.

"Hatuthubutu kuingilia uchaguzi wa nchi yoyote, jukumu lote linawahusu wao na ifahamike Kenya haijawahi kutuingilia na sisi hatutafanya hivyo. Kama kuna mtu au watu watajaribu kufanya hivyo kutokea hapa nchini, tutawabaini na kuwashughulikia, vyombo vyetu viko macho," alisema.

Kauli hiyo ya Waziri Dk. Mahiga, imekuja siku moja baada ya vyombo vya habari vya Kenya, kudai kuna kituo cha kuhesabia kura kinachomilikiwa na muungano wa NASA, kipo eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, kitakachofanya kazi sawa na ile ya Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC).

Mbali na hilo, Balozi Mahiga alisema siku mbili zilizopita, alikuwa jijini Nairobi, alikokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Kenya, Balozi Amina Mohamed, ili kutekeleza agizo la Marais Dk. John Magufuli na Uhuru Kenyatta.

Alisema maagizo ya wakuu hao wa nchi, yalikuwa ni kuujulisha umma wa nchi zote mbili kuhusu makubaliano yao ya kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizo mbili, vilivyowekwa kwa takriban miezi mitatu sasa tangu Aprili, mwaka huu.

"Marais wetu baada ya kukutana na kuzungumza, walikubaliana kuondoa vizuizi vyote vya kibiashara vilivyoweka hivi karibuni baina ya nchi hizo, kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo na kujali manufaa mapana ya Jumuia yetu ya Afrika Mashariki.

"Katika mkutano wao, Kenya walikubali kuondoa vikwazo kwa bidhaa za unga wa ngano na gesi ya kupikia kutoka hapa nchini huku Tanzania ikikubali kuondoa vikwazo vya bidhaa za maziwa na sigara zinazozalishwa nchini Kenya," alisema.

Waziri huyo pia alisema nchi hizo zimekubaliana kuondoleana vikwazo vyovyote, ambavyo vinaweza kuathiri biashara ya bidhaa na huduma ili kuongeza upatikanaji wa masoko na kuongeza ubunifu na ushindani wenye usawa baina ya wananchi wa pande hizo mbili.

Katika kuhakikisha makubaliano hayo yanadumu, Waziri Mahiga alisema Rais Dk. Magufuli na Uhuru Kenyatta, wameagiza kuundwa kwa tume ya pamoja itakayokuwa na jukumu la kuepusha tofauti za kibiashara zinazoweza kuibuka tena baina ya nchi hicho mbili.

Alisema tume hiyo imetakiwa kuongozwa na mawaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Kenya na Tanzania, huku wajumbe wakiwa ni mawaziri wa nchi hizo wanaohusika na masuala ya Jumuia ya Afrika Mashariki, Biashara, Fedha, Mambo ya Ndani ya Nchi, Kilimo, Uchukuzi na Utalii.

"Mawaziri hawa wataunda mfumo wa kupeana taarifa za mara kwa mara kuhusu masuala yenye changamoto za kibiashara kwa lengo la kuepusha kujirudia kwa tofauti kama hizi zilizokuwepo kwa muda mfupi uliopita," alisema.

Hivi karibuni, Kenya iliweka vikwazo kwa baadhi ya bidhaa za Tanzania kuingizwa nchini humo, ambapo Tanzania ilifanya jitihada za kulimaliza tatizo hilo bila mafanikio, hivyo kulazimu marais wa nchi hizo kukutana na kufanya mazungumzo yaliyozaa matunda.

No comments:

Post a Comment